Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchaguzi huru na wa haki, msingi wa demokrasia

Uchaguzi ni njia ya msingi ya kidemokrasia inayotumiwa na kundi la watu, jamii au taifa kuchagua viongozi wanaoaminiwa kuwa bora kwa kipindi fulani, kwa mujibu wa katiba au makubaliano ya pamoja, iwe kwa maandishi au kwa kauli.

Hata hivyo, kuwa na uchaguzi pekee hakutoshi; uchaguzi lazima uwe huru na wa haki. Wakati mwingine, jamii hukubaliana juu ya namna ya kuendesha uchaguzi, lakini utekelezaji wake hauakisi makubaliano hayo.

Katiba ya Zanzibar inaeleza kuwa uchaguzi uendeshwe ndani ya siku moja, lakini sheria imewekwa kuruhusu uchaguzi kufanyika kwa siku mbili. Baadhi ya wanasheria wanaona kuwa sheria yoyote inayokinzana na Katiba ni batili.

Ingawa imeelezwa kuwa mabadiliko hayo yamefanyika kwa nia njema, suala kuu linabaki kuwa je, waliowafanya walikuwa na mamlaka ya kikatiba kufanya hivyo? Wanaopinga pia wanafanya hivyo kwa nia njema kudai heshima ya Katiba.

Uchaguzi ni mchakato mrefu, na ubora wake haupimwi tu siku ya upigaji kura. Vigezo vya uchaguzi huru na wa haki vinahusisha mchakato mzima, kutoka katika sheria, maandalizi, hadi utekelezaji.

Pale ambapo kasoro hutokea, uhalali wa uchaguzi hubadilika, kama nguo iliyochafuka au kufunikwa kwa kiraka.

Sheria bora na Tume huru ya uchaguzi ni masharti ya msingi ya uchaguzi wa haki. Hata hivyo, kuna wasiwasi mkubwa kutokana na uteuzi wa maofisa wa tume wanaodaiwa kuhusika na kasoro za uchaguzi wa 2020, na sasa wameteuliwa tena kusimamia uchaguzi ujao.

Zimesikika taarifa za baadhi ya wananchi, wakiwemo waliowahi kuwa wabunge, mawaziri, na hata wale ambao hawajawahi kutoka Zanzibar tangu kuzaliwa, kunyimwa haki ya kujiandikisha kama wapigakura, wakati wengine wanaodaiwa kuwasili visiwani mwaka huu wanapatiwa haki hiyo.

Wakati viongozi wanahamasisha watu kujiandikisha, wameshindwa kulaani wazi kunyimwa kwa haki hiyo kwa wengine.

Ingawa kura ya mtu ni siri yake, dalili zinaonesha kuwa mazingira ya sasa yanatishia usiri huo. Katika chaguzi zilizopita, wafanyakazi wa vyombo vya Serikali, idara za Serikali na mashirika ya umma walilazimika kuwasilisha kadi zao za kupiga kura kwa waajiri wao.

Jambo hili ingawa lilifanyika kwa siri, lililalamikiwa na watumishi na vyama vya upinzani kwa kuwa lilitafsiriwa kama njia ya kuwashinikiza watu kupiga kura kinyume na matakwa yao.

Utaratibu wa kutumia kadi zenye nambari ambazo zinaweza kufuatiliwa unahatarisha dhana ya siri ya kura.

Katika chaguzi zilizopita, watumishi wengi wa Serikali, hasa walimu, walifukuzwa kazi au kupoteza haki zao kwa madai ya kutokuwa waaminifu kwa Serikali.

Kwa sasa, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Kitwana Mustafa, ameweka wazi jambo lililokuwa likifanyika kwa siri, kwa kuitisha mkutano na kuagiza wafanyakazi wa Serikali na taasisi za umma kuwasilisha kadi zao za kupiga kura.

Alieleza kuwa anataka kuhakikisha wote wamejiandikisha na akatumaini kuwa wataonesha imani yao kwa Serikali katika uchaguzi ujao.

Hata hivyo, mamlaka hayo ya Mkuu wa Mkoa yanazua maswali, kwani kwa mujibu wa sheria, kadi ya kupiga kura ni mali ya mpiga kura na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ndio yenye mamlaka ya kuidhibiti, si mtu mwingine yeyote.

Kwa mtazamo huu, hali ya uchaguzi huru na wa haki inazidi kufifia. Mkuu wa Mkoa anapaswa kutambua kuwa Zanzibar haina sheria inayolazimisha mtu kujiandikisha kupiga kura. Hii ni hiari ya mtu binafsi.

Na hata mtu akijiandikisha, bado ana uhuru wa kupiga kura au kutopiga au hata kuharibu kura, kama ilivyoshuhudiwa katika “kura za maruhani” huko Pemba.

Cha kusikitisha ni kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar haijatoa tamko lolote kuhusu hali hii, kana kwamba kuna Tume nyingi visiwani, zikiwemo za Wakuu wa Mikoa. Swali la kujiuliza: Kwa nini hali hii haitokei Bara?

Kuna nini Visiwani kinachopelekea vitendo vya ajabu kuelekea uchaguzi?

Iwapo nia ya Mkuu wa Mkoa ni kuongeza idadi ya wapigakura, basi angetumia nafasi yake kuhakikisha wale waliokataliwa kujiandikisha wanapewa haki yao.

Kisingizio cha “nia njema” kisiwe sababu ya kuchafua mazingira ya uchaguzi. Mwelekeo wa sasa unaibua wasiwasi kuhusu uwepo wa uchaguzi huru na wa haki.

Ni muhimu Katiba na sheria ziheshimiwe, na watu wapewe uhuru wa kupiga kura bila hofu wala vitisho.

Mungu aiwezeshe Zanzibar kuvuka salama katika uchaguzi ujao.