Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tatizo la rushwa litafutiwe dawa

Rushwa imekuwa changamoto inayoikumba jamii katika nyanja mbalimbali, zikiwamo za taasisi binafsi na Serikali.

Mbali na suala la rushwa kuonekana kuota mizizi kwa baadhi ya askari wa usalama barabarani ambao wamekuwa wakishirikiana na madereva wa daladala kutekeleza vitendo hivyo, hata katika sekta nyingine ni janga la kitaifa.

Taarifa za kukamatwa kwa askari wawili wa usalama barabarani kwa madai ya kupokea rushwa, zilizozungumziwa juzi na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ni ishara ya kuanza kwa hatua muhimu za kupambana na vitendo vya rushwa vinavyotia doa Jeshi la Polisi.

Tunafahamu kuwa, rushwa siyo tu inaathiri ufanisi wa usalama barabarani, bali pia imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na Serikali kwa jumla.

Kamanda Muliro amesisitiza kuwa, jeshi hilo halitavumilia vitendo vya aina hiyo vinavyodhalilisha taswira ya jeshi na Serikali.

Katika hilo, Serikali inatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuzuia rushwa, kama vile kuboresha utendaji kazi wa vyombo vya sheria na kutoa mafunzo ya uadilifu kwa wahusika wa sekta zote.

Kwa mujibu wa madereva, utoaji wa rushwa kwa askari wa usalama barabarani ni sehemu ya utaratibu wa kila siku ili kuepuka adhabu kama faini au kukamatwa kwa magari yao.

Malalamiko ya madereva kuhusu maombi ya fedha kutoka kwa polisi, hususan katika maeneo ya Vingunguti na Kipawa, yanaonyesha jinsi rushwa ilivyojengeka kama sehemu ya mfumo usioonekana wa utawala wa kila siku barabarani.

Hali hii inaathiri uchumi wa familia za madereva, inaongeza mzigo kwa wamiliki wa magari, na kuwaacha wasafiri wengi katika hali ya kutojiweza kutokana na mzunguko wa fedha usio na tija.

Ili kukabiliana na hali hiyo, ufundishaji wa uraia na maadili ya kijamii katika shule ni muhimu ili kuwaandaa vijana kuwa raia wema, wakiwa na uelewa wa madhara ya rushwa na umuhimu wa uadilifu katika utawala wa Taifa.

Hatua hiyo itawaandaa vijana kuwa na mtazamo sahihi kuhusu haki na usawa, hivyo kupunguza hali ya rushwa kwa jumla.

Vijana wanaweza kujifunza namna ya kuwa viongozi katika jamii zao, kufanya kazi kwa ushirikiano na kuanzisha miradi ya maendeleo na kusaidia kukuza ustawi wa jamii.

Vijana wanapojua haki zao, wanakuwa na uwezo wa kudai huduma bora na kushiriki katika mchakato wa maendeleo wa kitaifa bila kushiriki katika vitendo vya rushwa.

Tunafahamu kuwa, somo la uraia linajikita katika kuendeleza tabia za utu, uaminifu na uwajibikaji, hivyo itasaidia vijana waelewe rushwa inakosa maadili na inazuia maendeleo ya Taifa.

Aidha, ni muhimu kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya rushwa, ikiwamo kuelimisha jamii kuhusu hatua za kisheria zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

 Kampeni za kuhamasisha jamii kuzungumzia na kutoa taarifa dhidi ya rushwa pia zitakuwa na mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko chanya.

Katika kuhakikisha rushwa inatokomea, ni lazima jamii, Serikali na vyombo vya sheria vishirikiane kudhibiti mifumo hii mibaya.

Hiyo itakuwa ni njia ya kuleta maendeleo ya kweli, yatakayoleta manufaa kwa wote na kurudisha imani kwa taasisi za umma.

Jeshi la Polisi linapaswa kufahamu kuwa ushindi dhidi ya rushwa ni muhimu katika kujenga Taifa lenye ustawi na usawa.