Al Ahly yaendeleza ubabe kwa Yanga

Muktasari:
- Al Ahly wamefuzu na pointi 12 baada ya kushinda mechi tatu na kutoa sare tatu huku Yanga akimaliza na pointi 8 sawa CR Belouizdad wakiwa na tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Dar es Salaam. Yanga ikiwa kwenye Uwanja wa Cairo International, imeonyesha kiwango cha juu, lakini ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly.
Huu ulikuwa mchezo muhimu wa kutafuta nafasi ya kinara wa Kundi D, ambapo sasa ni rasmi Ahly imemaliza ikiwa kileleni na pointi 12, Yanga ikibaki nafasi ya pili na pointi nane na zote zilishafuzu hatua ya robo fainali.
Makosa waliyofanya mabeki wa Yanga dakika ya 46 ya mchezo, yalitosha kuipa Ahly ushindi huo mwembamba kwa bao safi lililofungwa na Hussein Shehata.
Yanga ambayo ilianza mchezo huo bila kiungo wake, Maxi Mzengeli ambaye hata kwenye benchi hakuwepo, ilionyesha kiwango kizuri lakini kwa dakika zote tisini ilishindwa kutikisa nyavu za mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho aliumia na kutoka ambapo aliingia Salum Abubakar 'Sure Boy' kucheza kwenye nafasi yake na kuwapa nafasi Ahly ya kushambulia kwa kasi lakini dakika tisini zilimalizika kwa ushindi huo mwembamba.
Katika mchezo mwingine, CR Belouazdad ambayo ilichapwa mabao 4-0 na Yanga wiki moja iliyopita, imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Medeame na kumaliza katika nafasi ya tatu ya kundi hilo ikiwa pointi nane sawa na Yanga.
Mabao ya CR yalifungwa na Raouf Benguit, Leonel Wamba na Jallow na kuwafanya Medeama wamalize mkiani na pointi nne.