Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TAHARIRI: Wasiovuta sigara walindwe kuepuka madhara

Jana katika gazeti hili tuliandika taarifa kuhusu athari zinazopata watu wasiovuta sigara au shisha wanaokaa karibu na wavutaji, hivyo kupata madhara kwa kuvuta moshi.

Mara nyingi wengi hujielekeza kuangalia zaidi athari kwa wavutaji wa moja kwa moja, lakini pia ni muhimu kufahamu kuwa wale wasiovuta, nao wapo hatarini.

Ingawa watu hawa hawavuti, wanapokabiliwa na moshi wa sigara, wanakumbana na madhara mengi ya kiafya. Moshi huu ambao unahusisha kemikali hatari kama vile nikotini, tar na monoksidi kabonia, unaweza kuathiri vibaya mfumo wa kupumua, moyo, na mwili mzima.

Kwa mfano, watu wasiovuta sigara wanaweza kupata matatizo ya kupumua kama vile pumu na bronkaiti ya mara kwa mara kutokana na moshi wa sigara.

Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi kwa watoto na watu wenye magonjwa ya mapafu au magonjwa ya moyo, kwani moshi huongeza hatari ya maambukizi na matatizo mengine ya kiafya.

Pia, moshi wa sigara unapotumika kwenye maeneo ya umma au katika nyumba, watu wasiovuta wanakuwa na hatari kubwa ya kuathirika na magonjwa kama vile saratani ya mapafu.

Utafiti umeonyesha kwamba watu wanaoishi na wavutaji sigara wanakumbana na hatari ya kupata saratani, hii sawa na wavutaji wenyewe.

Hali hii inaonyesha ukubwa wa athari kwa wavutaji na wale wanaopokea moshi huo kimakosa.

Tunafahamu kuwa kuna sheria inayozuia uvutaji wa sigara hadharani, hivyo ni muhimu jambo hilo likazingatiwa ili kuepusha madhara kwa watu wengine.

Madhara haya hayawaathiri tu watu wazima, bali pia watoto wachanga na watoto ambao hawajazaliwa.

Ni dhahiri kuwa jambo hili linatishia afya ya vizazi vijavyo, hivyo kuna haja ya kuwepo mikakati ya kuhakikisha jamii inakuwa salama kutokana na tishio hilo ili kulinda afya zao.

Tunaona ni muhimu jamii kuelimishwa kuhusu madhara ya moshi wa tumbaku, hasa katika maeneo ya starehe na maeneo ya kijamii ambako wavutaji na wasiovuta hukutana.

Ni wazi kwamba, ili kupunguza athari hizi, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa. Elimu ya umma inatakiwa kuwa endelevu ili kuhakikisha watu wanatambua hatari zinazohusiana na moshi wa sigara na shisha, hasa kwa wasiovuta.

Pia, sheria na sera zinazodhibiti maeneo ya kuvutia sigara na shisha, zinapaswa kuimarishwa, na zitekelezwe kwa umakini ili kulinda afya za watu wasiovuta.

Sheria iliyopo itakuwa na maana zaidi na manufaa kwa wananchi, iwapo mamlaka zinazohusika zitasimamia utekelezaji wake kikamilifu na kuwachukulia hatua wale wote wanaoonekana kwenda kinyume na kuhatarisha maisha ya wengine.

Lakini la umuhimu zaidi, wavutaji wanatakiwa kuweka kipaumbele kwa kujali afya ya watu wanaowazunguka kwa kujiepusha na kuvuta tumbaku kwenye maeneo ya umma.

 Jambo hili linatakiwa kuchukuliwa hatua madhubuti kwa wale wote wanaovuta ili kuepusha madhara kwa watu wengine wanaowazunguka. Tuwe waungwana kufuata sheria zilizopo bila shuruti.