Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UVCCM watolewa ukumbini Simiyu

Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa CCM mkoa wa Mara wakiwa wamesimama kwenye jukwaa kuu kwaajili ya kupiga kura, wajumbe hao wamelazimika kujipanga jukwaa kuu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Picha na Beldina Nyakeke

Bariadi. Wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kupitia Umoja wa Vijana UVCCM wameondolewa ukumbini baada ya matokeo ya uchaguzi uliowaingiza madarakani kufutwa.

Uamuzi wa kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Simiyu umetangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Novemba 21, 2022.

Kwa mujibu wa mtendaji huyo mkuu wa CCM, matokeo ya uchaguzi huo yamefutwa kutokana na uwepo wa viashiria vya vitendo vya rushwa.

Uchaguzi wa UVCCM Mkoa wa Simiyu ulifanyika Novemba 16, mwaka huu.

Muda mfupi baada ya tangazo hilo, ndipo wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Mkoa wa Simiyu kupitia UVCCM ambao tayari walikuwa ukumbini wakajikuta wakiamuriwa kutoka nje ya ukumbi kutokana na kukosa sifa.

Walioamriwa kutoka ukumbini aliyeshinda nafasi ya uenyekiti wa UVCCM Mkoa, mjumbe wa Baraza Kuu la vijana mkoa na mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa kupitia kundi la vijana.

Tangazo la kuwataka wajumbe hao kutoka ukumbini na kwenda kusimama umbali wa mita 200 lilitolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mohamed Ally.

"Viongozi wote wa UVCCM waliochaguliwa kupitia uchaguzi uliofutwa siyo wajumbe halali katika mkutano huu na wanatakiwa kutoka nje ya ukumbi," amesema Ally kupitia tangazo hilo.

Mkutano mkuu wa CCM Mkoa wa Simiyu unaendelea mjini Bariadi kuchagua viongozi watakaokiongoza chama hicho hadi mwaka 2027.

Pamoja na nafasi ya uenyekiti wa mkoa, wajumbe wa mkutano huo unaosimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila pia watamchagua mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), wajumbe wa Halmashauri Kuu Mkoa na wawakilishi wengine katika vikao vya chama na jumuiya zake.