Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana kugeuka ombaomba mitandaoni aibu

Vijana ni taifa la kesho. Ni msemo ambao mara nyingi hutumiwa na wazee, wakiamini kuwa taifa wanalolijenga litakuwa salama mikononi mwa kizazi kijacho.

Vijana wanawekewa viwango vya matumaini kuwa watakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha wanapojitafutia kipato. Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, hali halisi inaonesha kuwa badala ya kujenga taifa linalotegemea vijana, baadhi yao wamegeuka kuwa ombaomba na tegemezi kwa viongozi.

Kwenye mitandao ya kijamii, kwenye kurasa za watu mashuhuri, vijana wengi wamekuwa wakiomba fedha na msaada wa vitu mbalimbali, jambo ambalo ni aibu na linahitaji kushughulikiwa haraka.

Binafsi naona tabia hii imeongezeka baada ya baadhi ya viongozi kujibu jumbe za vijana hao ninaothubutu kuwaita ombaomba na kuwapatia kile wanachohitaji.

Na tatizo hili limeongezeka zaidi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumjibu msichana Beatrice aliyeomba cherehani.

Tukio hilo limekuwa chachu ya vijana wengi kufuata nyayo na sasa imekuwa kawaida kuona maoni mengi ya ombaomba kwenye machapisho ya Rais Samia na viongozi wengine.

Kwa mfano, katika kurasa za Rais Samia, maombi ya ombaomba ni mengi; kila mmoja anaomba na kutamani bahati imwangukie siku hiyo, si tu kujibiwa, bali pia kuhakikishiwa kupatiwa kile anachohitaji.

Nimekuwa nikijuliza hivi tunajenga taifa la aina gani tunaposhuhudia ongezeko la vijana ombaomba?

Tabia hii haiko kwenye kurasa za Rais Samia pekee; hata katika ukurasa wa Instagram wa Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, hali ni vivyo hivyo.

Maombi ya aina zote yamekuwa yakijitokeza, ikiwa ni pamoja na maombi ya vocha, fedha za matumizi au msaada wa kifedha kwa shughuli mbalimbali.

Mfano mwingine ni ombi la kijana aliyesema kamaliza chuo aliyesema, “Shikamoo mama, (akajitaja jina), nimemaliza chuo naelewa kuna changamoto ya ajira mama, nimetafuta kiasi fulani cha hela nimelipia fremu ila nimekosa hela ya kuweka mzigo ofisini, maana natengeneza furniture na kuuza, naomba mtaji mama (akaweka namba ya simu) nipo Moshi KCMC.”

Maombi kama haya yanapopewa majibu na baadhi yao kufanikiwa kupata kile walichoomba, yanazidi kuchochea watu wengi kuendelea kuomba wakitumaini siku moja watafanikiwa.

Swali tunalopaswa kujiuliza ni je, hii ya kusaidia mmoja mmoja itazaa matunda tunayotarajia au tunachochea zaidi ombaomba?

Ni wakati wa kufikiria mikakati ya kuwasaidia vijana kwa njia endelevu, badala ya kuwapa Sh5,000 au Sh10,000, tuwape ujuzi wa pamoja ambao utawasaidia kujikwamua kiuchumi. Tuchukue hatua za kuongeza ajira na fursa zaidi ili vijana waweze kujipatia kipato halali na kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Ingawa jitihada zinafanyika, kama vile ajira katika sekta za elimu na afya na kuongeza nguvu kazi katika taasisi mbalimbali, bado kuna pengo kubwa.

Idadi ya wanaoajiriwa ni ndogo ukilinganisha na wale wanaomaliza vyuo kila mwaka, na hivyo wengi wanabaki mitaani bila ajira.

Hali hii inawafanya vijana kuangalia njia mbadala za kujipatia kipato, ikiwemo nje ya taaluma zao, na wengine kufeli kutokana na kukosa ujuzi.

Pia inachangia vijana wengi kugeuka ombaomba, wakiwa na matumaini kuwa siku moja watafanikiwa kupata kile wanachohitaji.

Ukipitia maoni kwenye machapisho ya viongozi, utaona si wote wanaomba hela na wengine wanatafuta ajira kwa kutaja taaluma zao.

Hii ni ishara tosha kwamba tunahitaji mabadiliko makubwa katika namna tunavyoshughulikia suala la ajira na ustawi wa vijana wetu.