Tanzania kupeleka misaada Malawi, Balozi Polepole asema

Balozi Humphrey Polepole anayeiwakilisha Tanzania nchini Cuba.

Muktasari:

  • Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepeleka msaada wa chakula na vifaa vya kujihifadhi na kujiokoa raia katika changamoto ya kimbunga Freddy nchini Malawi ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limepeleka msaada wa chakula na vifaa vya kujihifadhi na kujiokoa raia katika changamoto ya kimbunga Freddy nchini Malawi.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Kimbunga hicho kilipiga eneo la Kusini mwa Afrika kwa mara ya pili ndani ya mwezi mmoja mwishoni mwa wiki na bado kiliendelea kusababisha mvua kubwa zilizoathiri juhudi za kutoa misaada.

Hadi kufikia juzi, idadi ya waliofariki dunia ilikuwa imeongezeka kutoka 190 hadi 225 huku 707 wakijeruhiwa kama ilivyothibitishwa na Idara ya usimamizi wa majanga nchini humo.

Kutokana na changamoto hiyo, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa JWTZ, Luteni Kanali Gaudentius Ilonda jana Jumamosi, Machi 18, 2023 katika taarifa yake kwa umma alisema tayari jeshi hilo limesafirishaji nchini humo tani 1,000 za unga, mahema 50, Blanketi 6,000 pamoja na Helkopita mbili zitakazotumika katika maafa hayo.

“Baadhi ya magari yataondokea Dodoma yakiwa yamebeba shehena hizo, lakini pia kuna shehena ya tani 60 za unga Iringa zitaondoka kila siku kuelekea Malawi,”amesema Kanali Ilonda.

Akishiriki mapokezi ya ndege hizo jana, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Humphrey Polepole alisema kutokana na mahusiano ya karibu kati nchi hizo hususani kijamii, changamoto yoyote ya Malawi itawagusa Watanzania moja kwa moja. Alifafanua misaada mingine iko njiani inaelekea nchini humo.