Ziara ya Makonda ilivyogeuka mwiba kwa watendaji

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Maswa mkoani Simiyu baada ya kupokelewa mkoani humo katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20. Picha na CCM

Ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda imekuwa kaa la moto kwa watendaji wa Serikali, hasa wakurugenzi wa halmashauri ambao wanahusika moja kwa moja na usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Makonda alianza awamu ya kwanza ya ziara yake Januari 19, mwaka huu, akiita ziara hiyo “back to back” na anatarajia kutembelea mikoa 20 akikagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020.

Mpaka sasa, tayari ametembelea mikoa 10 ambayo ni Simiyu, Tabora, Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida na Shinyanga, huku akitarajia kuendelea na ziara hiyo katika mikoa mingine 10 iliyobaki.

Katika ziara hiyo, Makonda amekuwa akiwaweke kitimoto watendaji wa Serikali kwenye maeneo anayokwenda baada ya kusikiliza kero za wananchi na kukuta utekelezaji wa miradi ya maendeleo ukisuasua au viongozi hao kulalamikiwa na wananchi.

Makonda anasema CCM ipo kwenye maabara ya kupima utendaji kazi wa watumishi waliopewa dhamana, lakini hawatekelezi majukumu yao kwa ufanisi, jambo alilodai linaleta uchonganisha kati ya wananchi na Serikali, hasa mkuu wa nchi, Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kama Idara ya Uenezi, staili yetu ni kutoka nje na kusikiliza kero za wananchi na kupima kama wale waliopewa dhamana wanatekeleza majukumu yao ipasavyo. Tunataka kupatiwa majibu papo hapo, yaani zege halilali,” anasema Makonda katika moja ya mikutano yake.

Baadhi ya wakurugenzi waliokuwa na wakati mgumu baada ya Makonda kufika kwenye maeneo yao ni Isaya Mbenje (Halmashauri ya Wilaya ya Pangani), Anderson Msumba (Manispaa ya Kahama) na Francis Namaumbo (Halmashauri ya Wilaya ya Hanang).

Wengine ni Anna Mbogo (Halmashauri ya Wilaya ya Babati), Michael Matomora (Halmashauri ya Wilaya ya Iramba) na Mwajuma Nasombe (Manispaa ya Moshi).

Mbali na wakurugenzi hao, pia wamo watendaji wengine waliobananishwa kwa kutotekeleza kikamilifu majukumu yao. Watendaji hao ni pamoja na waganga wakuu wa wilaya na mikoa pamoja na maofisa ardhi wa halmashauri.


DED asimamishwa

Akiwa Wilaya ya Pangani, Makonda alimuweka “mtu kati” Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Isaya Mbenje baada ya kubaini kuna changamoto lukuki zilizoshindwa kupatiwa ufumbuzi, huku bosi huyo akishindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Hilo lilibainika bada ya mwenezi huyo kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi waliodai kwamba Mbenje ameshindwa kutimiza majukumu yake ya kutatua kero zao.

“Wapo wafanyabiashara wanaiuzia halmashauri ya Wilaya ya Pangani malighafi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, lakini hawalipwi fedha zao, wakienda kwa mkurugenzi, ni mungu mtu,” anasema Makonda.

Simu ya Makonda kwa Bashe bei ya sukari

Kutokana na hilo, Makonda alimuagiza Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa akimweleza kuwa mapendekezo ya CCM ni kwamba Mbenje asimamishwe kazi na ipelekwe timu ya uchunguzi wa malalamiko dhidi ya mkurugenzi huyo.

Jambo hilo lilitekelezwa haraka na Waziri Mchengerwa aliyemuagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru kumsimamisha kazi kuanzia Januari 21, mwaka huu, kwa kushindwa kutimiza majukumu yake ipasavyo.


Mkurugenzi Moshi matatani

Akiwa Moshi, Makonda alimbana mkurugenzi wa manispaa, Mwajuma Nasombe akimtaka aeleze sababu za kusuasua kwa ujenzi wa soko la samaki, stendi ya Ngangamfuni na kero ya kodi kubwa kwenye maduka.

Akijibu kero hizo, Nasombe alisema sababu za kuchelewa kwa ujenzi huo ulioanza mwaka 2019 na kutarajiwa kukamilika 2021, ni mkandarasi kucheleweshewa malipo yake, lakini sasa wametenga bajeti kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.

“Mkandarasi alicheleweshewa malipo, lakini baada ya changamoto hiyo tumeona manispaa tuwe na bajeti katika mapato yetu ya ndani ili wizara inapochelewa kulipa, basi tulipe wenyewe na mkandarasi asikwame. Tunaomba tupewe miezi sita baada ya mkandarasi kurudi eneo la kazi ili tukamilishe,” alisema.

Makonda anatema nyongo

Kuhusu suala la kodi kubwa iliyolalamikiwa na baadhi ya wafanyabiashara wa Moshi katika maduka ya stendi, walimuomba Makonda kuingilia kati kutatuta changamoto hiyo.

Makonda hakuchelewa, mara moja akaagiza Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi kuketi kando ya mkutano huo wa hadhara kujadili suala hilo na kutoa majibu papo hapo.

Baada ya kukaa kwa muda mfupi, Meya wa Moshi, Zuberi Kidumo alitoa taarifa akisema: “Tumekaa hapa kama ulivyotuagiza, vilio vya wananchi wa Moshi vinasikilizwa na maisha yao yanakwenda.

“Tulianza kuwasikiliza awali katika kodi ya Sh1 milioni tukashuka hadi Sh450,000, lakini kwa mujibu wa sheria, bajeti ikishapitishwa na Bunge huwezi kuibadilisha hadi tupate kibali kutoka kwa Katibu Mkuu,” alisema.

