Tuchukue mazuri ya Kombe la Dunia 2026
Baada ya kusubiri kwa miaka minne, hatimaye keshokutwa Alhamisi, Fainali za Kombe la Dunia linarejea tena kwa mchezo wa ufunguzi utakaozikutanisha Mexico na Afrika Kusini.
Mechi hiyo itachezwa katika Uwanja wa Azteca uliopo jijini Mexico City kuanzia saa 4:00 usiku ukikumbushia mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia mwaka 2010 uliozikutanisha timu hizo nchi Afrika Kusini na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwa mara ya kwanza katika historia, mashindano hayo yanaandaliwa na nchi tatu ambazo ni Marekani, Canada na Mexico na yatashirikisha timu za taifa 48 kutoka mabara sita tofauti.
Hapana shaka hisia za mamilioni ya mashabiki wa soka duniani kwa sasa zinaelekezwa katika Kombe la Dunia, mashindano ambayo ndio yenye mvuto na thamani kubwa zaidi na kwa miaka mingi yamekuwa ndoto kwa nchi na mchezaji mmojammoja kushiriki.
Tanzania hatujapata bahati ya timu yetu ya taifa ‘Taifa Stars’ kufuzu mashindano hayo lakini bila shaka yatafuatiliwa kwa ukaribu na kundi kubwa la wapenzi wa mchezo wa soka na hata wale ambao sio wapenda sana michezo.
Lakini pamoja na Taifa Stars kutokuwemo katika mashindano hayo, sio vibaya kama nchi ambayo mwakani itakuwa miongoni mwa waandaaji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), kujifunza na kuyabeba yale tunayoyaona yanafaa katika fainali hizo.
Miongoni mwa ambayo tunaweza kujifunza ni kufanya mechi ya mpira wa miguu kuwa tukio la burudani ambalo litamfanya shabiki ashawishike kwenda uwanjani mapema na kuchelewa kuondona mara baada ya mchezo kumalizika.
Soka linachezwa kwa dakika 90 tu hivyo kunapokuwa na matukio ya kumburudisha mtazamaji, kabla, wakati na baada ya mchezo, inakuwa ni rahisi kuvutia wengi kujitokeza kutazama mechi.
Kwa mfano katika fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, FIFA imeanzisha utaratibu wa kufanyika kwa shoo ya muziki wakati wa muda wa mapumziko kama inavyokuwa katika tukio la michezo la Super Bowl.
Jambo lingine ambalo tunaweza kulifanyia kazi kupitia darasa la kinachoendelea katika Kombe la Dunia ni uwekezaji katika huduma za usafiri kwa watu wenye ulemavu na mifumo ya kuwahudumia mamilioni ya mashabiki.
Hii ni fursa ya kuacha urithi wa miundombinu hata baada ya mashindano kuisha.
Pia tunaweza kujifunza mbinu gani bora na za kisasa za kukabiliana na changamoto za kiafnya na magonjwa ya milipuko.
Nchi za Marekani, Canada na Mexico zimeweka mikakati ya kukabiliana changamoto zinazoweza kuwa na athari kwa afya na maisha ya watu kama vile joto kali.
Mfano wa mikakati hiyo ni kujenga vituo vya maji, maeneo ya kupumzikia na huduma za kupunguza athari za hali ya hewa kwa mashabiki.
Hii inaonyesha umuhimu wa kuweka afya za watazamaji na wachezaji mbele katika matukio makubwa.
Ni jambo lililo wazi kwamba Tanzania, Kenya na Uganda ambazo mwakani zitaandaa AFCON, hazina uchumi mkubwa ambao unaweza kuzifanya ziandae mashindano hayo kwa kiwango sawa na kile cha Mexico, Canada na Marekani.
Hata hivyo yapo baadhi ya mambo kama yaliyotajwa hapo juu, yanaweza kufanywa kwa bajeti iliyopo na kuwezesha uwepo wa fainali za AFCON zenye mvuto na msisimko.
Haitokuwa jambo jema, Fainali za Kombe la Dunia kumalizika huku sisi tukiwa hatujaona lolote la kujifunza kutoka kwa wenzetu walioandaa na hata nchi shiriki.