Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siku mstaafu alipoongezwa pensheni kwa mara ya mwisho

Kama utani, wastaafu wetu wa kima cha chini wanafikisha miaka 20 sasa tangu yule mwana mwema wa Msoga alipoamua kuwapa nyongeza ya pensheni yao ya Sh50,000 kwa mwezi, kuwa Sh100,000.

Japo hazikuwa haba lakini hali ngumu ya maisha iliishanza kupiga hodi, mfano mzuri ukiwa ni kilo moja ya sukari kuwa Sh600 badala ya Sh300, unga kuwa Sh300 badala ya Sh180 na maharagwe kuwa Sh350 badala ya Sh200.

Hii ilimfanya mungwana wa Msoga kuwaonea huruma wastaafu wake wa kima cha chini wa Taifa, ambao tunaweza kusema kwa uhakika kabisa kuwa wengi ndio walioipatia uhuru nchi hii na kuijenga hadi mlipoikuta.

Licha ya kwamba wengi wameshatangulia mbele za haki kupitia Kinondoni na kwingineko, wachache bado tupo na tunaihitaji sana nyongeza ya pensheni yetu ya ‘laki si pesa’, si ombi ni haki.

Ndiyo maana yule muungwana wa Msoga hakutaka kusubiri kamati au vikao vimpangie cha kuwasaidia wastaafu wake wa Taifa. Alitekeleza tu. Mungu ambariki.

Ni sawa kumlipa mstaafu wa Taifa hili Sh100,000 kwa mwezi kwa miaka 20, wakati kilo moja ya sukari iliuzwa kwa Sh600 lakini sasa kilo hiyohiyo moja inauzwa shilingi… mama wee! Sh3,000 kwa kilo?

Huyu mstaafu anaishije kwenye hali kama hii ambayo kila uchao shilingi yetu inazidi kuporomoka lakini kwenye vyombo vya habari tunaishia kujitekenya na kucheka wenyewe kwa kujifagilia kuwa uchumi wetu unapanda, huku tukikopa kushoto, kulia na katikati?

Ni Rais gani wa nchi aliyetuongoza kwenye kuijenga nchi hii bado anapokea mshahara uleule aliokuwa akipokea Rais mwenzake miaka 20 iliyopita? Na pensheni yake anayopokea sasa ni ileile aliyopokea mwenzake miaka 20 iliyopita?

Si zimeshapandishwa na wabunge wetu, lakini bado wastaafu wa kima cha chini wa laki moja kwa mwezi, bado wanasubiri, mwaka wa 20 sasa kamati itoe jibu wastaafu waongezwe nini.

Wote tujiulize, ni mfanyakazi gani anapokea mshahara uleule aliokuwa akipokea miaka 20 nyuma?

Ni mbunge yupi ambaye bado anapokea mshahara, posho, marupurupu na marapurapu yake aliyokuwa akipokea miaka 20 nyuma, kama alikuwepo bungeni?

Kuna mheshimiwa waziri yupi wa Siri-kali ambaye bado anapokea mshahara uleule ambao haujaongezwa kwa miaka 20 kama pensheni ya mstaafu, nani?

Bado kuna hili rundo la waheshimiwa kutoka hili rundo la vyama vya wafanyakazi.

Bado wanapokea mshahara waliokuwa wakipokea miaka 20 nyuma? Kwa kupigania tu masuala ya waajiriwa waongezwe mishahara lakini si wastaafu ambao walikuwa waajiriwa kuongezwa pensheni yao? Kwa miaka 20 vyama vya wafanyakazi vimefanya lipi kwa wastaafu? Ina maana wafanyakazi ni pale wanapokuwa kazini wakitoa ada ya chama, lakini wakishastaafu inakuwa imetoka hiyo, ikirudi pancha?

Wale wa vile vyama visivyokuwa vya ki Siri-kali vinavyodai kuwapigania wastaafu wawe na maisha mema wakishastaafu nao bado wanapokea mishahara, marupurupu na marapurapu waliyokuwa wakipokea miaka 20 iliyopita? Mbona mstaafu wanayedai kumpigania bado anapata pensheni ya laki moja kwa miaka 20 sasa? Na wafanyakazi wameuchuna tu kama vile hawatakuja kuzeeka.

Umoja wa Mataifa je? Si walikubaliana na Siri-kali yetu na kutiliana saini mkataba kuhusu kuwalinda wazee wa Taifa, kanuni mojawapo ikiwa ni kuwapa nyongeza ya pensheni yao kila baada ya miaka miwili, mitatu ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha?

Wanajua kuwa tuna miaka 20 sasa bado tunapokea ‘laki si pesa’ wamezibwa vinywa? Si wana ofisi hapa, wanangoja hadi tuwapigie hodi na kuwaeleza madhila yetu?

Kama Taifa linatakiwa lisimame na kwa kauli moja liseme imetosha. Lisikubali wastaafu kulipwa shilingi laki moja tu kwa mwezi, wakati kila muajiriwa hatimaye atakuwa mzee na kustaafu.

Ni Kristo tu aliweza kufanya muujiza wa kukaa jangwani kwa siku 40 bila msosi. Kumtaka mstaafu aishi kwa pensheni ya Sh100,000 kwa mwezi ni kumtaka afanye muujiza wa Kristo ambao hauwezi.

Kila mmoja linamhusu. Kila mtu ana mstaafu ama baba, mama, kaka au dada. Na mnayashudia wanavyopigika.

Unganeni kuwapigia kelele wahusika wanaotajwa hapa mstaafu apate nyongeza ya pensheni yake.

Wastaafu wenyewe wa kima cha chini wako wangapi jamani? Keki ya Taifa iliwe na kila aliyehusika kuipika na isiliwe na kikundi kidogo cha watu, huku mstaafu aliyeijenga nchi akiishia kupitiwa na harufu tu.