Bruno mguu sawa Yanga, dili lake liko hivi Jangwani

Muktasari:

  • Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ambazo Mwananchi limezithibitishiwa ni kwamba vigogo wa Yanga tayari wameshamalizana na kiungo wa Singida BS Bruno Gomez wiki mbili zilizopita.

Dar es Salaam. Klabu ya Yanga inahitaji ushindi tu kwenye mechi tatu zinazofuata za Ligi Kuu ili ijihakikishie rasmi ubingwa wa ligi msimu huu lakini wakati wakiajiandaa na sherehe za ubingwa, uongozi wa timu hiyo umekamilisha mpango wa usajili wa nyota mmoja matata ambaye kila shabiki wa soka Tanzania anatamani kuona akichezea timu yake.

Nyota huyo ambaye Yanga imeshafunga hesabu za kumsajili ni kiungo fundi wa Singida Big Stars, Bruno Gomez ambaye kama mambo yataenda kama yalivyopangwa, ataonekana katika jezi za rangi ya kijani, njano au nyeusi katika msimu ujao.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ambazo Mwananchi limezithibitishiwa ni kwamba vigogo wa Yanga tayari wameshamalizana na Gomez wiki mbili zilizopita alipokuja Dar es Salaam kupatiwa matibabu.

“Suala la usajili wa Gomez tulishalifunga na nakuhakikishia kama mambo yakienda vyema, msimu ujao tutakuwa naye kikosini. Huyu ni mchezaji mzuri sana na ataongeza kitu kikubwa kwenye timu yetu ukizingatia tayari ana uzoefu na soka la Tanzania na mazingira yake,” alisema mmoja wa vigogo wa Yanga.

Kigogo huyo alisema kuwa baada ya kumalizana na Bruno, kilichobakia kwa sasa ni kuanza mazungumzo na klabu yake ambayo nyota huyo kutoka Brazil bado ana mkataba wa kuitumikia timu hiyo.

Imeripotiwa kuwa usajili wa Bruno mwenye uwezo wa kupiga mipira iliyokufa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mapendekezo ya benchi la ufundi ambalo linaamini kuwa uwepo wa nyota huyo utaiimarisha kwa kiasi kikubwa kutokana na kiwango bora alichokionyesha msimu huu.

Bruno ameonyesha uwezo mkubwa wa kucheza nafasi tofauti uwanjani kwa ufanisi wa hali ya juu ambapo hadi sasa ametumika kama namba sita, namba nane, namba 10 na pia winga huku akifanya vizuri katika ufungaji wa mabao na kupiga pasi za mwisho.

Fundi huyo wa upigaji mipira iliyokufa, hadi sasa ameifungia Singida Big Stars mabao manane huku akipiga pasi za mwisho nne.

Mwanaspoti liliwatafuta viongozi wa Singida Big Stars kutaka kujua undani wa habari hizi lakini vigogo wote wa juu walikataa kutoa ushirikiano na kutaka atafutwe afisa habari wa timu hiyo.

Mwanaspoti lilimsaka afisa huyo, Hussein Massanza na amesema kiungo huyo bado ana mkataba na timu hiyo na bado anahitajika, hivyo wazo la kumuuza kwa sasa halipo.

“Bruno ana mkataba wa miaka mitatu na timu inamhitaji sana, hatuna mpango wa kumuuza kwa sasa.” alisema Hussein.

Hata hivyo, inadaiwa kwamba Yanga haitapata tabu kumnasa Bruno kwa kile kinachodaiwa uhusiano mzuri wa timu hizo.

Hivi karibuni, Singida Big Stars iliipa Yanga kipa Metacha Mnata kwa mkopo siku ya mwisho ya usajili baada ya kipa wa Wana Jangwani, Abou Mshery kuumia.

Pia, wakati Singida Big Stars ikitumia jina la Singida United iliipa Yanga kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto akiwa tayari ameshasajiliwa na Singida United.