Kidumo alisema wamekubaliana na madiwani wenzake kwenda kubadilisha kwenye bajeti inayokuja, kwa kupunguza Sh50,000 kwa kila eneo kuanzia sakafu ya chini, ya kwanza hadi ya pili ili kuwapa unafuu wafanyabiashara.


Alipwa deni lake

Akiwa Magugu, Wilayani Babati Mkoa wa Manyara, Makonda alipokea kero ya mkazi wa eneo hilo, Odilia Mkama aliyekuwa akiidai halmashauri ya wilaya ya Babati Sh4.6 milioni alizoahidiwa kulipwa baada ya kupata zabuni ya chakula kwenye shule ya sekondari ya Dareda, lakini hakupewa kwa miaka nane.

Baada ya maelezo hayo, Makonda alimtaka Mkama kupanda kwenye gari la mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Anna Mbogo ili kwenda kupata fedha zake anazozidai.

Baada ya muda kidogo, Makonda alimuuliza Mbogo kama ameshamlipa mwanamke huyo fedha zake, ndipo bosi huyo wa halmashauri alijibu kuwa mkuu wa shule husika anafanya utaratibu wa kumlipa ingawa kwenye mfumo inahitaji namba yake ya benki na TIN.

“Nimewaambia, amenipa namba ya akaunti, vingine hajanipa,” anasema Mbogo.

Simu ya Makonda kwa Naibu Waziri Pinda

Makonda hakufurahishwa na maelezo hayo, akisema wanaweka ugumu wa mama huyo kupata haki yake. Hata hivyo, mkuu wa mkoa wa Manyara, Sendiga aliingia kati na kubeba jukumu hilo kwa niaba ya Serikali.

“Umetoa maelekezo, ni maelekezo ya chama. Serikali kazi yake ni kutekeleza maelekezo ya chama, nikuhakikishie huyu mama tunamlipa fedha zake, kama kuna taratibu nyingine za kiofisi ikiwemo ya kuandika TIN Namba, tutazifanya baadaye kwa sababu deni lake ni la muda mrefu,” alisema Sendiga. Kabla Makonda hajaondoka mkoani Manyara kwenda Singida, Mkama alikabidhiwa hundi ya Sh4.9 milioni na Sendinga, ikiwa na ongezeko la Sh300,000 za usumbufu alioupata kwa miaka hiyo aliyozungushwa.

Suala la kuchelewesha madeni lilimkabili pia mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Iramba, Michael Matomora ambaye anatakiwa kulipa Sh8 milioni inayodaiwa na chama cha kuweka na kukopa cha Chamwai, hata hivyo wamekuwa wakizungushwa kwa muda mrefu.

Kwa maelekezo ya Makonda, mkurugenzi alikutana na madiwani katika halmashauri hiyo na kuahidi kulipa deni hilo ndani ya siku 14, jambo ambalo liliridhiwa na kiongozi huyo akisisitiza viongozi kutimiza majukumu yao.


Si wakurugenzi pekee

Mbali na wakurugenzi watendaji wa halmashauri, pia watumishi wa sekta ya afya ni miongoni mwa watu waliojikuta katika mazingira magumu mbele ya Makonda, baada ya kubananishwa wakitakiwa kutoa majibu kwa ufasaha kuhusu huduma za afya na maendeleo ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati kwenye maeneo yao.

Mganga mkuu wa mkoa wa Tanga, Dk Japhet Simeo ni mmoja wa watumishi ambao hawatamsahau Makonda kwa namna alivyowekwa kitimoto kwenye mkutano wa hadhara, akitakiwa kutoa majibu kuhusu kuteseka kwa wananchi wanaokwenda kupata huduma hospitali ya Rufaa ya Bombo.

Mwingine ni mganga mkuu wa wilaya ya Maswa wilayani Simiyu, Dk Mpollo Adorat ambaye alitakiwa kutoa maelezo au tafsiri sahihi ya huduma za matibabu bure kwa wajawazito. Hatua hiyo ilitokana na mjamzito mmoja kudai kuwa alipokwenda kupatiwa huduma, alitakiwa kutoa fedha ili kulipia gharama za vipimo.

Maofisa ardhi nao hawakubaki salama, waliingia kwenye 18 za Makonda wakitakiwa kutoa maelezo ya namna wanavyotatua migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa miongoni mwa kero zilizojitokeza katika mikoa 10 aliyotembelea Makonda.

Mama amlilia Makonda mumewe kutekwa

Waichambua ziara yake

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Nassor Seif Amour anasema ziara ya Makonda inasaidia kuwaamsha watendaji wasiotekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ikiwemo kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi wa haraka.

“Namuunga mkono Makonda kwa ziara anazozifanya za kusikiliza kero za wananchi, CCM imepata mtu sahihi wa kufuatilia kero na utekelezaji wa ilani ya chama hicho tawala, viongozi wengine wa Serikali wanapaswa kuiga mfano huu ili kutatua haraka changamoto za Watanzania.

“Wananchi wanatozwa kodi wakitarajia kupata huduma serikalini, hawapati kwa uhakika kutokana na kuwepo watu wazembe, kama kweli tunataka kuondosha changamoto za wananchi basi wafanye kama Makonda,” anasema Amour.

Mkazi wa Kahama, Idd Shaaban anasema ziara za Makonda zinawatisha baadhi ya watendaji wa halmashauri wasiotekeleza majukumu yao kwa sababu wanajua staili ya mwenezi huyo ni kutaka matokeo au majibu ya papo kwa papo.

“Ndiyo maana watu wamekuwa wakitoka katika wilaya mbalimbali kuja kumsikiliza Makonda, anatusaidia kuwachangamsha watendaji waliobweteka, tunamuomba Mungu aendelee kumlinda kiongozi huyu,” anasema Shaaban.