Aussems kocha mpya Singida BS

Muktasari:

  • Timu  ya Singida Black Stars imemrudisha Tanzania kocha wa zamani wa Simba Patrick Aussems na kumpa mkataba wa mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Singida Black Stars imethibitisha kuingia mkataba wa mwaka mmoja na kocha wa zamani wa Simba Patrick Aussems.

Taarifa iliyotolewa jioni hii Juni 7, 2024 na kusainiwa na Ofisi ya Afisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Jonathan Kasano imesema Aussems atakuwa kocha mkuu wa timu hiyo kuanzia msimu ujao.

Aussems, ataanza kazi rasmi Julai Mosi ambapo sasa ataendelea na majukumu ya kukijenga kikosi hicho kwenye eneo la usajili, akishirikiana na uongozi wa klabu hiyo.

Aussems raia wa Ubelgiji ataanza kazi na klabu hiyo ikiwa na jina jipya ikitoka kubadilishwa kutoka iliyokuwa Ihefu ya Mbarali kabla ya kuhamishiwa Singida na kuitwa Singida Black Stars.

Hata hivyo, taarifa hiyo haijaonyesha kocha huyo atakuwa na wasaidizi gani na hatma ya aliyekuwa kocha wao msimu uliopita Mecky Maxime.

Singida inakuwa klabu ya pili kwa Tanzania kumpa ajira Aussems ambaye kabla ya hapo aliifundisha Simba kwa mafanikio ikibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili na kufikisha hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.