Zitto aridhika na mapokezi ya ACT-Wazalendo, Mkuranga

Kiongozi wa ACT wazalendo, Zitto Kabwe akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasir Ali (kushoto) alipowasili Mwandege wilayani hapo wakati akielekea Ikwiriri kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara wa chama hicho. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Msafara wa viongozi wa ACT- Wazalendo umepokelewa na uongozi wa Wilaya ya Mkuranga, Zitto asema hiyo ni ishara ya namna siasa nchi zilivyobadilika tofauti na miaka saba iliyopita.

Mkuranga. Viongozi wa ACT-Wazalendo wameanza ziara ya kuimarisha chama hicho mkoani Pwani huku kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe akisema hatua ya wao kupokelewa na viongozi wa Serikali inaonyesha demokrasia inavyoimarika tofauti na miaka iliyopita.

Msafara wa viongozi wa ACT- Wazalendo ukiongozwa na Zitto, Juma Duni Haji (Mwenyekiti wa ACT), Ado Shaibu (Katibu Mkuu), Dorothy  Semu (Makamu Mwenyekiti Bara) na wajumbe wa kamati kuu wa chama hicho walipokelewa na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Mkuranga wakiongoza na DC, Khadija Nasri Ali.

Viongozi hao waliopokelewa eneo la Mwandege baada ya kuingia wilayani humo na huku polisi wakiimarisha ulinzi wakati Zitto akitoa salamu kwa wananchi wa eneo hilo wakati wa safarini kwenda wilayani Rufiji kwa ajili ya mkutano wa hadhara.

Akitoa salamu zake, Zitto amesema kwa niaba ya viongozi wenzake wamefarijika na mapokezi ya uongozi wa Wilaya ya Mkuranga akisema hatua hiyo ni ishara ya namna siasa zinavyoendelea kubadilika.

"Kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan, siasa sio uadui, zamani ilikuwa nadra mwanasiasa wa upinzani akiwa na timu yake ya ziara ya kueneza chama kupokelewa na uongozi wa wilaya.

"Khadija (DC) uendelee hivi hivi usiiishie kwangu na kwa wengine pia lakini hakikisha haki inatendeka kuna vijana wa bodaboda na wafanyabishara wadogo shughuli zao zitendewe haki kwa sababu tunajenga Taifa la Wote kwa maslahi ya wote," amesema.

Lakini wakati akimpa salamu za shukrani Khadija, kuhusu mapokezi yao Zitto alikatishwa na wananchi waliokuwa wanafuatilia hotuba yake fupi kwa kumweleza kwamba kiongozi huyo wa wilaya hana baya, jambo lililomfurahisha mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Mjini.

Hata hivyo, Zitto aliwaambia wananchi wa Mlandege na Vikindu kwa amepita kuwasalimia na kwamba atapanga ratiba siku nyingine kwa ajili ya kufanya mkutano wa hadhara wilayani Mkuranga.

"Nawaomba msisikite zamu yenu inakuja maana ndio kwanza mikutano ya hadhara imefunguliwa, lazima twende hatua kwa hatua. Kwa hatua ya sasa tumepanga kufanya mkutano wa hadhara Ikwiriri (Rufiji)," amesema Zitto.

Hata hivyo, Zitto aliwataka wananchi kusema ukweli kuhusu viongozi wao na kutowaonea aibu pindi wanapokwenda kinyume katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Lakini niwaambie ACT- Wazalendo hatutawaonea aya tutawafumbia macho na kuwaeleza ukweli kwamba bi Khadija umefanya hivi au Ded (Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuranga), Mwantumu Mgonja hilo mlijue.

"Lakini tumefurahishwa sana mapokezi huu ndio mfano mzuri wa kuigwa kwa viongozi, ndio raha ya kuwa na viongozi vijana au sio. Jamani raha sio raha...

Naye, Semu amesema " tunaushukuru uongozi wa wilaya na wananchi wa Mkuranga kwa mapokezi mazuri kwetu asanteni sana..." amesema Semu.