FYATU MFYATUZI: Wanajifanya kufyatuana ili watufyatue tena aisee?

 Nkwazi Mhango

Naandika nikilia kwa uchungu. Juzi nilinusurika kupata kichaa. Sikuamini niliyoona kwenye runinga kuwa fyatu tena muishiwa wa chata twawala angewafyatua wanene mawazira wasiozira bali kufyatua kuwa wamefyatua matrilioni ya madafu. Unajua madafu trilioni yanaonekaje? Kama hujui, ukipanga noti za jero, trilioni ina urefu kuliko mlima Kimaranjaro.

Mnainyaka mafyatu wangu? Wamjua Luhanga Mpini? Alimfyatua paka kapuni na kufyatua mtama kwenye kuku wengi, tukiwemo wafyatuaji na kutupa nyenzo ya kufyatua haya mafyatu manene mafyatuaji njuluku za mafyatu waliofyatuliwa.

Kabla ya kuendelea, kabla ya hapo nilipata nyuzi kuwa maza na washauri wake wananyaka ufyatuzi wangu. Nimewafyatua hadi wakafyatuka na kugeuka mafyatu kama ninyi mafyatu zangu mnaosoma ufyatuaji, ufyatukaji na ufyatuzi wangu.

Fyatu mmoja alinitonya kuwa maza alisoma vitu vyangu alicheka hadi akaomba maji ya kunywa. Hivyo, nawataarifuni rasmi, nami ni mshauri wa maza msikivu na msomi dokitari.

Hivyo, ninachofyatua hapa kitamfikia na atakifanyia kazi kwa kuwafyatua ninaotaka wafyatuliwe baada ya Mpini kutaka wafyatuliwe na kurejesha njuluku walizofyatua wakati mafyatu walio wengi wakifyatuliwa na ukapuku.

Mpini kweli kashika mpini. Maana ukimsikiliza anapowaambia takokuru wawafyatue mafyatu anaowatuhumu tena wanene, anajua anachofyatua. Nawashauri watuhumiwa wajue hivyo na kumwelewa hata wale waliowapa ulaji.

Je, siku zote alikuwa wapi? Give the devil his due. Amethubutu hata kama ni kwa faida ya chata lake na kutaka kuwaingiza mafyatu mkenge kama kawa wapige kura ya kula kwenye uchakachuaji.

Mpini alisema kuwa mawazira waliokwiba njuluku wajipime au maza awapime na kuwafyatua kabla hajafyatuliwa na mafyatu kwenye uchakachuaji ujao. Mpini alitaja ripoti ya CAG ambayo ilifanya jana nishindwe kula.

Nilijaribu kanywaji nikashindwa. Kila kitu hata chakula cha usiku nilishindwa. Nilijikuta nachanganyikiwa kwanini nakuwa kapuku wakati mijizi minene ikiendelea kupiga utadhani shamba la bibi. Hii kaya ya mama siyo ya bibi.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, kaya ilipigwa madafu trilioni 30, bado mafyatu wanalala na wengine kupeana ulaji! Inakuwaje zipigwe njuluku ndefu kama hizi halafu mama anahangaika eti kwenda na kombe mkononi akibomu ukiachia mbali kaya kujaliwa ukwasi mwingi ajabu ambao tunao lakini tunaukalia?

Inakuwaje halioni hili au linahitaji macho ya ziada au linampendeza tu? Iweje? Kwa nini? Hajui? Anajua? Ilikuwaje akawapa ulaji tena nyeti watuhumiwa kama Mwiguu Michembe, Janiwari son of Joseph Makambale, ImmaTutubu, Maukame Mbawala na wengine aliowafyatua Mpini?

Kwa nini njuluku ndefu hupigwa kila karibu na uchakachuaji au hii kitu ni kubwa kuliko inavyoweza kuonekana? Halafu anatokea muishiwa anatetea chata la walaji kuwa halitetei hawa wevi kana kwamba wanachaguliwa au kuteuliwa na wapingaji.

Oneni aibu jamani, nasi hata kama mafyatu, tuna akili pia kumbukumbu za kufyatuliwa. Natamani yule anayejiita doktari wa uchumi aliyeficha tasnifu yake tuwekwe kitimoto nimuubue lau aseme udoktari wake ima ni wa kupewa au kughushi au kufanyiwa lakini si wa kusomea. Hayo tuyaache.

Inapofikia muishiwa wa chata twawala kushindwa uzalendo akaamua kama mbaya mbaya akafyatuka, jua mambo siyo poa. Hii huitwa kufyatua, kutyatuliwa, kufyatuka na kufyatuana katika sayansi ya mafyatuzi na ufyatuzi. Hata hivyo, huu ufyatuaji wa njuluku za mafyatu si wa kawaida wala wa kuufyata.

Nani aufyate wakati huu ambapo mafyatu wanafyatuliwa na taabu tena za kutengenezwa na mafyatu wanene wanaopaswa kufytuliwa hasa baada ya wao kufyatuana? Je, huu uchungu umeanza lini? Kwa nini sasa? Je, kuna kitu mafyatu hawajakimanya, hivyo wanapaswa kuwa makini wasifyatuliwe kwa maneno matamu na uzalendo mahepe na machezo?

Je, hapa wanashindwa uzalendo au ni yale yale ya karata tatu kwa kujua uchakachuaji umekaribia lazima mafyatu wavikwe mkenge kwa uzalendo wa ghafla bin vu?

Kwa nini sasa si wakati ule njuluku zilipoanza kupigwa? Je, hatuwaoni akina Kagoda wakiandamana au kumtangulia bi mkubwa kwenye ziara zake nje? Je, hapa tumuamini nani kati ya hawa wadogo wa chata lilelile?

 Kama mnamaanisha kweli basi fyatukeni mjiunge na mafyatu wa upingaji mpige mzigo kieleweke kuliko kuwa ndumakuwili kwa Kiingereza.

Hivi uchakachuaji wa uchaguzi ni lini? Alaa kumbe!