Yatakayombeba Mandonga leo

Dar es Salaam. Rekodi, hamasa ya mashabiki na maandalizi ni vitu vinavyotarajiwa kumbemba, bondia namba moja nchini kwenye uzani wa Cruiser, Karim Mandonga usiku huu atakapopanda ulingoni nchini Kenya.
Mandonga atazichapa na Mganda, Kenneth Lukyamuzi, pambano la ubingwa wa PST la uzani wa lightheavy litakalopigwa kwenye Uwanja wa Ndani wa Kasarani, jijini Nairobi.
Mtanzania huyo ambaye jana alipima uzito na afya, anawania ubingwa wake wa kwanza tangu alipoingia kwenye ndondi miaka minane iliyopita, japo hakuwa na muendelezo bora hadi 2022, aliporejea upya ulingoni na tambo zake kukubalika kwa mashabiki licha ya kupigwa mara kadhaa.
Katika miezi ya karibuni, Mandonga alibadili mfumo wake wa mazoezi na kushinda mfululizo mapambano mengine mawili likiwamo la Daniel Wanyonyi lililompa umaarufu nchini Kenya.
Kwa mara ya pili, Mandonga leo atapanda ulingoni nchini humo, pambano ambalo licha ya kucheza ugenini, tayari amejizolea mashabiki wengi ambao wanatajwa kumuongezea morali ya ushindi licha yakuwa ugenini.
Rekodi za kidunia nazo zinambeba Mtanzania huyo mwenye nyota moja akiwa nafasi ya 244 kati ya 1184 kwenye uzani wa cruiser, mpinzani wake akiwa wa 400/1531 kwenye uzani wa middle, wote wanatumia zaidi mkono wa kushoto (orthodox), na Mandonga amelazimika kushusha uzani huku mpinzani wake akipandisha ili wazichape katika ule wa juu mwepesi (kilogramu 81).
Tofauti na mazoezi yake ya nyuma, msimu huu bondia huyo alibadili ratiba ya mazoezi ambayo kambi yake inaamini yamefanyika kwa ubora, yakimjenga na yanakwenda kumpa matokeo bora leo ambaye matokeo ya mapambano matano ya karibuni, ameshinda matatu kwa RTD (kona ya mpinzani alisalimu amri), pointi na TKO, alipigwa moja na jingine lilivunjika, wakati mpinzani wake alishinda mara nne na kupigwa moja.
“Nimejipanga kufanya vizuri, Mganda atake atapigwa asitake atapigwa tu,” alisema Mandonga anayetarajiwa kucheza raundi 12, likiwa ni pambano lake la kwanza la ubingwa kucheza kwa dakika 36.
Akizungumza kutoka Kenya, bosi wa PST, Emmanuel Mlundwa alisema maandalizi yanaendelea vema na mabondia wote Watanzania wamewasili Kenya.