Wamefunga katika Kombe la Dunia wakiwa wadogo

Wamefunga katika Kombe la Dunia wakiwa wadogo

Muktasari:

  • Kufunga bao kwenye fainali za Kombe la Dunia ni heshima kubwa kwa mchezaji kuifikia katika kipindi chake wakati akiutumikia mchezo huo.

Doha, Qatar. Kufunga bao kwenye fainali za Kombe la Dunia ni heshima kubwa kwa mchezaji kuifikia katika kipindi chake wakati akiutumikia mchezo huo.

Na hilo linakuwa tamu zaidi kama akifanya hivyo akiwa na umri mdogo kama walivyofanya Pele, Lionel Messi na Michael Owen. Wanasoka hao mahiri ni miongoni mwa nyota waliofunga mabao wakiwa na umri mdogo kwenye Kombe la Dunia, huku Pele akiweka rekodi ya kufunga akiwa na umri chini ya miaka 18.

Hii hapa chini orodha ya wanasoka waliofunga mabao wakiwa na umri mdogo kwenye fainali za Kombe la Dunia. Nani ataingia kwenye rekodi hizo kwenye fainali zitakazofanyika mwaka huu huko Qatar? Ni suala la kusubiri.

10. Constantin Stanciu - miaka 19, siku 92 - 1930

Stanciu alifunga kwenye mechi hiyo kama alivyofanya mchezaji mwenzake Kovacs wakati Romania ilipoichapa Peru 3-1 kwenye mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia. Alikuwa mfungaji wa 10 kwenye michuano hiyo, lakini yeye na Kovacs walisambaratishwa na Uruguay, ambao walikuwa mabingwa wa fainali hizo na hivyo kutupwa nje ya michuano.

9. Martin Hoffman - miaka 19, siku 88 - 1974

Hoffman alicheza mechi zote sita za Ujerumani Mashariki kwenye Kombe la Dunia 1974 - ikiwa ni fainali pekee ambacho nchi hiyo ilishiriki. Straika huyo alifunga kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Chile na aliweza kuisaidia pia Ujerumani Mashariki kushinda Medali ya Dhahabu kwenye Olimpiki 1976. Hoffman ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa na umri mdogo kufunga Kombe la Dunia.

8. Divock Origi - miaka 19, siku 65 - 2014

Nyota wa Liverpool alionyesha kiwango bora kwenye fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil, ambapo alifunga bao la ushindi dakika ya 88 dhidi ya Russia akiwa na Ubelgiji kwenye Kundi H. Hilo lilikuwa moja kati ya mabao matatu ya Origi kwenye kikosi cha Ubelgiji, lakini anaweza kuwa na wakati mzuri wa kuongeza mabao mengi kama atafaguliwa na Roberto Martinez huko Qatar.

7. Julian Green - miaka 19, siku 25 - 2014

Staa huyo wa Marekani, Green alifunga bao matata kwelikweli dhidi ya Ubelgiji, ambapo lilikuwa la kwanza kwenye timu yake ya taifa. Hata hivyo, bao hilo haliwakuzuia Marekani wasitolewe kwenye hatua ya robo fainali ya fainali hizo za Brazil. Green hakuwa na maisha marefu kwenye timu ya taifa, alicheza mechi 16 tu na mara ya mwisho ilikuwa 2018.

6. Lionel Messi - miaka 18, siku 357 - 2006

Messi mechi yake ya kwanza kwenye Kombe la Dunia ilikuwa dhidi ya Serbia huko Ujerumani, 2006. Na hakika mechi hiyo ni ya kukumbukwa kwake, ambapo aliingizwa dakika 15 za mwisho, ambapo kwanza alitengeneza asisti moto kwa Hernan Crespo kabla ya yeye mwenyewe kufunga bao. Sasa atakwenda Kombe la Dunia 2022 huko Qatar akiwa na umri wa miaka 35.

5. Dmitry Sychev - miaka 18, siku 231 - 2002

Sychev alifanya kama alivyofanya Owen kwenye Kombe la Dunia baada ya kuwapiga bao maridadi kabisa Ubelgiji na hivyo kujikuta akipachikwa jina la “Michael Owen wa Russia”. Kiwango chake katika fainali hizo zilizofanyika Mashariki ya Mbali, Sychev alijikuta akipata dili la kutua Marseille, lakini Lokomotiv Moscow ndiko alikofanikiwa zaidi, akifunga mabao 74 kwenye mechi 224.

4. Nicolae Kovacs - miaka 18, siku 197 - 1930

Staa huyo wa Romania alikuwa mchezaji wa 11 kufunga bao kwenye Kombe la Dunia wakati alipofunga katika mechi ya tatu mwaka 1930. Kovacs aliifungia mabao sita Romania, lakini bao lake dhidi ya Peru liliweka rekodi kwenye Kombe la Dunia licha ya kwamba alifanya hivyo mbele ya mashabiki 2,549 tu. Kovacs ni mmoja wa wafungaji makinda kwenye Kombe la Dunia.

3. Michael Owen - miaka 18, siku 190 - 1998

Wakati huo, Michael Owen alikuwa akiibukia Liverpool na hakika alikwenda kuwasha moto kwenye Kombe la Dunia 1998 huko Ufaransa na bao lake la kwanza alifunga dhidi ya Romania. Lakini, bao la pili lilikuwa na mvuto zaidi, alilowafunga Argentina, huku akiingia kwenye rekodi ya wachezaji wenye umri mdogo kuwahi kufunga mabao kwenye fainali za Kombe la Dunia.

2. Manuel Rosas - miaka 18, siku 93 - 1930

Beki huyo wa Mexico alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo kufunga bao kwenye Kombe la Dunia ambapo rekodi yake ilidumu kwa miaka 28 baada ya kufunga mara mbili dhidi ya Argentina. Bao lake la kwanza lilikuwa la mkwaju wa penalti na hiyo ndiyo penalti ya kwanza kufungwa kwenye Kombe la Dunia na akafunga la pili, lakini Mexico ilichapwa 6-3.

1. Pele - miaka 17, siku 239 - 1958

Mwanasoka bora wa zama zote, Pele alijitambulisha kwenye dunia baada ya kufunga mabao sita katika fainali zake za kwanza za Kombe la Dunia 1958. Bao la kwanza alifunga kwenye robo fainali dhidi ya Wales, kabla ya kufunga hat-trick dhidi ya Ufaransa kwenye nusu fainali na mawili kwenye fainali dhidi ya wenyeji Sweden, kuisaidia Brazil ikishinda ubingwa kwa mara ya kwanza.