Miraji kumrejesha Okwi Msimbazi?

PALE Msimbazi kulikuwa na mfalme mmoja tu. Emmanuel Arnold Okwi. Alifanya alivyotaka na hakukuwepo mtu wa kumchulia hatua za kinidhamu.

Aliwachukiza mashabiki wa Simba na viongozi alipoenda kwao Uganda kwa mapumziko. Okwi alichelewa kurudi na kukosa programu za timu mwanzo wa msimu.

Hakuwepo mtu wa kumfanya chochote. Mashabiki walimsema vibaya na viongozi walishindwa kumwadhibu. Okwi alifanya vituko kama hivyo si chini ya mara moja.

Lakini alipoingia uwanjani kuitumikia Simba, aliwafanyia kile kitu wanachotaka, mashabiki na viongozi walisahau maumivu yote aliyowasababishia. Aliwafunga midomo, aliitendea haki jezi ya timu yake.

Mwaka 2013, Okwi aliondoka Simba kwa mara ya kwanza baada ya klabu hiyo kumuuza Etoile du Sahel ya Tunisia.

Mashabiki wa Simba walisikitika sana lakini hawakuwa na la kufanya kutokana na uamuzi huo wa viongiozi wa Simba chini ya Ismail Aden Rage. Mfalme aliondoka na kuacha majonzi. Watu walisahau mabaya yake yote, wakazikumbuka chenga zake na mabao yake ya mbali.

Wakati Okwi akiondoka Msimbazi, Simba na Yanga zilikuwa zikimgombania beki kutoka Rwanda, Mbuyu Twite.

Mwenyekiti wa Simba Rage alikwenda Rwanda, kufanya mazungumzo na beki huyo kwa ajili ya kutua Msimbazi.

Rage alikubaliana na Twite na kumpa kiasi cha pesa, kisha akapiga naye picha. Ndicho kitu alichoambulia. Mwenyekiti wa Usajili wa Yanga wakati huo, Abdallah Bin Kleb akamzidi kete Rage na kwenda kumchukua na kumshusha Jangwani Twite.

Hilo lilikuwa bao kwa Yanga dhidi ya Simba. Twite alitua Dar es Salaam akiwa na jezi namba nne ya Yanga, nyuma likiandikwa jina la Rage.

Kwa kuandikwa jina hilo, Yanga ilisawazisha lile bao la beki, Victor Costa ‘Nyumba’ alipochukuliwa na Simba nyumbani kwa Jamal Malinzi, huku mgongoni likiandikwa jina la Malinzi (aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga wakati huo).

Simba iliingia msimu wa Ligi Kuu 2014 katika raundi ya kwanza ikiwa haina huduma ya Okwi. Ilicheza dhidi ya Yanga katika mchezo ambao ilikuwa na wachezaji wengi chipukizi.

OKWI MPYA AIBUKA

Simba ikiwa na makinda wengi, ahai akiwemo Edward ‘Edo’ Christopher iliisumbua sana beki ya Yanga. Katika mchezo huo wa Oktoba 18, 2014, Edo alimtesa sana Twite, kama mwamuzi angetenda haki, beki huyo angepata kadi nyekundu au angeisababishia penalti timu yake.

Bahati nzuri mechi iliisha bila ya kupatikana kwa mbabe, lakini Simba iliamini haikuwa tena na haja na Mganda, Emmanuel Okwi. Kiwango alichokionesha Edo kilikuwa jibu tosha.

EDO APOTEA

Bahati mbaya sana, mechi hiyo ndio ilikuwa ya kwanza na ya mwisho kwa Edward Christoper kuonesha kiwango cha Okwi.

Mengi yanazungumzwa. Wapo wanaodai Edo alivimba mabega na kuwa staa mkubwa sana, akaendekeza starehe kiasi cha kupoteza uwezo wake.

Lakini wapo wanaopingana na hilo. Inadaiwa Edo alichanganywa na mmoja kati ya viongozi wa Simba (jina tunalo). Inadaiwa kiongozi huyo alimdhulumu pesa za usajili mchezaji huyo kwa kumuona bado kinda.

Lakini baada ya kuonesha kiwango kikubwa dhidi ya Yanga, Edo akaukataa unyonge wa kudhulumiwa pesa zake, akakoromea kiongozi huyo kudai haki yake. Kiongozi akatumia madaraka yake vibaya, akamwambia ‘tuone kama utacheza tena?’ Kilichofuata ni Simba kumpoteza Mtanzania mwenye uwezo kama wa Emmanuel Okwi. Mtoto wa watu akachanganyikiwa na kuamua kusepa zake Kagera Sugar.

Edo alionesha hasira zake kwa kuifunga Simba katika mchezo wa mwisho wa msimu wa 2017/18. mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli. Siku hiyo Simba ilikuwa ikikabidhiwa ubingwa wa Ligi Kuu. Edo akatia mchanga kwenye pilau.

OKWI NI YULEYULE

Simba ikahangaika sana kumtafuta mrithi wa Okwi, haikumpata.

Lakini furaha ilirejea tena Msimbazi mwaka 2014. Maisha ya Tunisia yalimshinda Okwi. Labda, hakuweza kuyafanya vibweka kama alivyokuwa akivifanya Simba. Mwaka huohuo alirudi kwao, Uganda kuitumikia Sports Club Villa. Baadaye akatua Yanga.

Alidumu na Yanga kwa miezi michache tu, mwanzoni mwa mwaka 2014 akarejea kwenye ufalme wake pale Msimbazi. Kikubwa Okwi hakuwa amebadilika kitabia. Alikuwa yuleyule. Akawatesa tena mashabiki na viongozi wa Simba kwa tabia zake zilezile. Lakini pia hakuacha kuwapa furaha ile waliyoitaka.

