MWIBA MDOGO-11
ILIPOISHIA JANA...
“Kabla ya kuingia tulifanya upekuzi wa hali ya juu kuhakikisha ofisi ipo sawa, ndipo tulipomruhusu aingie ofisini kwake kisha kila mtu alichukua nafasi yake. Baada ya tishio umakini uliongezeka maradufu, si unajua mkuu hatunaga kazi mbovu,” Queen alimhakikishia bosi wake usalama wa Mabula.
ENDELEA...
“Mmh! Sawa.”
“Vipi kuna tatizo mmesikia?” Queen aliuliza baada ya swali la Maliki kuonekana lina mashaka.
“Kuna bwege mmoja amesema eti amemuua Mabula.”
“Anachekesha, hata huyo mtoa roho hawezi kuingia kwa ulinzi tulioweka.”
“Poa kazi njema.”
Maliki baada ya kumaliza kuongea na Queen alimgeukia Chifu wake na kumweleza aliyozungumza na msaidizi wake.
“Laki...” hakumalizia sentesi simu iliita tena na kufanya anyamaze na kuiangalia simu, ilikuwa namba ileile ya mtoto wa marehemu, aliipokea na kusema kwa sauti ya chini kidogo.
“Haloo.”
“Baba mbona tumeanza vizuri mpaka leo nashangaa nini kimekugeuza? Najua baada ya zoezi la leo hutaniona tena kwa vile unanijua ila hunifahamu mimi ni nani. Nimeamua kujisalimisha kwa heshima yako, bila hivyo watu wote ningewaua bila kujua nani muuaji na mauaji yametokea kwa sababu gani. Nakupa dakika kumi kunijulisha nijisalimishe kwako au niondoke na hutaniona tena katika umbile la muuaji bali raia mwema.”
“Sawa.”
“Nataka kuwatahadharisha sumu iliyomuua Mabula ni kali sana kuliko sumu zote nilizowahi kuzitumia. Kama ikizidi saa mbili kabla hamjautoa mwili wake ofisini Mabula atavimba na kupasuka harufu yake itageuka sumu kila atakayeivuta ataathirika vibaya.”
“Sa..sa..sawa,” Chifu alikata simu.
Hakutaka maelezo zaidi alimweleza Maliki amfuate.
“Maliki nifuate,” alisema huku akinyanyuka na kuchukua simu yake iliyokuwa juu ya meza.
“Wapi mkuu mbona ghafla?”
“Sitaki maswali nifuate.”
Waliingia kwenye gari na safari ya kuelekea kwenye jengo lililopo karibu na mzunguko wa barabara ya Stesheni na Kenyata. Lilikuwa moja ya majengo marefu jijini Mwanza la ghorofa kumi na saba mali ya Mabula.
Njia nzima alijiuliza kama kuna ukweli wa kauli ya Mtoto wa Marehemu ambayo siku zote ilikuwa ya ukweli, ulinzi waliofanya una faida gani. Hakuamini kirahisi kutokana na ulinzi aliopewa Mabula na familia yake mtu amuue kirahisi.
Alipofika eneo la tukio aliteremka kwenye gari na kuelekea ndani ya ofisi huku akifuatiwa nyuma na Maliki. Kabla ya kupanda lifti kwenda ghorofa saba kwenye ofisi ya Mabula simu yake iliita. Aliipokea haraka baada ya kujua inatoka wapi.
“Haloo.”
“Baba naomba ukifika katika ofisi ya Mabula usiingie ndani, mtume kijana mmoja aingie na barakoa au kitambaa puani. Akiingia tu ndani azime AC kisha afungue madirisha kuacha hewa yenye sumu kutoka nje na hewa ya nje iingie ndani kwa dakika tano. Sumu ikipata hewa ya nje hukatika mara moja.”
“Sawa,” mkuu alikubali bila kuongeza neno.
Baada ya kukata simu wakati huo walikuwa ndani ya lifti iliyokuwa ghorofa ya sita kisha kusimama ghorofa ya saba.
Waliteremka na kutoa taarifa kwa kijana wake mmoja kuingia ofisini awajuze kuna nini, yule kijana aliingia hadi ofisini na kurudi akiwa ametahayari.
“Vipi?” Chifu Shila aliuliza.
