Tamasha la Pasaka lisambaze ujumbe wa upendo kidini

Rebeca Malope kutoka Afrika ya Kusini akitumbuiza katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye tamasha la pasaka mwaka jana
Muktasari:
Mfano mzuri ni Tamasha la Filamu kwa Nchi za Jahazi, ZIFF, hufanyika kila mwaka Zanzibar na hutoa fursa kwa watengezaji na watayarishaji wa filamu kuonyesha kazi zao za filamu.
KUMEKUWA na matamasha mengi ya muziki wa kila aina na mambo mbalimbali hata michezo ambayo wengi hutumia fursa hiyo kujifunza na kupata mambo mapya kujiendeleza.
Mfano mzuri ni Tamasha la Filamu kwa Nchi za Jahazi, ZIFF, hufanyika kila mwaka Zanzibar na hutoa fursa kwa watengezaji na watayarishaji wa filamu kuonyesha kazi zao za filamu.
Hii ni fursa nzuri kujifunza kutoka kwa mataifa mengine, iwe kwa wasanii wetu wakongwe ama wachanga na kutoa kitu bora ama kuboresha kazi zao kabla ya kuziingiza sokoni.
Juzi juzi kulimalizika Tamasha la Muziki la Sauti za Busara lililofanyika Zanzibar, limetoa fursa kwa wasanii mbalimbali kuonyesha kazi zao na katika siku zote, vikundi zaidi ya 40 vilionyesha kweli inawezekana.
Kila mmoja amekuwa katika mlengo wake kuonyesha kuwa nini kinafanyika na nini kifanyike katika kuendeleza eneo hilo.
Hivi karibuni, kumetangazwa kufanyika kwa Tamasha la Pasaka la muziki wa injili litakalofanyika jijini Dar es Salaam Machi 31.
Mara nyingi hushirikisha wasanii mchanganyiko wa hapa nchini na Afrika Mashariki na Kati. Hii inapendeza, na ni fursa nyingine kwa wasanii wa mlengo huu wa injili pia kujifunza.
Lakini ni wakati sasa wa tamasha hilo na mengine yanayofanana na hilo kutumia fursa hiyo kutangaza amani na upendo miongoni mwa Watanzania bila kujali rangi, kabila, dini na mahali wanapoishi.
Katika siku za karibuni, kumekuwa na mashambulizi ya viongozi kwa viongozi wa dini na wakati mwingine vifo kama ilivyokuwa kwa Padre Evarist Mushi wa Zanzibar huku Katibu wa Mufti wa Zanzibar Fadhili Soraga akimwagiwa tindikali.
Vilevile kulikuwa na mauaji ya Mchungaji wa Kanisa la Pentecoste Assemblies of God Tanzania (PAGT), Buseresere, Wilaya ya Chato, Mathayo Kachila ambaye aliuawa kutokana na vurugu za kidini, Geita mkoani Mwanza.
Vurugu za kidini zilizotokea Mbagala, Geita, mauaji na kila suala linalohusisha vurugu za imani, lazima kukemewa kwa nguvu zote na kila mmoja afahamu kuwa vita vya kidini, moto wake ni kama wa nyika.
Kuna mataifa ambayo hadi leo hali ni tete. Kuna mataifa yanayojutia hali ilivyo na ninaamini kuna baadhi ya watu ama taasisi zinapandikiza mbegu za chuki kwa wahusika ili kuiharibu amani iliyopo.
Haiwezekani. Tukiwa tunaelekea miaka 52 ya Uhuru halafu tuanze vita ya kidini, ni mbaya kwa kweli. Ninamini wale wasioitakia mema taifa ndiyo hao wanaoshangilia kinachotokea sasa katika ardhi ya Tanzania.
Inapendeza, katika siku za karibuni, viongozi mbalimbali wa kidini wamekuwa mstari wa mbele kuhubiria na kuhakikisha kunakuwepo na amani, kila mmoja anahubiri amani na ninaamini kwa waelewa watakuwa wameelewa.
Kwa upande mwingine, hii ndiyo nafasi kwa wasanii, waimbaji, watayarishaji wa muziki wa injili kujipanga mapema hata kutunga nyimbo za kuhubiri amani, umoja upendo na mshikamano.
Pamoja na kwamba ni muda mfupi, lakini wapo wazoefu kama Rose Mhando, Christine Shusho na wengine kama watashiriki, watakapokuwa ukumbini watumike kutengeneza mashairi mapya ama katikati ya nyimbo zao kuzungumzia kulaani mauaji na vurugu za kidini.
Ni vema pia wasanii si wa muziki wa injili tu, hata ladha nyingine, wanaposhiriki kwenye matamasha, wakumbuke kuwa ni muhimu kuangalia maslahi ya taifa kwa kutunga nyimbo za kuhamaisha amani, umoja, upendo na mshikamano kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Itapendeza kusikia wakiimba amani na nini cha kufanya kwa hali iliyopo badala ya kushangilia hili la kualikwa kwenda kutumbuiza jukwaani bila kuwa na mlengo na mtazamo wa nini kifanyike kukabiliana na hali hiyo.