Wanavyoizungumzia Siku ya Kimataifa ya Demokrasia

Muktasari:
- Siku ya Kimataifa ya Demokrasia huadhimishwa kila Septemba 15 ya kila mwaka ambapo ulimwengu hutafakari umuhimu wa demokrasia katika maisha ya binadamu na namna inavyochochea maendeleo.
Dar es Salaam. Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia ambapo baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wametoa jumbe zao kuhusiana na siku hii ikiwemo kuhimiza kuzingatiwa kwa demokrasia nchini.
Siku ya Kimataifa ya Demokrasia huadhimishwa kila Septemba 15 ya kila mwaka ambapo ulimwengu hutafakari umuhimu wa demokrasia katika maisha ya binadamu na namna inavyochochea maendeleo.
Maadhimisho hayo kwa mwaka 2024 yamekuja wakati zaidi ya nchi 50, zinazowakilisha nusu ya idadi ya watu duniani, zinafanya uchaguzi ili kupata viongozi.
Hapa nchini, watu mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu siku hii ikiwemo ubalozi wa Marekani hapa Tanzania ambao umeandika katika ukurasa wake rasmi wa X:
“Leo tunasherehekea Siku ya Demokrasia kwa kutambua umuhimu wake katika kuendeleza amani, ujumuishi na haki duniani kote. Demokrasia inawapa watu mamlaka. Tuhakikishe sauti za kila mtu zinasikika na kuheshimiwa. Jiunge nasi katika kuhamasisha demokrasia shirikishi.”
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) Zanzibar, kupitia ukurasa wa X kimeandika: “Wadau wote tunatakiwa tuungane kuweka ajenda zetu pamoja. Msajili wa vyama vya siasa akipewa ripoti ya vyama ni lazima akague namna vyama hivyo vinasaidia kuwaimarisha wanawake.”
Jana, mbunge wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka alisisitiza umuhimu wa kuwa na mgombea binafsi kama njia ya kupanua demokrasia kwa kuruhusu wananchi kuwachagua watu wanaowataka na siyo vyama.
Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) umesema Siku ya Kimataifa ya Demokrasia ilianzishwa kupitia azimio lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2007 likihimiza Serikali kuimarisha demokrasia.
“Tunawahimiza wabunge wetu wote kuadhimisha siku hii kwa matukio na sherehe. Tangu siku hiyo ilipoadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2008, mamia ya matukio ya bunge yamefanyika duniani kote.
“Haya yamejumuisha mashindano ya picha, warsha kwa watoto, mijadala ya moja kwa moja ya televisheni, simu za redio na mikutano na mashirika ya kiraia,” imeeleza IPU.
Umoja wa Ulaya umeeleza kudhamiria kuimarisha na kulinda demokrasia, ndani na nje ya mipaka yake.
Mwaka huu, mamilioni ya watu duniani wanarejea tena ahadi yao kwa demokrasia, iwe kama wagombea au wapiga kura, mara nyingi katika hali ngumu.
“Muungano wa Ulaya unapongeza wale wanaolinda demokrasia, mara nyingi kwa hatari kubwa. Kulinda demokrasia ni muhimu ili kuhifadhi na kukuza heshima ya kila raia, pamoja na kukuza haki za kijamii, maendeleo jumuishi na amani.”
“Katika maeneo mbalimbali, wananchi wanakutana na vitisho na juhudi za kudhoofisha mchakato wa kidemokrasia, kama vile vurugu za kisiasa, udanganyifu wa uchaguzi, ulaghai, matumizi mabaya ya rasilimali za serikali, upotoshaji wa habari, au kuingilia kati kutoka nchi za kigeni. Vitendo hivi vinadhuru uadilifu wa uchaguzi na msingi wa demokrasia,” imeeleza taarifa ya EU.
EU, kupitia matumizi ya Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi na zana nyingine za kusaidia demokrasia, inafanya kazi kutambua, kuzuia na kutoa mapendekezo kuhusu masuala haya ili kuruhusu na kuhamasisha ushiriki wa moja kwa moja katika uchaguzi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres amesema siku hii: “Ni fursa ya kusisitiza umuhimu wa kuzingatia uhuru wa kujieleza, uhuru wa raia, utawala wa sheria, kuhakikisha taasisi zinazowajibika zinalinda na kukuza haki za binadamu.”