KONA YA MAKENGEZA: Sera ileeeee sura hiiii
Muktasari:
Ndiyo maana asipotambua kwamba anahitaji kutushawishi na kutushirikisha wote, atakwisha. Watamdhibiti na uthubutu wake.
Juzi nilishangaa sana kuletewa barua:
We Mwishiwa Makengeza,
Watakiwa kuhudhuria bila kukosa kikao cha kwanza cha Waishiwa ndani ya Awamu ya Tano. Haki na masupusupu yatakuwapo kama kawaida.
Sasa Mungu akupe nini, hasa wakati mwisho wa mwezi unaonekana masafa ya mbali.
Nilijipeleka kule raha mstarehe udenda ukidondoka tayari kwa hamu ya kufakamia supu kama enzi zile. Niligundua jinsi ambavyo nimekuwa naimiss supu dah.
Kwa jinsi nilivyoondoka mapema, nilifikiri nitakuwa wa kwanza lakini kumbe wengi walikuwa wameniwahi kwa matamanio hayohayo ya kwangu. Niliona hata na sura mpya nyingi. Sasa kilichonishangaza ni kwamba wengine kweli walikuwa wanafakamia lakini wengi walikuwa wamekaa pale, bakuli tupu. Lakini sikutaka kuuliza maana nilikuwa nimeletewa supu na ilibidi ninyamazishe michango ndani ya tumbo kwanza. Punde si punde na mimi pia nilikuwa na bakuli tupu na kamfupa pembeni kama wengine. Hapo ilibidi nijiulize kulikoni.
‘Bwana ee! Huyu Mwishiwa Supu wetu amerukwa na akili kabisa. Eti yeye na mwenye sebule wameamua kwamba supu iende kwa shule ya karibu watoto wetu wapewe madawati. Eti tunavyofakamia supu tunawasahau hata watoto wetu.’
‘Duh!’
‘Kabisa. Lazima tufanye kitu. Haiwezekani atudharau namna hiyo. Waishiwa ni waishiwa na wengine ni wengine. Tuna haki zetu eti.’
Na wengine kweli walianza kupiga meza zao.
‘Haki yetu, supu tatu. Haki yetu supu tatu.’
Mwishiwa Supu hakushtuka. Badala yake alionekana kupiga simu. Mwishiwa mwingine alipaza sauti.
‘Bwana ee, mnataka kutwangwatwangwa kwa sababu ya bakuli ya supu? Hebu tuone hizi habari za wengine ni nguvu za kweli au kufuata mkumbo tu.’
Mwingine naye alidakia.
‘We unafikiri tutaelewekaje mbele ya wananchi wenzetu? Utateteaje masupusupu yako mbele ya watu wenye shida?’
‘Mbona katika awamu nyingine tulizidi kuongezewa supu siku hadi siku?’
‘Lakini mwanzoni haikuwa hivyo. Kila anayepanda kwenye kiti cha dhahabu anaanza vivyohivyo. Tutakomesha anasa. Tuwatumikie wananchi. Na gari lake linakwenda vizuri sana hadi hapo linapopigwa pasi na watu walioshika dola za dola. Utaona tu.’
‘Hakuna. Huyu anaonekana tofauti. Hajaahidi tu. Tayari amechukua hatua. Mtu kama huyu ni hatari sana. Tutaishije bila masupusupu yetu?’
‘Sawa. Inawezekana huyu ana nguvu ya bia zaidi maana povu limetulia palepale badala ya kuishia hewani. Lakini hii ni Bongo Bwana, si Bongo Muvi.’
‘Una maana gani?’
‘We si unaona katika muvi. Mtu mmoja anao uwezo wa kutwanga kundi ya watu mia peke yake. Na unapoangalia vizuri unaona kabisa watu wamejipanga kabisa kutwangwa mmoja baada ya mwingine. Lakini katika hali halisi, hakuna kupanga foleni. Watu wanavamia kundi lote na utabaki kukanyagwakanyagwa tu.’
‘Bado sijakuelewa.’
‘Huyu jamaa namsifu. Kweli hata mimi nasikitika kukosa supu ya tatu hadi ya nne lakini maneno yake yana mantiki.’
Mwingine anadakia.
‘Ni kweli. sera ya upinzani ndani ya sura ya walewale.’
‘Sawasawa. Ndiyo maana asipotambua kwamba anahitaji kutushawishi na kutushirikisha wote, atakwisha. Watamdhibiti na uthubutu wake.’
Mwingine naye akacheka.
‘Naam. Kiongozi akijipeleka mbele bila kuhakikisha yupo na watu, watamwona wa kimbelembele tu na kumwacha peke yake, kama si kumchukulia hatua zaidi.’
‘Sasa unataka afanye nini zaidi? Ameonyesha mfano, sisi ni wa kufuata.’
‘Ndiyo tatizo letu sisi Wabongo. Tunamsubiri Masiya atufanyie kila kitu bila kutaka kufanya wenyewe. Kwani ndani ya maeneo yetu ya kazi hatujui maovu yaliyopo?’
‘We Bwana unataka tumwage unga hivihivi? Enzi za kujitoa mhanga zimekwisha.’
‘Ndiyo tatizo letu sisi Wabongo. Hatuamini kwamba tuna nguvu tukiamua kufanya kwa pamoja. Umeshasahau manyomi ya juzi. Hata kama wengi hatukupata matokeo tuliyoyataka, lakini yameleta mabadiliko kwa namna fulani. Tawala ikageuka pinzani iendelee kutawala.
