Sugu, Dk Tulia ni jino kwa jino Mbeya Mjini

Mbeya. Wakati Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson akieleza utayari wake kukabiliana na yeyote kwenye uchaguzi mkuu ujao, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema wakutane mwaka 2025.

Kauli za wanasiasa hao zimeendelea kuchochea joto la uchaguzi mkuu ujao, hasa ikichagizwa na Dk Tulia, ambaye ni Spika wa Bunge, kuwasilisha maombi serikalini akiomba jimbo hilo kugawanywa kutokana na ukubwa wake kwa kuwa na kata 36.

Hata hivyo, hivi karibuni Dk Tulia alinukuliwa na vyombo vya habari akisema anayetaka kuchuana naye aende kupima kina cha maji kama kinamtosha katika uchaguzi mkuu ujao.

Mei 4 mwaka huu akizungumza katika mahojiano maalumu na Kituo cha Redio cha Wasafi, Dk Tulia alizungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa, ikiwemo mgawanyo wa jimbo lake pamoja na kile kilichoelezwa kutaka kumkimbia mpinzani wake.

“Ubunge wangu haijalishi jimbo limegawanywa au halijagawanywa, mimi ndiye mbunge, kama nilimtoa mtu katika kata 36, ataweza kunitoa kata zikiwa chache kweli? Mbona itakuwa mtihani, zikibaki kata 36 nitawafyeka.

“Nisingeshangaa kujadiliwa na wao, tena napenda sana wao wameanzisha huo mjadala, nimefurahi na wanaposema watanifuata, nataka wajipime kama wanaona kina cha maji kinawatosha waje, kama niliwatoa na kata 36 wataniweza wapi na kata chache,” alihoji Dk Tulia.

Katika mahojiano hayo, Spika aliulizwa kama hatishiki kukabiliana na Sugu katika uchaguzi ukiwa huru na haki, hasa ikizingatiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, wapinzani wengi waliamini kuna nguvu ya ziada ya dola iliyotumika kuwabeba washindi.

“Sihofii kupambana naye, niko vizuri, sina wasiwasi na hilo, naomba Mungu aniweke. Nimefanya kazi kubwa, nyie nendeni Mbeya Mjini mtaamini,” alieleza Dk Tulia, katika mahojiano hayo yaliyofanyika katika makazi rasmi ya Spika jijini Dodoma.


Sugu ajibu

Katika mikutano yake miwili jijini hapa aliyofungua juzi katika kata za Nzovwe na Igawili, Sugu alianza kwa kuwashukuru wananchi, akisema walimpa kura za kutosha lakini utawala wa awamu ya tano uliamua ulivyotaka.

Sugu alisema hoja ya kugawanywa jimbo hilo kwake halielewi kitaalamu, akifafanua kuwa akiwa mbunge aliweza kuhudumia kata zote 36 bila tatizo.

Alisema pamoja kutofahamu mambo ya kitaalamu kwenye mgawanyo wa jimbo hilo, iwapo itabidi kuwa hivyo kwake ni sawa, lakini isimfanye mpinzani wake kuhamaki na uchaguzi mkuu ujao 2025 na kwamba wakutane aone kama atapita.

“Watu wameniuliza kuhusu kugawa jimbo, mimi sijui mambo ya kitaalamu, lakini mimi nilikuwa nahudumia vizuri kata zote, ila ikibidi kugawanywa ni sawa tu, ila aje tukutane 2025 tuone kama atapita hata kwa kupata kura 2,000,” alisema.

“Ameanza kupaniki (kuhamaki) kwa sababu anafahamu hakuna kazi aliyoifanya jimboni zaidi ya kugawa mikopo na kuwasumbua wananchi na kuleta muziki na wasanii tu, ieleweke kwamba mimi nalitaka jimbo la Mbeya Mjini,” alisema.

Aliongeza: “Tunakusubiri, tunakusubiri tunakusubiri…tunaamini uchaguzi ujao utakuwa wa huru na haki, kwa sasa jiji ni chafu, licha ya wananchi kutozwa fedha za taka, enzi zangu tulipata hati na zawadi ya jiji safi,” alisema Sugu.

“Tuliumizwa sana kwenye utawala wa awamu ya tano, sisi tumesamehe ila hatuwezi kusahau, ndiyo maana hadi leo tunaendelea kuongea kutokana na machungu ya miaka sita tuliyopitia.

“Mimi ni mzaliwa wa hapa Sae, Mbeya, shule ya msingi na sekondari nimesoma hapahapa, nimeuza mitumba pale Mwanjelwa, nikafanya shughuli za muziki hapahapa ila sikuwahi kupelekwa gerezani tofauti na nilipoingia kwenye siasa.’’


Wachambuzi wanasemaje?

Mchuano huo unamwibua mchambuzi wa siasa na mkufunzi msaidizi katika Chuo Kikuu cha Teofil Kisanji (Teku) Mbeya, Walfogang Patrick, aliyesema kutokana na mnyukano wa wanasiasa hao, ushawishi wa mtu binafsi na hoja zenye mashiko, ndizo zitakazoamua hatima yao kwenye uchaguzi ujao.

Alisema amekuwa mfuatiliaji wa mikutano ya hadhara kwa pande zote na kuona mwitikio wa wananchi, lakini kwa upande wa Sugu aliona tofauti, kwani licha ya kutokuwa mbunge kwa sasa lakini alionekana kuwavuta wananchi wengi.

“Kuna ushawishi wa mtu na hoja zake, ukizingatia uchaguzi ujao tunatarajia kuwa huru na haki, hivyo mtu atapigiwa kura na mshindi kupatikana tofauti na kile kilichotokea 2020,” alisema Patrick.

Kuhusu hoja ya kuligawa jimbo, msomi huyo wa masuala ya jiografia alisema haoni sababu za kuligawa jimbo hilo, labda kama kuna maslahi ya kisiasa ndani, kwani jiji la Mbeya watu wake wanafikika.

“Labda ingekuwa Mbeya vijijini, naweza kukubaliana na mgawanyo wake kwa kuwa watu wamegawanyika sehemu tofauti kuliko Mbeya mjini, labda kama mtu anataka kupima eneo wanapomkubali ili agombee huko,” alisema mchambuzi huyo.

Kwa upande wake, Dk Onesmo Kyauke alisema ukiyaweka kando matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uliokuwa na changamoto mbalimbali, jimbo la Mbeya mjini ni gumu, hasa kama utafanyika uchaguzi huru na wa haki.

"Uchaguzi wa mwaka 2025 utakuwa mgumu endapo utafanyika kwa uhuru na haki kwa sababu ule wa mwaka 2020 ulikuwa na vitisho, ndio maana upinzani ulipoteza majimbo ambayo kwa kawaida huwa wanashinda. Nadhani uchaguzi wa mwaka 2025 utakuwa wa tofauti kutokana na haya mabadiliko yanayoendelea, ikiwemo mifumo ya uchaguzi," alisema Dk Kyauke ambaye ni mwanasheria kwa taaluma.

Dk Kyauke alisema uchaguzi mkuu ujao ukiwa huru na haki, hata mapambano yatakuwa na usawa, akisisitiza Mbeya Mjini ni jimbo gumu.

Katika uchaguzi uliopita Dk Tulia kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) aliibuka mshindi kwa kupata kura 75,225 huku mpinzani wake Sugu akiambulia kura 37,591. Hata hivyo Sugu alililamikia uchaguzi huo kugubikwa na dosari hivyo kudai kutokuwa huru na haki.