Aliyewahi kuwa kocha wa Simba afariki

Kocha wa zamani wa viungo wa Simba, Adel Zrane amefariki dunia huku chanzo cha kifo chake kikiwa bado hakijafahamika.
Kwa mujibu wa klabu aliyokuwa akiifundisha kabla ya mauti kumfika, APR ya nchini Rwanda, imethibitisha kufariki kwa kocha huyo kupitia mtandao wake wa kijamii 'Instagram'.

"Tunasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa kocha wetu wa viungo Zrane, sababu ya kifo chake bado haijafahamika. Pumzika kwa amani," inasomeka hivyo taarifa ya APR.
Zrane ambaye alipita Simba akiwa msaidizi wa Didier Gomes Da Rosa pamoja na aliyekuwa kocha wa makipa Mbrazili Milton Nienov, kwa pamoja waliachana na timu hiyo baada ya kutupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu wa 2021-22.

Kabla ya kifo chake Zrane alipoondoka Simba aliandika: “Kwa masikitiko makubwa naondoka nchi niipendayo Tanzania. Yametimia. Muda umekwisha. Naipenda Tanzania nawatakia kila la heri watu wote na utawala wake.

"Tanzania itakuwa kimbilio langu la kwanza kwa likizo. Nawapenda wote na asante kwa misimu yote minne iliyopita.  Mmekuwa familia yangu ya pili, nawapenda na kuwaheshimu wote.”


Mastaa wamlilia

Wakimzungumzia kocha huyo wachezaji mbalimbali wamezungumzia nafasi waliyopata kushirikiana naye enzi za uhai wake, huku wengine wakionyesha tu kuumizwa na kifo chake.

Kiungo mkabaji wa zamani wa Simba ambaye kwa sasa anakipiga APR, Taddeo Lwanga ameposti picha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Instagram na kuandika 'Maisha ni mafupi, tumezungumza jana, sikufahamu kama utakutana na aliyekuumba leo. Pumzika kwa amani rafiki."

Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Singida Fountain Gate na sasa  Namungo, Meddie Kagere ameandika 'Ni habari mbaya pumzika kwa amani kaka yangu Zrane kila siku nitakukumbuka."