Aucho ndani Yanga, aikacha Simba

Tuesday August 03 2021
yangapic
By Mwandishi Wetu

YANGA imeendelea kusuka mipango yao ya kuchukua mataji msimu ujao na sasa wako katika mazungumzo ya mwisho kabisa kumleta kiungo mwingine wa kazi, Mganda Khalid Aucho.


Aucho kama atatua Yanga basi litakuwa pigo lingine kwa Simba dhidi ya tajiri wa GSM, Ghalib Mohammed kwani Wekundu hao walikuwa wamemuweka kwenye malengo yao na hata straika Emmanuel Okwi aliwahakikishia ni jembe licha ya kushindwa kuwika Misri.


Yanga inataka kumchukua Aucho kuja kupambana na nahodha wao wa tatu Mkongomani Mukoko Tonombe ambaye alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi ya mwisho ya watani wa jadi mjini Kigoma.
Hesabu za Yanga kwa Aucho Mwanaspoti linafahamu kwamba wananchi hao wanataka pia Aucho awepo katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na muda wowote unaeza kuona picha zake kwenye insta ya Mwanaspoti akitua kwenye Uwanja wa JKN Dar es Salaam.


Yanga inajua kwamba Mukoko atakosekana katika mechi tatu za kwanza atakazokuwa anatumikia adhabu ya kusimamishwa kutokana na kadi ya kile kiwiko cha mshambuliaji wa Simba, John Bocco.


Mbali na sababu hiyo Yanga inaona Mukoko anatumika sana na kukosa ubunifu na kukosa changamoto ya mtu wa kupigania naye nafasi ndio maana wameamua kushuka jembe hilo liliachana na Makassa ya Misri wikiendi iliyopita baada ya kushindwa kufiti kwenye hesabu za Kocha.


Tayari Aucho ameshakubaliana kila kitu na wakati wowote wiki hii atatua nchini kuja kusaini mkataba na Yanga ambayo tayari imeshawasaini Wakongomani watatu, Fiston Mayele, Heritier Makambo na Djuma Shaaban.

Advertisement


Usisahau pia kuna Jimmy Ukonde kutoka Msumbiji na wazawa, David Brayson(KMC) Dickson Ambundo(Dodoma Jiji),Mohamed Yusuf(Biashara) ambao wote wamesaini mkataba wa miaka miwili.


Yanga imepania kuja na kikosi kipya cha kwanza na sasa wanapambana kukamilisha sajili hizo ili kuwahi muda wa Shirikisho la Soka Afrika(CAF) kwa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba na Yanga zitaiwakilisha Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Biashara na Azam wakienda Shirikisho.

Advertisement