Hongera Airtel, huku ndiko mpira uliko

Muktasari:
- Mashinmdano hayo yameandaliwa na Chama cha Mpira wa miguu wilaya ya Kinondoni.-KIFA.
Katika habari ambazo zimenifurahisha na kunisisimu kwa juma hili na binafsi kuwa ndiyo habari ambayo niliiona kwangu ni muhimu ni kitendo cha Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel kuamua kufadhili mashindano ya ‘mchangani.
Mashinmdano hayo yameandaliwa na Chama cha Mpira wa miguu wilaya ya Kinondoni.-KIFA.
Natoa hongera pia wilaya ya Kinondoni kwa kuthubutu kuwatafuta Airtel. Sishangazwi na ubunifu wa viongozi wa KIFA kwa kutambua kwamba wao ndio walioasisi kwa kiwango kikubwa soka kwa wanawake hapa nchini (chini ya Katibu Mkuu, Frank Mchaki ambaye binafsi ninamwona ni kiongozi mbunifu na mwenye kuona mbali kuhusu maendeleo ya soka na ndiyo ukawa mwanzo wa kuunda timu ya Twiga Stars.
Mada yangu ya leo kama nilivyosema hapo juu ni kwanza kuupongeza uongozi wa KIFA kwa uanzishaji wa mashindano hayo katika ngazi ya chini kabisa ambako wengi huwa hawafikirii (mara nyingi mashindano katika ngazi husimamiwa na wadau wapenda mpira wa eneo husika).
Aidha pia kitendo cha Airtel kukubali kuyadhamini mashindano hayo pamoja na kwamba kwa mtazamo wa wengi yasingepata mdhamini wa kiwango kikubwa hivyo.
Airtel wamesaidia maendeleo ya mpira wa nchi hii kupitia udhamini wao wa mashindano ya Airtel Rising Star ambayo yalisaidia uundwaji wa timu ya Taifa ya Vijana ya Serengeti Boys ambayo sote tulishuhudia jinsi ilivyofika ngazi ya fainali ya michuano hiyo Africa mwaka huu.
Kitendo walichokifanya Airtel kinapaswa kuigwa na wale wote ambao kwa sasa wanausaidia mpira wa miguu nchini, mathalani Vodacom, Serengeti Breweries (SBL), Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL), Benki ya NMB, AZAM na wengine wote ambao kwa namna moja huwa wanasaidia mpira wa miguu kupitia mabonanza mbalimbali kama Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Kwa anayependa na kuifuatilia soka, anagundua kwamba kuna vijana wenye vipaji vya soka kwa ufasaha tena bila ya kupata maelekezo yoyote ambao hawaangaliwi na kutambuliwa ili kuwafikisha sehemu sahihi.
Binafsi nina ushuhuda wa vipaji vya vijana mitaani kwa sababu nautumia muda wangu mwingi na kundi hilo la wachezaji.
Mathalani, nilikigundua kipaji cha kijana Moris a.k.a. Chuji pale uwanja wa shule ya msingi ya Tabata akiwa darasa la tano shule ya msingi Kigogo. Baada ya miaka miwili kupita, wakati wa mashindano ya kitaifa ya timu za mikoa za watoto wa chini ya miaka 12 pale Mwanza, aliibuka mfugaji bora na mchezaji bora wa mashindano na kuchaguliwa timu ya Taifa na sasa ni mmoja ya wachezaji wa kutumainiwa wa timu ya Taifa ya U-17. Nina imani kubwa matunda ya utaratibu huo wa KIFA na Airtel yataonekana katika kipindi kifupi kijacho.
Ombi langu kwa wote ambao watavutiwa na utaratibu wa udhamini wa namna hii, wasaidie kuwajengea uwezo makocha wa timu hizo.
Ninafahamu kila timu ndogo ya mtaani ya watoto hao ina makocha ambao takribani karibu wote hawana elimu yoyote ya ukocha na pengine hawana sifa za kujiunga na kozi za ukocha za awali ‘preliminary’.
Ninashauri kwamba makocha hao wapewe mafunzo yatakayosaidia namna ya kuwatambua wachezaji wenye vipaji na aina ya mazoezi na muda wa kufanya hayo mazoezi ili kutowaathiri wachezaji hao. TFF inaweza kusaidia kutengeneza mwongozo kwa ajili ya kazi hiyo na wale ambao wataonekana kufanya vizuri, wakashauriwa kujiunga na mafunzo ya ukocha ya awali ‘prelimiary’. Nimalizie mada yangu kwa kurejea kuwapongeza Airtel na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano huo.