Vigogo katika hesabu tofauti Mabingwa Ulaya

Vigogo katika hesabu tofauti Mabingwa Ulaya

Muktasari:

  • Mechi nane za Ligi ya Mabingwa Ulaya leo katika viwanja na miji tofauti zinaweza kulainisha au kuongeza ugumu kwa baadhi ya timu kutimiza lengo la kucheza hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.

London, England. Mechi nane za Ligi ya Mabingwa Ulaya leo katika viwanja na miji tofauti zinaweza kulainisha au kuongeza ugumu kwa baadhi ya timu kutimiza lengo la kucheza hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.

Nafasi ambayo timu hizo kila moja ipo kwenye makundi manne yanayokamilisha raundi ya tatu, inalazimisha kila moja kutoka na pointi tatu leo, ili ama ijiweke katika mazingira mazuri na rahisi ya kusonga mbele ama kuzidi kujiweka pabaya na kubakia kutegemea bahati ya raundi tatu za mwisho.

Mechi inayoweza kuwa na mvuto na msisimko mkubwa ni ile ambayo itazikutanisha Chelsea itakayokuwa nyumbani katika Uwanja wa Stamford Bridge kukabiliana na AC Milan.

Baada ya kuvuna pointi moja katika mechi mbili za kwanza dhidi ya Dinamo Zagreb na RB Salzburg, Chelsea inahitaji ushindi wa nyumbani ili uwafanye watoke mkiani mwa kundi hilo na kusogea ama hadi kileleni au katika nafasi ya pili jambo litakalofanya nafasi ya kufuzu 16 bora kuwa wazi kwa timu zote za kundi hilo E.

Lakini ikiwa AC Milan inayoongoza kundi hilo itapata ushindi wa ugenini leo, itafikisha pointi 19 na hivyo itahitaji kushinda mechi moja tu kati ya tatu itakazobakiza ili iende hatua inayofuata.

Mchezo mwingine wa kundi hilo leo utakuwa ni baina ya Dinamo Zagreb inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu ambayo itakuwa ugenini kukabiliana na RB Leipzig.

Ushindi wa nyumbani leo dhidi ya Shakhtar Donetsk, utawafanya mabingwa watetezi Real Madrid kufikisha pointi 10 na kujikita zaidi kileleni mwa msimamo kundi F na hivyo watabakia na kibarua cha kusaka pointi moja tu katika raundi tatu za mwisho ili wasonge mbele mapema.

Huko Austria, wenyeji RB Leipzig watawakaribisha Celtic ambapo kila timu itakuwa ikisaka ushindi wake wa kwanza kwenye mashindano hayo msimu huu.

Baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-3 dhidi ya watani wao wa jadi, Manchester United, juzi Jumapili kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England, Manchester City leo watakuwa nyumbani kuwakaribisha FC Copenhagen ambapo ushindi utawafanya wafikishe pointi 10 na kuzidi kujichimbia kileleni mwa kundi lao G lenye pia timu za Sevilla na Borussia Dortmund ambazo nazo zitakutana leo.

Hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa Juventus iwapo itashindwa kuibuka na ushindi nyumbani leo dhidi ya vibonde wa kundi H, Maccabi Haifa ya Israel.

Kichapo au sare kwa Juventus ambayo haina imepoteza mechi mbili za mwanzo kwenye kundi hilo, yatakuwa ni matokeo ambayo yataziweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya 16 bora, timu za Benfica inayoshika nafasi ya pili na vinara PSG ambazo nazo zinakutana leo huku kila moja ikiwa imevuna pointi sita.