Mwingine naye alidakia.
‘Juzi niliangalia kipande cha video kuhusu Wasukuma wakilima. Alikuwapo kiongozi na zeze lake ambaye alikuwa anaimba wimbo mtamu sana. Sasa unafikiri wenzie walikuwa wanamwangalia na kumpigia makofi? Thubutu! Walitumia wimbo ule kuimba na wao na kulima kwa nguvu. Na kwa kuwa walikuwa wanaimba pamoja waliweza kulima eneo kubwa licha ya ugumu wa ardhi na jua kali.
‘Ah, toka hapa na mifano yako.’
‘Nawaambieni.
Mwenye zeze haendi kupiga peke yake, anapiga palipo na watu, anawashawishi na zeze lake na kwa kufanya hivyo, yeye na wenzake wote wanafaidi. Vinginevyo ataonekana zuzu na zeze lake.’
Watu walitaka kuendelea kubishana lakini akaja mwingine.
‘Bwana ee. Tunafanya nini hapa? Lazima tutoke.’
‘We bwana tumeshakubali. Tutaeleweka vibaya kung’ang’ania supu wakati watoto wetu hawana madawati …. ‘
‘Angalau kwa muda.’
‘Ndiyo. Angalau kwa muda. Mwangalie hata Mwishiwa Supu. Kabugia moja tu. Ukitaka kufakamia supu nyingine, kanunue mwenyewe.’
‘Siongelei haya. Huoni wageni wa Mwishiwa Supu wetu. Unawatambua?’
‘Yule pale si alikuwapo pamoja nasi. Aliletwa na Mwishiwa Supu kama mshauri wake.’
‘Ndiyo lakini baadaye tulimtoa kwa kuwa wengine walimpenda yule mwenzetu zaidi. Unamwona mwenzetu hapa.’
‘Utamwona wapi Bwana. Mwishiwa Supu si alimpiga marufuku eti anajidai kiongozi kuliko yeye.’
‘Ni haki hiyo? Lazima tutoke kupinga uonevu wa aina hiyo.’
Yule jamaa wa wimbo wa Wasukuma alicheka kwa kejeli.
‘Yaleyale.’
‘Una maana gani? ‘
‘Mwishiwa Supu anafanya maamuzi bila kutushirikisha sisi. Ni vibaya na tunakasirika. Na sisi tunafanya maamuzi bila kumshirikisha mtu yeyote. Tukifanya fujo kwa kukosa supu, nani atatuelewa? Na tukitoka kupinga maamuzi ya kulazimisha ya Mwishiwa Supu, nani atatuelewa pia? Tumefanya juhudi gani kuwaelewesha wananchi kwa nini tunafanya vile?’
Mwingine akamwunga mkono.
‘Ni kweli. Yaani sisi tunajiona sisi tu. Tunaona kwa kuwa tumeelewa kitu fulani kwa namna fulani, basi watu watatufuata. Kwa nini tuwafuate? Wanakubaliana nasi? Tumewaelewesha na kuwashawishi na kuwashirikisha katika maamuzi? Tunatenda tu kisha tunashangaa wakitushangaa na hata kutukataa.’
‘Hii siyo hoja. Lazima tuonyeshe msimamo.’
‘Umekuwa na wiki ngapi tangu yule mwenzetu awekwe pembeni bila sababu? Na tangu hii itokee umefanya juhudi gani kuhakikisha kwamba wote wanaelewa kwa nini ni lazima kuchukua hatua ili iwe hatua ya wote, si hatua ya wapiga zeze tu. Hata nyinyi mtaonekana mazuzu pia.’
Wakati huu Mwishiwa Supu aliamka na kutaka kusema.
Yule jamaa na wenzake walianza kupiga kelele lakini Mwishiwa Supu hakushtuka. Akapiga mluzi mmoja wakaingia mabaunsa.
Wale jamaa walitoka hata kabla ya kubaunsiwa. Baada ya hapa Mwishiwa Supu aliendelea kana kwamba hakuna lililotokea.
Kwa kweli sikumsikiliza sana maana tayari kichwa kilikuwa kimejaa mawazo. Naona sisi waishiwa tumeiga vya hawa waheshimiwa wa sponji na bosi wao. Bosi kapiga zeze vizuri sana, lakini wapi kutushirikisha na sisi. Anapoongea anasema mimi … yangu … mimi … yangu … mimi … au sisi … yetu … sisi … yetu … sisi? Tunamtakia mema kweli lakini bila kutushirikisha na sisi …. Mmmh! Na hawa wengine waliotoka. Kweli wana haki ya kufanya hivyo lakini wametushirikisha? Wametuelewesha? Maana ya demokrasia siyo nyomi ya mwezi mmoja wala si vitendo vya kushtukiza. Ni kutushirikisha kila siku, kila wakati. Kwa njia hiyo tutalima vizuri shamba letu.
Je ataendelea?
Je ataweza kuendelea?
Kweli sisi ni Watanganyika.
Njia iliyopo ni kutoka nje tu? Mmewaandaaje wananchi?
Sera ya wapinzani ndani ya chama cha wenyewe.
Nchi si rais, nchi si kundi la wabunge, nchi ni wananchi.