Simba ikamuuza tena Denmark kwa Klabu ya SønderjyskE Fodbold. Huko nako mambo yalikuwa ni yaleyale, hakuweza kudumu. Labda hakuwa akibembelezwa kama pale Msimbazi. Hakuonesha uwezo wake. Akaona isiwe tabu akarudi kwenye kituo chake cha mapumziko, Sports Club Villa. Bado Simba haikuwa imempata mrithi wake, mwaka 2017 akarudi Msimbazi. Akaitendea haki kwa kuifungia mabao 16 katika msimu ulioisha.

NDIO MWISHO WA OKWI?

Kabla msimu huu haujaanza, Okwi akaamua kumaliza ufalme wake pale Simba, safari hii yeye aliamua kutafuta maisha mengine Uarabuni. Akajiunga na Al Ittihad Alexandria Club.

Kama kawaida aliwaacha mashabiki wa Simba na baadhi ya viongozi wakiwa bado wanaihitaji huduma yake, aliwaachia majonzi, tena wakiwa.

AVAA VIATU VYAKE

Kabla ya kuanza msimu huu wa Ligi Kuu, Miraji Athuman alionesha cheche zake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Song kwa kusababisha penalti.

Katika mchezo huo alitokea benchi na kusababisha penalti iliyosawazisha bao ililofungwa kwa penalti ya Erasto Nyoni. Watu waliamini kama Kocha wa Simba, Patrick Aussems angemwanzisha tangu mwanzo mambo yangekuwa tofauti.

Kwenye Ligi Kuu msimu huu, mashabiki wa Simba wakaamini wamempata Okwi mpya. Ndani ya mechi nne tu, staa huyo wa kimataifa wa Uganda alianza kusahauliwa. Miraji ‘Sheva’, kinda wa zamani wa Simba ndiye aliyechukua ufalme wa Okwi pale Msimbazi.

Hiyo ni kutokana na kiwango alichokionesha staa huo aliyechukuliwa kutoka Lipuli ya Iringa.

Uzuri wa Miraji, anaweza kutokea pembeni (kama Okwi), anaweza kupasua msitu wa mabeki na kusababisha madhara, ni kama Okwi tu, ambaye ubora wake ulikuwa ukielekea ukingoni kutokana na umri.

Ndio, Okwi alishapungua makali yake lakini Miraji anaonekana ndio kwanza anaanza ni kama Okwi wa mwaka 2010 aliyejiunga Simba akiwa moto wa kuotea mbali.

Miraji alifunga katika mchezo wa kwanza dhidi ya JKT Tanzania akitokea benchi. Akafunga tena dhidi ya Mtibwa Sugar kwa shuti la mwana ukome, akitokea benchi. Katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar alisababisha penalti akitokea benchi.

Akarudia kufunga dhidi ya Biashara Shinyanga akicheza kikosi cha kwanza na alitoa asisti kwa Meddie Kagere. Unataka nini tena?

Mashabiki wa Simba wameanza tambo juu yake. Wanachosubiri ni John Bocco apone ili aungane na Sheva na Kagere kutengeneza utatu mtakatifu.

NJIA ALIZOPITIA

Miraji alianzia soka lake Kikosi B cha Simba chini ya Kocha Selemani Matola akiwa makinda wengine enzi hizo kina Abdallah Seseme ( sasa Kagera Sugar), Edo (Ruvu Shooting), Ramadhani Singano (TP Mazembe), Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla (Simba).

Mbali na Simba B, alipitia Sifa United, Soccer Rangers ya na alipotoka Simba alijiunga na Toto Africa, Mwadui ya Shinyanga hatimaye akatua Lipuli ya Iringa.

NDIO KAZI YAKE

Inaonekana Miraji amezaliwa kwa ajili ya kufunga. Hiyo ndio starehe yake kubwa anapokuwa uwanjani. Kufunga na kusababisha mabao kwa wengine, hebu angalia rekodi yake ya mabao hapa.

Akiwa na Toto Africa aliifungia mabao saba, Mwadui FC (manne) na Lipuli (saba). Hii ni kuonesha aliweza kufunga bila ya kuwa na msaada wa wachezaji wenye uwezo mkubwa, akiwa katika timu za kawaida. Itakuwaje akiwa Simba?

ATAFUNGA MANGAPI?

Msimu wa Ligi Kuu 2017/ 18 Okwi aliibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu akiwa na mabao 19,na msimu wake wa mwisho, aliifungia Simba mabao 16 huku Meddie Kagere akifunga mabao 23, Bocco akiwa na 18. Sheva atafunga mangapi hadi kufikia mwishoni mwa msimu huu?

Ukipiga hesabu kutokana na wastani wake wa sasa wa mechi nne za Ligi Kuu akiwa amefunga mabao matatu, Miraji anaweza kufunga mabao 28+. Hiki kitu kinawezekana au kisiwezekane na anaweza kumpa changamoto straika hatari wa Simba, Kagere.

Lakini kwa makisio ya kawaida, kama Kocha Aussems atamtumia vizuri, winga huyo anaweza kufunga mabao 16 hadi 20.

Je, Okwi atarudi tena Simba? Jibu la swali hilo litatokana na kiwango cha Miraji katika msimu huu wa Ligi Kuu. Kama Miraji atavimba makwapa na kujiona ni staa mkubwa au figisufigisu za viongozi wa soka zitamuondoa kwenye reli, basi bila shaka, Simba na Taifa Stars zitampoteza Okwi wa Tanzania. Kama hayo yakitokea, labda Okwi anaweza kurejea kwenye kiti chake cha ufalme pale Msimbazi. Tusubiri tuone!