“Hali inatisha, Mabula amekufa kifo kibaya sana sijawahi kuona kifo kama kile.”
“Utani huo!” alisema Queen.
“Nyemo kama ulivyoingia mwanzo zima AC kisha kafungue madirisha yote acha hewa iingie ndani kisha toka.”
Nyemo aliingia ndani na kufanya kama alivyoelekezwa na bosi wake kwa kuzima AC kisha kuyafungua madirisha yote na kutoka nje. Japokuwa alielezwa aingie baada ya dakika tano lakini aliongeza kumi zaidi kisha aliingia na vijana wake na kukutana na picha ya kutisha.
Mbele yao Mabula alikuwa amelalia meza alikuwa amekufa kama wenzake waliotangulia kwa kutoka damu sehemu ya kichwani masikioni, puani, machoni yaliyomtoka kama chura ulimi nje.
Kingine kilichokuwa tofauti na wenzake waliotangulia, yeye mwili ulikuwa umevimba na kuanza kubanduka ngozi, hasa sehemu za usoni. Haraka liliitwa gari la wagonjwa kuja kumchukua Mabula na kumpeleka hospitali ya rufaa ya Bugando.
Baada ya kuondoka mwili wa marehemu kila mmoja alikuwa akiwaza lake, huku Chifu akiamini kifo kile ni uzembe na kujiamini kupita kiasi.
“Mmh! Kazi ipo muuaji amejipanga sivyo tunalivyokuwa tukifikiria,” Maliki jasho lilimtoka pamoja na uwezo wake mtihani ule ulikuwa wa kwanza kwake kufeli japokuwa aliamini kama angeanza naye katika matukio angemtia mkononi.
“Mkuu, huyu si mtu wa kawaida, hakuna mtu aliyeingia tangu jana kuna ulinzi mzito sana.
“Siamini ameingiaje lazima atakuwa anatumia uchawi,” Queen hakuamini Mabula kuuawa pamoja na ulinzi mzito.
“Mlijiamini sana ndipo adui yenu alipowapatia, inaonekana mlimdharau baada ya kutoka kwenye kazi nzito na kulegeza ulinzi.”
“Hii sumu inaonekana ilitegeshwa kwenye AC, hivyo hewa iliyotoka ilikuwa sumu tupu ambayo aliivuta Mabula bila kujua,” Ngumije alitoa ushauri.
“Hata kama sumu ameiweka kwenye AC kaingiaje?” Queen aliendelea kushangaa.
“Hii ni aibu, inaonekana sumu imewekwa usiku,” Maliki alijibu.
“Sasa kapitia wapi?” Queen alihoji.
“Hebu angalieni kila kona tuone kuna sehemu gani imetumika kuingilia ndani,” alisema Chifu akiwa amekunja uso kwa hasira baada ya vijana wake kumuangusha.
Walifanya upekuzi kila kona, wakiwa bado wanajadiliana, Molandi aliyeingia maliwatonialimwita Chifu.
“Chifu.”
“Unasemaje Molandi?”
“Mkuu maliwatoni kuna tundu dogo lililozibwa kitaalamu sana japo dirisha lilikuwa limefungwa kwa ndani.”
Waliongozana wote hadi bafuni, baada ya kuangalia kwa umakini sana waliweza kugundua tundu dogo hata mkono ulikuwa haupiti ambalo lilikuwa limezibwa na stika ya rangi ya kioo.
Baada ya uchunguzi makini waliona chini ya sakafu kuna waya mdogo ambao ulionyesha ndio uliotumika kufungulia na kufunga na mtumiaji alidondosha wakati wa kufunga.
“Kweli sasa hivi tumekutana na mtu wa kazi japokuwa nina imani katuzidi hesabu kutokana na mitego aliyotutegea tukaingia. Mitego yake ukiiangalia vibaya utaiona ya kitoto, lakini imetegwa kwa akili kubwa sana, yataka utulivu wa hali ya juu,” alisema Maliki, huku akifungua dirisha na kuchungulia nje.
“Mkuu alitumia kama kuning’inia toka juu.”
Unaweza kufuatilia hadithi hii kupitia tovuti ya Mwananchi, pia Mwananchi Digital katika Mtandao wa Youtube
Itaendelea kesho