Tujenge utamaduni wa kuunga mkono wasanii wetu

Diamond akiwa na Zari
Muktasari:
Kuwa mshabiki maridhawa sio jambo baya, maana kushabikia wakati mwingine ni hamasa kwa yule anayeshabikiwa, na ushabiki ndio humpa motisha anayeshabikiwa kufanya mazuri zaidi ili asiwaangushe mashabiki wake.
Moja katika mambo ambayo wadau wa tasnia ya sanaa tumefanikiwa kuyafanya kwa umakini katika kipindi chote cha mwaka huu ni ushabiki. Watanzania ushabiki tunauweza na tunaweza kuwekeza muda na nguvu kazi katika hili.
Kuwa mshabiki maridhawa sio jambo baya, maana kushabikia wakati mwingine ni hamasa kwa yule anayeshabikiwa, na ushabiki ndio humpa motisha anayeshabikiwa kufanya mazuri zaidi ili asiwaangushe mashabiki wake.
Ila sasa kuna wakati tukae na kufikiria tunashabikia nini hasa, tunachokishabikia kina tija gani kwetu, kwa tasnia ya sanaa na hata kwa Tanzania kwa ujumla. Tunapaswa kushabikia ya maana na yenye maslahi kwa taifa letu kwa sababu sanaa ni kioo cha jamii. Tukiona wasanii wanavurunda, tunapaswa kuwaasa na kuwarudisha katika mstari na si kuwashabikia katika mabaya na maovu.
Wapo watu wanaojenga majina kutokana na kashfa na masuala ya uhusiano. Huwa tunashabikia sana na hufurahia kusikia msanii fulani katembea na fulani ama kafumaniwa, hayo ndiyo mambo yenye mashiko katika jamii yetu hivi sasa, watu wanpenda kuzungumzia habari za watu na wala si masuala mazito ya kimaslahi.
Mfano ambao uko dhahiri ni maisha ya kila siku ya mwanamuziki Nasib Abdul, wengi mnamjua kwa jina la Diamond ambaye juzi tu ametoka kufanya maajabu katika tunzo za muziki za Channel O, kwa kunyakua tunzo tatu kati ya nne alizotajwa kuwania.
Mashabiki wake wengi hawaangalii anachoimba wala anachofanya, wengi wameweka macho yao katika maisha yake hasa ya kimapenzi kwamba aliwahi kuwa na mpenzi huyu na huyu na huyu, huku wakimuongelea na kujenga timu katika mitandao ya kijamii za kumsifia na za kumsema vibaya.
Kwa mtazamo wetu hii haina mantiki, mahusiano ya kimapenzi au yoyote yale ni maisha binafsi ya mtu na tunapata wasaa wa kuyajua kwa sababu tu huyu anayeyafanya anajulikana kwa jamii nzima kutokana na kazi yake nzuri ya kisanii anayoifanya lakini kimsingi hayatusaidii kitu.
Haya hufanywa na mtu yeyote yule na inawezekana kuna mtu anabadilisha wapenzi kila siku kwenye jamii yetu sema tu kwa sababu hana jambo kubwa analolifanya litakalosababisha tumjue ndio maana habari zake hatuzisikii.
Ushauri wetu kwa wadau wa sanaa wiki hii ni kuwaunga mkono wasanii wetu na wawakilishi mbalimbali katika kila wanalolifanya katika kuhakikisha wanaipeperusha bendera ya nchi nje ya mipaka yake. Haya mambo binafsi ya kimaisha tuwaachie wenyewe.
Ukiangalia kwa makini utakuta wanamuziki wetu wanakubalika sana nje ya mipaka ya nchi na huko wanapigiwa kura ambazo kwa mfano, leo tunajivunia tunzo tatu za Diamond, wakati alipigiwa kura nyingi na washabiki wake kutoka Rwanda na Burundi. Hii inadhihirisha ule msemo maarufu usemao kuwa ‘Nabii hathaminiwi kwao.’ Kwanini sisi tusiwe mfano wa kuwafikisha wanamuziki wetu kwenye kilele cha mafanikio?
Wiki hii tunaye Idris Sultan ambaye anawania taji la mchezo wa Big Brother Africa, tujitahidi kwa pamoja, kwa kila njia kuhakikisha kwamba tunampigia kura na anachukua taji na kuipeperusha bendera ya taifa letu kimataifa. Tuthamini vyetu vinavyotuwakilisha.