Tumia mchango wa harusi kwa malengo yake
Muktasari:
- Mwenyewe utajipa moyo na kusema “Akh! Wajinga wakubwa. Wamedonyoa donyoa...” Lakini kumbe wenzio ndo washakula. Wanadili na vikonyo na magamba tu ambavyo ndivyo vinavyobeba utajiri wa chakula, na kukuachia boya la chokaa.
Nilisema, ninasema na nitasema daima kuwa panya anatuzidi akili kwenye chakula. Anajua na kuheshimu sana virutubisho kuliko harufu au nakshi ya chakula hicho. Mfano hai utauona kwenye ghala la mahindi lililotembelewa na panya.
Mwenyewe utajipa moyo na kusema “Akh! Wajinga wakubwa. Wamedonyoa donyoa...” Lakini kumbe wenzio ndo washakula. Wanadili na vikonyo na magamba tu ambavyo ndivyo vinavyobeba utajiri wa chakula, na kukuachia boya la chokaa.
Kinyume chake hata panya asipofanya ziara ya kushtukiza humo ghalani, binadamu kwa hiyari yake hukoboa mahindi (kuondoa gamba na kikonyo) na kula ile chaki iliyobaki! Pengine anapendezwa na ugali mweupe kama pamba.
Katika miaka ya 1980 tuliletewa msaada wa mahindi ya njano wakati tulipokumbwa na kinenge. Watu waliokuwa na uwezo au nyadhifa waliugomea ugali wa “yanga” kwa kuamini siyo wa hadhi yao. Wengi ni wale wanaoamini kwamba paka mweusi ni mchawi na mweupe ndiye rafiki. Au malaika ni weupe kama theluji bali shetani ni mweusi kama mkaa. Imani kitu cha ajabu sana!
Lakini wataalamu wa chakula walikuja na ukweli wa kushangaza. Walisema kulingana na tafiti zao, ukiguguna pande moja kubwa cha muhindi wa njano uliochemshwa unapata gramu nne za protini, 3.5 za nyuzi lishe, 30 za wanga, 1.5 za mafuta, 3.6 za sukari na 100 za maji.
Kwa maana hiyo ukila ugali wa njano, hata kama umelumagia picha ya nguru bado utakuwa juu zaidi ya aliyekula chipsi yai miksa na kuku.
Ukweli huu unathibitisha kuwa binadamu anaishi kwa imani. Haiwezekani kula chaki (unga wa kukoboa) kwa samaki wa maboksi au viazi kwa mayai yasiyo na mama halafu bado ukaishi. Wengine wanakula mchele uliotengenezwa kwa tambi na kuku asiye na wazazi lakini anaendelea kunenepa tu.
Ni maajabu ya imani. Inaeleweka kuwa mgonjwa anayedanganywa kuwa afya yake inaimarika anaweza kuishi zaidi ya yule anayeambiwa ukweli kuwa afya yake inazidi kuporomoka.
Lakini imani ina uzuri na ubaya wake. Kule Mashariki ya Kati kulipandikizwa imani za chuki baina ya koo mbili. Tangu akiwa mdogo, mtoto wa Kiyahudi alifundishwa kulenga shabaha juu ya picha ya Mpalestina. Upande wa pili nao ukafanya vivyo hivyo. Babu wa babu zetu walishuhudia, na vining’ina wa kizazi hiki kama watakuwepo basi watashuhudia vita ya ndugu hawa isiyo na mwisho.
Mafundisho ya imani za mila, desturi na dini za pande zile mbili yalisisitiza chuki dhidi ya adui; kwani ni machukizo kwao, kwa wahenga na hata kwa Mungu. Katika hali ya namna hiyo, usipofuata mafundisho hayo nawe unageuka kuwa chukizo!
Silaha hii bado ingali inatumika kwa nguvu nyingi kwenye nchi changa (kiuchumi) kama yetu. Wapo viongozi wanaotumia mchezo mchafu wa kuwapotosha raia wao imani. Mtu anaanza kuwagawa watu kwa fedha, dini na ukabila ili kupata kundi atakalolifunga nira na kulipeleka atakako.
Watu werevu wanapoona hali hii, huanza kuwatahadharisha wenzi wao kuwa “huko tunakokwenda siko”. Lakini haraka wale viongozi wasio na weledi huwatangaza werevu hawa kuwa wachochezi na wanaokusudia kuleta vita.
Hakuna mtu anayeweza kuhimili kuona watoto wake wakiuana na kutiana vilema katika vita. Hivyo haraka anajitenga na werevu kwa nia ya kuepusha majanga. Ni afadhali kuongopewa kuliko kuletewa vita. Na kwa vile imani hufunga macho, masikio na hisia. Yule mwerevu akisema “Unapelekwa korongoni” hutakubali kufumbua macho.
Matokeo yake kunakisekana ushirikishwaji. Yanakuwa maamuzi ya mmoja na majibu ya “ndiyo” na “sawa” kutoka kwa umma. Hata kama katiba na sheria zitavunjwa, kitendo cha kuhoji kitakutupa kwenye kundi la “machukizo”.
Kwa bahati mbaya viongozi wetu wanafanya kazi kwa mazoea. Wanaamini raia ni kuku wa kuchinjwa alfajiri, hawahangaiki kukimbizana naye. Wameshatufukisha imani za kutosha, sasa wamefikia mahala pa kutuamulia jinsi mpya ya kuishi nyumbani kwetu hata kama mila na desturi zinakiukwa.
Sisi tunajua kuishi kama jamii bila kuvunja sheria. Hatuvunji sheria tunapopeana zawadi, misaada, hongera na pole. Kama ndugu, tuna kawaida ya kushirikishana kwenye shughuli zetu. Iwapo ninatarajia kumuoza mwanangu, nitasambaza jumbe kwa ndugu, jamaa na marafiki, ili tukijaaliwa tumsherehekee kwa pamoja kijana wetu.
Wapo watakaonipa michango ili kufanikisha shughuli hiyo adhimu. Najua kwamba nikisema “Asanteni lakini michango yenu nimekarabati choo cha Shule” nitachafua hali ya hewa. Maadamu nilichangisha kwa minajili ya kufungisha ndoa, basi ilibidi nifanye hivyo japo Shule ni kitu cha msingi zaidi.
Hili lililotokea Arusha limenishangaza sana. Nikadhani Wameru na Wamasai wana tamaduni tofauti na zetu. Iweje watu watoe rambirambi kwa wenzi wao baada ya msiba mkubwa wa wanafunzi, walimu na dereva, kisha mamlaka ziamue kutumia rambirambi hizo kukarabati Hospitali?
Tunaamini mfarijiwa ndiye mtu wa mwisho katika maamuzi ya faraja anazopewa. Kama Serikali ya Mkoa ilishindwa kuliombea fedha tatizo lao kutoka Serikali kuu, ingetangaza harambee nasi tungeichangia.