Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfumo jike utaathiri watoto wa kiume kisaikolojia

Machi 8 kila Mwaka, Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya wanawake. Hii ni kampeni ya kila mwaka ya Umoja wa Mataifa ya kuhamasisha juhudi za kuleta usawa wa kijinsia duniani kote.

Lengo kuu la kuadhimisha siku hiyo ni kutoa fursa kwa jamii kupima utekelezaji wa maazimio, matamko, mikataba na itifaki mbalimbali za Kimataifa na kikanda zinazohusu maendeleo ya jinsia na uwezeshaji wanawake.

Wanawake wamekua wakipigania haki ya usawa, kumiliki mali, nafasi sawa za uongozi na kuondoa ukandamizi wowote unaomfanya mwanamke ashindwe kufikia malengo yake ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Azimio la Beijing la mwaka 1995 lililenga kumkomboa mwanamke na kutaka afikie nafasi ya 50/50 kwenye ngazi ya maamuzi na kusisitiza usawa wa jinsia, kuwaongezea wanawake uwezo na kuzingatia haki za binadamu.

Yote haya yanafanywa ili mtoto wa kike awe na haki sawa na yule wa kiume, juhudi ambazo kwa kiasi kikubwa zimezaa matunda japo lengo halijatimia.

Wakati ambao dunia ikipambania usawa wa mtoto wa kike, lipo bomu linalotengenezwa yamkini bila kujua ambalo linamuacha nyuma mtoto wa kiume na kumfanya ajione hana haki kwa jamii na hakustahili kuzaliwa kwenye ulimwengu huu. Wakati ambao tunataka mazingira wezeshi kwa mwanamke kwa kuhamasisha apate elimu kwenye mazingira rafiki, tukumbuke pia mtoto wa kiume anapaswa kusoma kwenye mazingira rafiki na kujengewa uwezo ili aweze kuwa baba bora wa kesho.

Katika maadhimisho ya siku ya wanawake mwaka huu, kumekuwa na kauli zisizofaa kwa baadhi ya viongozi zikionyesha kuwanyanyapaa waziwazi wanaume.

Ni dhahiri uanzishwaji wa siku ya wanawake haukulenga kumpinga mwanaume bali ililenga kuweka usawa wa kijinsia hivyo kutumia siku hii kumnyanyapaa mwanaume ni kuendeleza unyanyapaa ambao tunapambana kuutoa kwenye jamii.

Zimekuwepo kauli zisizofaa na zisipokemewa zitaendelea kumuathiri mtoto wa kiume. Mathalani kiongozi kusimama na kutangazia wanawake kutomchagua mwanaume kwenye chaguzi zijazo huo ni unyanyapaa lakini pia inaonyesha bado wanawake hawajui wanachopigania.

Kama mababu zetu walipinga mwanamke kupata nafasi za uongozi na kuwanyima haki ya kupata elimu na sasa karne ya 21 wapo wanawake wakitangaza wanaume wasipewe nafasi kwenye chaguzi, haina tofauti na wazee wetu wa zamani waliomnyanyapaa mwanamke na kumnyima haki.

Kauli hizi tunaweza kuziona za kawaida lakini zinaathari kubwa kwa watoto wa kiume wanaozisikia kwanza zinawaathiri kisaikolojia na kuwafanya washindwe kujiamini.

Sipingi hatua za kumuinua mtoto wa kike la hasha napingana na wale wanao ona wanaume na watoto wa kiume hawana haki kwakuwa tuu mfumo wa zamani uliwabeba zaidi wao.

Maisha yamebadilika, mfumo dume uliokuwemo enzi za mababu zetu haupo kwa kiasi kikubwa mila na tamaduni kandamizi zimepungua na ni vema tuendelee kuzitokomeza lakini sio kwa kuwafanya watoto wa kiume kujiona wakosa na hawana haki.

Viongozi wanawake ni vema wakawa makini na kauli zao wanaposimama majukwaani kuhamasisha uwekezaji kwa mtoto wa kike, waepuka sana kumponda mtoto wa kiume usawa tunaoutaka uende sambamba na kwa mtoto wa kiume.

Kama tutambeba mtoto wa kike na kumuacha nyuma mtoto wa kiume kwa madai watoto wa kike walikosa haki ni wazi tunatengeneza Taifa la ajabu, ambalo litakuwa na wanaume wanaovaa suruali lakini hawana uwezo wa kufanya maamuzi na watakua mzigo kwa familia.

Mwanamke imara wa kesho atakua na furaha kama atakuwepo baba imara kwenye familia, ukikutana na wanawake wengi sasa lawama kubwa zipo kwa wanaume kuwa wameshindwa kutunza familia na mama kuachiwa mzigo wa malezi.

Tusibaki kutaka haki sawa kwa kumpendelea mtoto wa kike, kama ambavyo tunatengeneza mazingira wezeshi kwa mwanamke basi mazingira hayo yajengwe pia kwa mtoto wa kiume ili kuepuka kuwa na Taifa lenye wanaume wasio jiamini.

Badala ya kulaumu tujiulize sasa tumekosea wapi? Mwanamke anapopewa mbinu za kujikwamua kiuchumi huyu mtoto wa kiume anajengewa uwezo huo? kuwahukumu wanaume kwa kuwaweka kando kwa makosa ya enzi za babu zetu tunawaonea na tunaonea pia kizazi kijacho. Ukweli ambao haupingiki ni kuwa hakuna mwanamke bila mwanaume na Mwenyezi Mungu hakukosea kumuumba Adamu na kumpa Hawa kama msaidizi wake.