Arsenal yatwaa Ubingwa wa Dunia
Wachezaji wa Arsenal wakishangilia baada ya kutwaa taji la Dunia la Klabu za Wanawake dhidi ya Corinthians. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kwa ushindi huo, Arsenal imeingiza kitita cha Pauni milioni 1.67 (Sh5.3 bilioni) kwa kucheza mechi mbili pekee
London, England. Klabu ya Arsenal ya wanawake, imetawazwa kuwa Mabingwa wa dunia baada ya kuifunga Corinthians ya Brazil mabao 3-2 katika fainali ya Kombe la Dunia la Klabu za Wanawake. Bao la ushindi limefungwa na Caitlin Foord, akihitimisha ushindi wa kihistoria kwa washika mitutu wa London.
Arsenal, ambao walitwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei mwaka jana, walikumbana na upinzani mkali kutoka kwa mabingwa wa Amerika Kusini waliocheza kwa kasi, nguvu na mbinu za mashambulizi ya kushtukiza, wakisukumwa na mashabiki wao wengi waliokuwa wamejitokeza kwa wingi uwanjani.
Hata hivyo, uzoefu wa soka la Ulaya na kikosi kipana cha nyota wa Arsenal uliwapa faida, na hatimaye wakaibuka washindi katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani wa hali ya juu.
Arsenal walianza mchezo kwa kasi na kupata bao la mapema kupitia Olivia Smith, lakini Corinthians walisawazisha kupitia Gabi Zanotti baada ya kupeleka presha kubwa langoni mwa Arsenal.
Mshambuliaji wa Arsenal, Caitlin Foord, akishangilia baada ya kufunga bao la tatu katika ushindi wa 3-2 dhidi ya Corinthians . Picha na Mtandao
Kipindi cha pili Arsenal walirejea kwa nguvu, Lotte Wubben-Moy akiirejesha timu yake mbele kwa kufunga bao la kichwa.
Hata hivyo, Corinthians hawakukata tamaa mpaka walipopata penalti ya dakika za lala salama, iliyofungwa na Vic Albuquerque na kupeleka mchezo kwenye muda wa nyongeza.
Katika muda wa ziada, mchezo uliendelea kuwa wa wazi kwa pande zote mbili, lakini shambulizi la kushtukiza la Arsenal lilizaa matunda baada ya Caitlin Foord kufunga bao la ushindi.
Baadhi ya wachezaji wa Arsenal wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 3-2 walioupata dhidi ya Corinthians. Picha na Mtandao
Kwa ushindi huo, Arsenal wameingiza kitita cha Pauni milioni 1.67 (Sh5.3 bilioni) kwa kucheza mechi mbili pekee baada ya awali kuwafunga mabingwa wa Afrika, AS FAR kwenye nusu fainali, kisha kuishinda Corinthians. Fedha hizo ni zaidi ya walizopata walipoifunga Barcelona kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Mashindano haya mapya ya FIFA, yanayokutanisha mabingwa wa mashirikisho sita ya soka duniani, yameibua mjadala kuhusu ratiba, ustawi wa wachezaji na mustakabali wa soka la wanawake. Wapo waliotilia shaka umuhimu wa mashindano hayo kutokana na msongamano wa mechi, huku wakiona yanaweza kuzinufaisha zaidi klabu kubwa zenye nguvu kifedha.
Baadhi ya wachezaji wa Corinthians, wakishangilia moja ya bao katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Klabu za Wanawake iliyomalizika kwa kupoteza 3-2 dhidi ya Arsenal. Picha na Mtandao
Baadhi ya wadau wameona kuwa Arsenal walikuwa na faida ya kucheza mashindano hayo nyumbani, bila changamoto za safari ndefu au uchovu wa maandalizi, tofauti na wapinzani wao.
Licha ya changamoto zilizopo, ushindani huo umeonesha ukuaji wa soka la wanawake kimataifa. Ligi zenye ushindani mkubwa zinaendelea kuongeza thamani ya mchezo huo, na ushindi wa Arsenal umeonesha wazi mwelekeo mpya wa soka la wanawake duniani.