Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usiyoyafahamu kuhusu uchaguzi Afrika Kusini

Johannesburg. Wananchi wa Afrika Kusini leo Jumatano, Mei 29, 2024 wanafanya uchaguzi kuchagua wabunge ambao baadaye watamchagua Rais wa nchi hiyo.

Afrika Kusini inafuata mfumo wa uchaguzi wa Kibunge (Parliamentary System) unaolipa Bunge nguvu ya kumchagua Rais aliyependekezwa na chama husika.

Chama kinachopata wabunge wengi ndiyo kinapewa nafasi kubwa ya kutoa Rais wa nchi hiyo, lakini kama chama hakitafikia wastani wa asilimia 50 ya viti bungeni, kitalazimika kutengeneza muungano na chama kingine ili kuunda Serikali ya pamoja.

Mfumo huu ni tofauti na ule unaotumiwa na mataifa mengi dunia ikiwemo Tanzania wa ‘anayepata kura nyingi ndiyo mshindi’ na ambao wadau wengi wamekuwa wakiulalamikia kwa madai kuwa hautoi uwakilishi wa haki kwenye chaguzi.


Mshikemshike kila kona leo

Waafrika Kusini wanapiga kura leo katika uchaguzi muhimu zaidi tangu mfumo wa ubaguzi wa rangi kumalizika mwaka 1994.

Zaidi ya watu milioni 27 wamejiandikisha kupiga kura huku ikitarajiwa kuongezeka kwa mgawanyiko wa kisiasa baada ya miaka 30 ya demokrasia.
Vyama 70 vilivyosajiliwa na wagombea binafsi 11 wanashiriki katika uchaguzi huo ambapo, watapigia kura bunge jipya na mabunge tisa ya majimbo.

"Ukuaji mkubwa wa vyama unaonyesha kukatishwa tamaa na vyama vikubwa vya zamani au wakosoaji wanaweza kusema, watu wanatafuta fursa ya kuingia bungeni na kulipwa pensheni," mchambuzi wa siasa, Richard Calland ameiambia BBC.

Kikiwa madarakani tangu aliyekuwa akiongoza mapambano ya kupinga ubaguzi wa rangi, Nelson Mandela aliposhinda uchaguzi mwishoni mwa utawala wa Wazungu wachache, Chama cha African National Congress (ANC) kinawania muhula wa saba madarakani.

Ingawa kina uhakika wa ‘ushindi wa uhakika’, kura za maoni zimekuwa zikipendekeza mara kwa mara kuwa chama hicho kitapoteza wingi wake wa wabunge kwa mara ya kwanza na kukilazimisha kuingia katika muungano na chama kimoja au zaidi cha upinzani.

"Tunaingia katika awamu inayofuata ya demokrasia yetu na itakuwa ni mpito mkubwa," Profesa Calland ameliambia BBC.

"Tutakuwa na  demokrasia yenye ushindani na kukomaa zaidi, au siasa zetu zitasambaratika zaidi," ameongeza.

Kampeni hiyo imetawaliwa na ufisadi ulioenea serikalini, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana, kuzorota kwa huduma za umma na uhalifu uliokithiri.
Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kimetia saini mkataba na vyama vingine 10, vikikubali kuunda Serikali ya mseto iwapo vitapata kura za kutosha ili kukiondoa ANC madarakani.

Lakini hili haliwezekani sana, ANC kinatarajiwa kubaki kuwa chama kikubwa zaidi, na kukiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza muungano. Ilipata asilimia 57.5 ya kura katika uchaguzi uliopita ikilinganishwa na asilimia 21 ya DA.

Rais wa zamani, Jacob Zuma alisababisha mshituko mkubwa alipotangaza Desemba 2023 kwamba anaachana na ANC na kufanya kampeni kwa ajili ya chama kipya, Umkhonto weSizwe (MK), ambacho kinatafsiriwa kama mkuki kwa taifa.

Ingawa amezuiwa kugombea ubunge kwa sababu ya kukutwa na hatia ya kudharau mahakama, jina lake bado litaonekana kwenye karatasi ya kura kama kiongozi wa MK.

Kura za maoni zinaonyesha MK kitapata takribani asilimia 10 ya kura. Inatarajiwa kufanya vyema hasa katika jimbo lake la KwaZulu Natal, ambako hali ya wasiwasi imekuwa juu, huku baadhi ya matukio ya vurugu yakiripotiwa wakati wa kampeni.

"Uchaguzi  KwaZulu Natal unaweza kuwa wa fujo sana, tutarajie mizozo mingi na ushindani kuhusu matokeo," Profesa Calland amesema.

Wanawake ni asilimia 55 ya wapigakura waliojiandikisha  karibu milioni 15, kulingana na takwimu zilizotolewa na tume ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa kundi la umri, usajili wa wapigakura ni wa juu zaidi kati ya wale walio na umri wa miaka 30 hadi 39, ambapo wanafikia  takribani milioni saba kati ya wapigakura milioni 26.7.
Lakini, Profesa Calland amesema karibu wapigakura milioni 13.7 waliotimiza masharti ya kupiga kura hawakujiandikisha, huku wengi wao  wanaofikia karibu  milioni nane wakiwa chini ya umri wa miaka 30.

"Wameipa mgongo demokrasia yetu changa. Dhana ni kwamba wamepoteza matumaini, wanahisi kutengwa kiuchumi na kuona hakuna upinzani wowote," ameongeza.