Dunia imempoteza shujaa Nelson Mandela

Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela. Picha na Maktaba
Muktasari:
Hadi mauti yanamkuta Mandela alikuwa ni alama ya juu duniani kwa kupinga ubaguzi wa rangi kwani alifungwa kwa miaka 27 na kutoka jela mwaka 1990 akipinga utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwapo nchini Afrika Kusini.
Mzee Nelson Rolihlahla Mandela alifariki dunia juzi nyumbani kwake, Mtaa wa Houghton, Johannesburg, Afrika Kusini akiwa na miaka 95. Mandela alikuwa ni rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini ambaye aliliongoza taifa hilo kuanzia mwaka 1994 hadi 1999 baada ya kukaa jela miaka 27 ikiwa ni adhabu aliyopewa na watawala dhalimu wa nchi hiyo kwa kupinga utawala wao wa ubaguzi wa rangi.
Kwa muda mrefu sasa, Mandela alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya mapafu, ambapo mwaka huu alilazwa hospitalini kwa muda wa miezi mitatu, lakini baadaye madaktari walimruhusu aendelee kupata matibabu akiwa nyumbani kwake.
Hata hivyo, tangu siku ya Jumatano wiki hii kulikuwa na pilikapilika nyingi nyumbani kwa Mandela, hali iliyoashiria kunaweza kutokea tukio kubwa.
Ni kweli, juzi Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kwa majonzi makubwa alitangaza Nelson Rolihlahla Mandela, Madiba amefariki dunia.
Zuma alitangaza kifo cha Mandela na kusema kuwa kiongozi huyo mwenye historia ya pekee katika Bara la Afrika amepumzika kwa amani.
Hakika nguzo imara imeondoka. Familia imepoteza baba. Afrika Kusini imepoteza mtu muhimu, Afrika imepoteza mtu muhimu, Dunia imepoteza mtu muhimu, Dunia inahuzunika imepoteza mtetezi wa wanyonge.
Mandela atakumbukwa kwa mengi, lakini kubwa zaidi ni kitendo chake cha kupigania uhuru wa taifa la Afrika Kusini lililokuwa likiongozwa kwa misingi ya ubaguzi wa rangi. Aliongoza kampeni ya uhuru kwa ujasiri mkubwa na kujitolea maisha yake.
Hadi mauti yanamkuta Mandela alikuwa ni alama ya juu duniani kwa kupinga ubaguzi wa rangi kwani alifungwa kwa miaka 27 na kutoka jela mwaka 1990 akipinga utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwapo nchini Afrika Kusini.
Baada ya Mandela kutoka jela mwaka 1990 na kushinda uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini na hivyo kuwa rais mpya wa nchi hiyo 1994 hadi 1999, watu wengi walitarajia Mandela angelipiza kisasi kwa makaburu kwa kuwafanyia vitendo vya ubaguzi wa rangi, lakini Mandela hakufanya hivyo ila alihimiza umoja, upendo na demokrasia huku akisisitiza haki sawa kwa watu wa rangi zote katika nchi ya Afrika Kusini.
Ni wazi Mandela ametufundisha na ametuachia mambo mengi, kubwa likiwa ni kusamehe na kuwa tayari kujitolea maisha kwa ajili ya wengine katika dunia hii, pia Mandela ametufundisha kuwa na matumaini ya kile tunachokipigania badala ya kuwa waoga.
Tunaitakia familia ya Mandela, raia wa Afrika Kusini na watu walioguswa na kifo cha Mandela moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kikubwa cha msiba wa Mzee Mandela.
Tunasema hivyo kwa sababu tunafahamu kufa ni lazima. Wanapokufa watu kama Mandela huacha majonzi na hofu, lakini wanaobaki wanatakiwa kuwa na moyo mkuu, kuelewa kwamba kifo cha mtu kama Mandela kiwe na majonzi kiasi gani, siyo mwisho wa dunia.
Tunaamini maisha lazima yaendelee, lakini njia moja muhimu ya kumuenzi Mandela ni kudhihirisha kwa vitendo kwamba ni kweli tupo tayari kusamehe, kupigania wanyonge na kuwa na matumaini ya kile tunachokipigania badala ya kuwa waoga. Dunia imempoteza shujaa Nelson Rolihlahla Mandela, Madiba.
Mola ailaze roho ya Mandela mahali pema peponi. Amina.