Watatu wateuliwa kugombea Muhambwe

Sunday April 04 2021
wagombea pic

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Muhambwe, Diocles Lutema alipokuwa akitangaza vyama ambavyo havitagombea ubunge kutokana na kushindwa kukidhi vigezo

By Mwandishi Wetu

Kibondo. Vyama sita vya siasa kati ya 10 vilivyokuwa vimechukua fomu kugombea  nafasi ya ubunge Jimbo la Muhambwe wilayani Kibondo vimeondolewa katika mchakato huo kutokana na kushindwa kukidhi vigezo vya vilivyowekwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa.

Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Muhambwe, Diocles Lutema alipokuwa akiwatangazia wagombea,  amevitaja vyama hivyo ni UPDP,CCK, Demokrasia Makini,ADC,SAU na AAFP huku Chauma, kikishindwa kurudisha fomu  na kueleza kuwa vyama vilivyokidhi vigezo ni vitatu ambavyo ni CCM, DP na ACT Wazalendo

Lutema amesema wagombea walitolewa kwenye mchakato wameshindwa kutimiza mashariti kwa kukosa wadhamini, kulipa fedha Sh 50,000 za dhamana na wengine kushindwa kuwasilisha picha zao hivyo kutokana na maelekezo ya tume wameamua kuwaondoa ili vibaki vyama na wagombea waliokidhi vigezo.

Wagombea walioenguliwa ni Shabani Itutu wa chama cha ADC, Tulisubya Mugana wa UPDP, Mohamed Juma Haji wa Demokrasia Makini, Rehema Rabia (CCK), Yunis Masanja (SAU) na Luti Ally (AAFP) huku mgombea wa Chauma, Benard Ngarama akishindwa kurudisha fomu.

Walioteuliwa na tume hiyo ni Florence Samizi wa CCM, Julius Masabo wa ACT Wazalendo na Filipo Fumbo wa DP.

Kwa upande wao, baadhi ya wagombea wa vyama vilivyoenguliwa katika mchakato huo, ambao ni Shabani Itutu kupitia ADC, na Mohamed Juma wa Demokrasia Makini wamesema walifuata maelekezo yote na kuyatimiza hivyo wameonewa na watakata rufaa

Advertisement

Nao wagombea kupitia vyama vya CCM, Dk Samizi na Masabo wa ACT Wazalendo wamewataka watu wa Muhambwe kushiriki katika kampeni ili waweze kusikiliza sera za vyama hivyo.

Advertisement