Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dengue itibiwe kitaalamu, si vinginevyo

 Yapo maswali mengi ya msingi ambayo yanaulizwa kuhusu ugonjwa huu ambao unaelezwa kuwa unaenezwa na jamii ya mbu wanaouma wakati wa mchana.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Ni vyema, ieleweke kuwa watu wa aina hii kama huyu anayejiita nabii wa dengue anayepatikana Dar es Salaam, hawafai kuachiwa waendelee na ghiliba zao za kuwapotosha wananchi na jamii kwa njia yoyote ile.

Nchi yetu inapita katika kipindi kigumu wakati huu kutokana na ugonjwa wa homa ya dengue ambao awali ulidhaniwa kuikumba Dar es Salaam, lakini sasa umeenea katika maeneo mengi.

Tangu kuzuka kwa homa hii, hatua mbalimbali zimechukuliwa baada ya vyombo vya habari kuongoza kampeni ya kuutaarifu umma kuwapo kwa ugonjwa huo uliosababisha vifo na wengie wengi kugundulika kuupata.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imechukua hatua zikiwamo za kupuliza dawa hadi kwenye mabasi yaendayo mikoani, kazi ambayo ilitarajiwa kumalizika jana.

Tumeambiwa na wataalam wa afya kwamba ugonjwa huo ulizuka kwa mara ya kwanza nchini mwaka 2009 na ukajitokeza 2011, mwaka jana na tena mwaka huu, ingawa mara zote hatua zilizochukuliwa zimekuwa za dharura. Yapo maswali mengi ya msingi ambayo yanaulizwa kuhusu ugonjwa huu ambao unaelezwa kuwa unaenezwa na jamii ya mbu wanaouma wakati wa mchana.

Tunachukua nafasi hii kupongeza hatua zote ambazo zimechukuliwa na zaidi na vyombo karibu vyote vya habari kwa kuueleza umma kuhusu ugonjwa huu unavyoambukiza na namna ya kujikinga.

Dengue ni ugonjwa ambao una athari kubwa kwa maisha ya watu wengi, mijini na vijijini na mwingiliano wa Watanzania unaweza kusambaza ugonjwa huo haraka. Tunashauri wachunguzi wakaze kamba katika utafiti wao ambao utaonyesha uhusiano baina ya jamii mbalimbali za mbu na jinsi uhusiano huo unavyoweza kuchangia katika kupunguza ugonjwa huo miongoni mwetu.

Lazima tukubali kuwa madhara ya dengue kwa maisha ya Watanzania hayawezi kufidiwa.

Pamoja na pongezi, tunasikitika kuona baadhi ya watu wachache wameanza kujitokeza na kudai kwamba wanaponyesha homa hii ya dengue, tena kwa njia rahisi na nyepesi.

Ni vyema, ieleweke kuwa watu wa aina hii kama huyu anayejiita nabii wa dengue anayepatikana Dar es Salaam, hawafai kuachiwa waendelee na ghiliba zao za kuwapotosha wananchi na jamii kwa njia yoyote ile.

Tunaungana na hatua ya uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kwa kukemea haraka vitendo vyovyote vya kuhamasisha ukiukwaji wa kanuni za kupambana na ugonjwa huo na kutafuta njia za mkato kama anavyohamasisha mtu huyo anayejiita nabii na wengineo wanaojaribu kupotosha wananchi.

Tunashauri watu kama hawa wasipewe nafasi hata kidogo katika jamii yetu na serikali haina budi kuweka mkakati wa kuhakikisha kuwa watu hao hawapati nafasi ya kujitangaza na wagonjwa hawaruhusiwi kutoka hospitalini bila ya kufuata taratibu, huku juhudi zaidi zikiongezwa katika elimu ya afya na tiba kupambana na ugonjwa huo.

Tunaheshimu imani za dini zote na viongozi wa kiroho, lakini kwa kuwa tunaishi katika ulimwengu wa mwili, lazima masuala yanayohusu afya ya mwili yashughulikiwe kwanza kwa taratibu zilizowekwa kitaalamu na baadaye watu waendelee na imani zao, hasa kwa magonjwa ya milipuko kama dengue.

Hatutarajii sasa viongozi wa serikali kuanza kufunga safari kuelekea kwa nabii huyo kama ilivyokuwa wakati ule wa kikombe cha Mirerani kwa kuwa kufanya hivyo kutaaminisha watu na kuwafanya wapuuze ushauri wa kitaalamu.

Pia, watu kama hao popote walipo washughulikiwe haraka , tiba zao kama ile ya nabii Yaspi zizuiwe.

Haiwezekani kutumia juisi yake kuponya dengue, inafaa tiba hii bandia ipigwe marufu haraka na ikiwezekana mhusika akamatwe na kuchukuliwa hatua zikiwamo za kisheria.

Inafaa wananchi wawe makini na mambo kama haya ambayo yanajitokeza kila mara.

Haiingii akilini kuona watu wakipotoshwa na mtu kwamba anaponya dengue au ugonjwa wowote kwa juisi ambayo haijafanyiwa uchunguzi wowote wa kisayansi.Jambo hili halikubaliki, halifai kuachiwa liendelee kufanyika na sisi kama wananchi ndiyo tunaoweza kukomesha mambo ya ulaghai kama haya.

Watanzania wakatae ulaghai wa watu hao watambue kuwa dengue haina tiba, ila inaponyeshwa kwa urahisi kwa kufuata ushauri wa kitaalam wa kutoruhusu mazalia ya mbu, kusafisha mazingira na wale wanaohisi homa wakimbilie hospitali, vituo vya afya kwa uchunguzi.