Haya yazingatiwe kwa Serengeti Boys
Baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ walipokuwa wakishangilia moja ya ushindi katika mechi za AFCON-17
Kwa miaka mingi soka la taifa limekuwa likisafiri kwenye safari ya matumaini yanayojirudia, lakini mara nyingi bila kufika mwisho wa ndoto. Wapo wanaolieleza hali hii kama ‘ndoto za alinacha,’ yaani matarajio makubwa yanayoishia hewani bila kutimia.
Ni safari ambayo imekuwa na vipindi vya mwanga wa matumaini, kisha ghafla kurejea kwenye giza na changamoto.
Si jambo jipya. Katika vipindi tofauti, soka la Tanzania limewahi kuibua kauli kali na ‘tata’ zikiakisi hali halisi ya soka nchini.
Miongoni kauli maarufu zaidi ni ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili, hayati Alhaj Ali Hassan Mwinyi, ambaye mwaka 1993 alinukuliwa akitumia taswira ya ‘kichwa cha mwendawazimu’ kuelezea hali ya soka la Tanzania.
Mzee Ruksa alitoa kauli hiyo kufuatia miaka ya matokeo duni ya timu za Tanzania katika mashindano ya kimataifa, hali iliyoacha mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa soka la taifa.
Katika nyakati tofauti pia, viongozi na wadau wengine wa soka wamewahi kuonesha kukerwa na mzunguko huo wa mafanikio ya msimu mmoja na kurudi nyuma wa miaka mingi, ambapo matumaini yamekuwa yakizaliwa upya kisha kufifia haraka.
Ni katika muktadha huo ndipo vipindi vichache vimewahi kuwasha tena mwanga wa matumaini, kama ilivyotokea kupitia mafanikio ya Serengeti Boys, timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, ambayo sasa imefungua ukurasa mpya wa mjadala kuhusu mustakabali wa soka la Tanzania.
Kufika fainali ya michuano ya Afrika si jambo dogo. Ni matokeo ya uwekezaji wa muda mrefu kupitia akademi za soka, kazi ya makocha wa vijana na juhudi za wachezaji wenyewe.
Hata hivyo, mafanikio haya si ya kushangilia kisha kuyahifadhi kwenye kumbukumbu. Ni mafanikio yanayopaswa kuchukuliwa kama mwanzo wa kazi kubwa zaidi ya kujenga kizazi cha dhahabu kitakachotutoa kimasomaso kwenye mashindano mbalimbali hapo baadae.
Hii inathibitisha jambo moja muhimu, Tanzania haina tatizo la vipaji. Tatizo kubwa ni mfumo wa kuvibaini, kuvilea na kuvifikisha kwenye kiwango cha juu.
Hilo limethibitishwa zaidi kwa kuwa licha ya mafanikio ya pamoja, Serengeti Boys walionesha ubora binafsi kupitia tuzo walizovuna.
Kiungo mshambuliaji Issa Mussa Chole alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano. Kwa upande mwingine, mshambuliaji Dismas Shida Athanasi alitwaa kiatu cha dhahabu baada ya kuwa mfungaji bora wa michuano.
Hii ni ishara ya wazi kwamba Tanzania ina wachezaji wachanga wanaoweza kutumia nafasi kwa ufanisi na kuliwakilisha vyema taifa katika majukwaa makubwa.
Lakini pamoja na mafanikio haya, swali muhimu linabaki pale pale, Tanzania itafanya nini kuhakikisha kizazi hiki hakipotei kama ilivyotokea kwa vipaji vingi vya Afrika vilivyoanza kwa kishindo kisha kufifia kimya kimya?
Swali hilo linachagizwa na historia ya soka barani Afrika na soka letu wenyewe pia ambalo limejaa mifano lukuki ya timu za vijana zilizong’ara lakini baadaye kushindwa kuhamia kwenye mafanikio ya timu za wakubwa.
Sababu kubwa zimekuwa ni ukosefu wa mipango ya muda mrefu, mifumo dhaifu ya maendeleo na wachezaji kukosa muda wa kucheza kwenye viwango vya ushindani.
Tanzania ina nafasi ya kuepuka makosa hayo, lakini inahitaji maamuzi ya makusudi sasa, si baadaye.
Kwanza, mafanikio haya yasichukuliwe kama mwisho wa safari bali mwanzo wa mchakato mpya. Serengeti Boys wanapaswa kuwa mradi wa taifa, si tukio la kushangiliwa na kusahaulika. Lazima kuwepo mfumo wa kuwafuatilia wachezaji mmoja mmoja na kupima maendeleo yao kwa muda mrefu.
Pili, wachezaji hawa wanapaswa kupewa muda wa kucheza katika klabu za Ligi Kuu na kuangalia mazingira bora zaidi ya kwenda kucheza soka la kulipwa barani ulaya ambayo ni njia inayofanya mataifa makubwa kisoka kama Senegal kuendelea kutawala soka la Afrika kutokana na ubora wa wachezaji walio nao kwenye kikosi wakitumikia timu kubwa ulimwenguni.
Ikumbukwe, mchezaji wa miaka 17 hawezi kukua akiwa benchi kwa misimu miwili au mitatu. Dakika za mechi ndizo zinazojenga wachezaji wakubwa, si mazoezi pekee.
Tatu, maendeleo yao lazima yaende sambamba na malezi ya nje ya uwanja. Soka la kisasa linahitaji zaidi ya kipaji; elimu ya lishe, afya ya akili, usimamizi wa fedha na uwezo wa kukabiliana na presha ya umaarufu ni muhimu kama mazoezi ya uwanjani.
Aidha, Tanzania inapaswa kuendelea kuimarisha mfumo uliowatoa Serengeti Boys, kuanzia akademi za soka, mashindano ya vijana na mafunzo kwa makocha lazima viendelee kupewa kipaumbele ili kuzalisha vizazi vingine vinavyoendelea.
Hata hivyo, kuna makosa yanayopaswa kuepukwa. Kwanza ni kuwabebesha vijana hawa mzigo mkubwa wa matarajio ya haraka. Sio wote watakomaa kwa wakati mmoja, na kila mmoja ana njia yake ya maendeleo.
Pili, soka lisigeuzwe uwanja wa siasa au migogoro ya maslahi. Mafanikio yao yanapaswa kubaki kwenye maendeleo ya wachezaji, si mjadala wa nani anapata sifa zaidi.
Kwenye hili ni vyema kuweka msisitizo zaidi kwa sababu hakuna taifa lililowahi kufanikiwa kwa kuchanganya soka na siasa.
Tatu, uhamisho wa haraka kwenda nje ya nchi usifanywe bila mipango thabiti. Si kila safari ya mapema huleta mafanikio. Ni vyema kuangalia kwa umakini usio wa kawaida ‘nature’ ya sehemu tunazowapeleka vijana wetu ili wakakue na sio kufifia.
Mwisho, Tanzania inapaswa kuepuka kuridhika. Kufika fainali ya Afrika ni hatua kubwa, lakini si mwisho wa safari.
Serengeti Boys wanaweza kuwa daraja la mageuzi ya ‘Taifa Stars’ ikiwa wataendelezwa vizuri. Wanaweza kuwa msingi wa timu ya taifa yenye ushindani Afrika na hata kufuzu Kombe la Dunia.
Kwa mantiki hiyo, Tanzania imepewa nafasi adimu ya kuandika upya historia ya soka lake.
Sasa uamuzi uko mikononi mwa viongozi na wadau; ama mafanikio haya yabaki kuwa kumbukumbu ya muda mfupi, au yawe mwanzo wa enzi mpya ya soka la taifa.