Azam yaipiga bao Simba

Sunday June 19 2022
Mkandala PIC
By Thomas Ng'itu

SIKU chache baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba kiungo fundi wa mpira wa Dodoma Jiji, Cleophas Mkandala alikuwa kwenye rada za Simba, hali imebadilika baada ya fundi huyo kutua Azam ili kwenda kuliziba pengo la Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyepo Yanga kwa sasa.

Habari za ndani kutoka kwa mtu wa karibu wa Mkandala zinasema kuwa, kiungo huyo na mabosi wa Azam wameshamalizana na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa Ligi Kuu Bara ili atambulishwe rasmi.

Inaelezwa awali mezani kwa mabosi wa Azam kulikuwa na majina ya viungo wawili, Aziz Andambwile na Mkandala lakini wakaona kwanza wamalizane na kiungo huyu wa Dodoma Jiji.

Mmoja wa watu wa karibu na mchezaji huyo aliliambia Mwanapoti kuwa, mabosi wa Azam hawataki kuliweka jambo hilo hadharani kwa sasa kwa vile wanafanya mambo yao kimyakimya.

“Mkandala ataenda Azam kwani ameshamalizana nao kwa kiasi kikubwa na kilichobaki mkataba wake ukimalizika atatangazwa,” kilisema chanzo hicho.

Mkataba wa Mkandala na klabu yake ya Dodoma Jiji unatarajiwa kumalizika Julai 15 na mkataba ambao amesaini na Azam utaanza rasmi kufanya kazi Julai 1.

Advertisement

Mchezaji huyu kutua kwake Azam anaenda kuongeza nguvu katika eneo la kiungo ambalo baada ya kuondoka Salum Abubakari kumekuwa na ingia toka katika nafasi hiyo akicheza Kenneth Mguna, Mudathir Yahya, Frank Domayo au Never Tigere.

Mkandala ni miongoni mwa wachezaji wenye muhimili mkubwa katika kikosi cha Dodoma Jiji katika eneo la kati hivyo kuondoka kwake kutawafanya walima zabibu kutafuta mbadala wake haraka.

Kiungo huyu pia ilikuwa inaelezwa anahitajika na klabu ya Simba chini ya kocha, Pablo Franco lakini kuondoka kwa kocha huyo kumevuruga dili lake la kutua Msimbazi.

Advertisement