Chikola anavyohitaji kucheza na kukua kisoka
Mshambuliaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo Singida Black Stars, Offen Francis Chikola ameeleza kuwa kukosa nafasi ya kutosha katika kikosi cha Wananchi, Yanga ndio sababu ya msingi iliyomfanya aondoke Jangwani na kwenda kujiunga na Singida Black Stars kwa mkopo.
Chikola alisema jambo muhimu kwakwe ni kupata nafasi ya kucheza na kuendeleza kiwango chake na uamuzi wa kwenda Singida Black Stars ulikuwa sehemu ya maendeleo yake kisoka.
“Kwangu mimi, jambo muhimu zaidi kama mchezaji ni kupata nafasi ya kucheza na kujiendeleza. Uamuzi wa kwenda Singida Black Stars kwa mkopo ulikuwa sehemu ya maendeleo yangu ya kisoka.
"Niliamini kuwa kupata dakika nyingi za kucheza kungeweza kunisaidia kukua zaidi, kuongeza uzoefu na kuonyesha uwezo wangu.
“Nina heshima kubwa kwa Yanga, lakini wakati mwingine mchezaji anahitaji mazingira yatakayompa nafasi zaidi ya kuonyesha kile anachoweza kufanya," alisema Chikola.
Uamuzi huo umemfanya nyota huyo kujitofautisha na wengine ambao wamekuwa wakikosa nafasi za kucheza na bado wanaendelea kusugua benchi kwenye klabu mbalimbali, jambo ambalo linachangia kushusha kiwango cha mchezaji.
Mshambuliaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo Singida Black Stars, Offen Chikola (wa pili kulia) wakati alipokuwa anacheza katika vituo vya kukuzia vipaji
Waliomshika mkono
Chikola ambaye alikulia kwenye vituo kadhaa vya kukuzia vipaji hapa nchini kama Moro Kids na Moro Youth anaeleza mchango mkubwa aliopata kutoka kwa watu kadhaa waliomshika mkono katika safari yake ya soka iliyokuwa na changamoto za hapa na pale.
“Watu wenye mchango katika maisha na soka langu ni wengi sana, lakini nikitaja wachache wa muhimu zaidi ni kama Profesa Madundo Mtambo. Baada ya kumaliza elimu yangu ya msingi, alinipokea na kunilea nyumbani kwake pamoja na familia yake kutokana na changamoto za maisha nilizokuwa napitia kipindi hicho.
“Hilo lilikuja baada ya kocha wangu, Majuto, kumuomba na kumueleza hali yangu halisi. Mbali na kunipa nafasi ya kuendelea na soka, alinipa mazingira mazuri ya kukua kama mchezaji.
“Pia Edna Lema (Kocha wa Yanga Princess) ana mchango mkubwa sana katika maisha yangu. Hadi leo amekuwa akinisimamia kama mlezi wangu na kunisaidia katika mambo mengi muhimu ya maisha na safari yangu ya soka.
"Vilevile, makocha mbalimbali, ndugu, marafiki na wachezaji wenzangu wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yangu. Kila mmoja wao kwa namna yake amechangia kunifikisha hapa nilipo,” alisema Chikola.
Mshambuliaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo Singida Black Stars, Offen Chikola
Alivyoonja mafanikio
Chikola anaamini kuchezea timu kubwa ni moja ya mafanikio aliyopata kwani si rahisi kutokana na njia alizopitia kuanzia Morogoro hadi kufikia kiwango alichonacho sasa.
“Mafanikio ninayojivunia zaidi ni kuona ndoto yangu ya kucheza soka la ushindani ikitimia na kupata nafasi ya kucheza katika klabu kubwa na mazingira ya kiwango cha juu.
"Pia ninajivunia hatua zote nilizopitia kutoka Morogoro hadi kufikia kiwango nilichonacho sasa, kwa sababu kila hatua imehitaji kujitolea, uvumilivu na kazi kubwa, alisema Chikola.
Mshambuliaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo Singida Black Stars, Offen Francis Chikola
Bado ndoto hazijatimia
Licha ya kufikia malengo ya kucheza katika timu kubwa hapa nchini, Chikola bado ana ndoto ya kufikia kiwango cha juu katika soka na kupata nafasi ya kucheza ligi kubwa duniani.
“Bado nina ndoto kubwa ya kufikia kiwango cha juu zaidi katika soka, kucheza ligi kubwa duniani, kushinda mataji makubwa na kuiwakilisha Tanzania kwa mafanikio makubwa katika mashindano ya kimataifa. Ninaamini bado nina mengi ya kufanya na kujifunza ili kufikia malengo hayo, “ alisema nyota huyo.
Mshambuliaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo Singida Black Stars, Offen Chikola wakati alipokuwa anacheza katika vituo vya kukuzia vipaji
Wito kwa wachezaji wachanga
Kutokana na changamoto nyingi alizopitia katika maisha yake ya soka, Chikola alitoa wito kwa vijana ambao wana ndoto za kuja kucheza soka la ushindani akiwataka kuwa wavumilivu.
“Ningependa kuwaambia wasikate tamaa hata wanapokutana na changamoto. Wawe na nidhamu, wajitume kwenye mazoezi, waheshimu makocha wao na waamini katika uwezo wao. Hakuna mafanikio yanayokuja kwa bahati; kila kitu kinahitaji kazi kubwa, uvumilivu na kujitolea kwa muda mrefu, “alisisitiza Chikola.
Mshambuliaji wa Yanga anayecheza kwa mkopo Singida Black Stars, Offen Chikola (kushoto), akiwa pamoja na rais wa Yanga, Hersi Said
Akiwa nje ya uwanja
Nyota huyo wa zamani wa TRA United anaamini maisha ya mchezaji si ndani ya uwanja pekee kwani kupitia maisha ya kawaida anajifunza vitu vingi vinavyomsaidia kufanya vizuri anapokuwa uwanjani.
“Nje ya uwanja napenda kutumia muda na familia, marafiki pamoja na watu wa karibu nami. Pia napenda kupumzika, kusikiliza muziki na kutazama mechi mbalimbali ili kujifunza mambo mapya kutoka kwa wachezaji wengine.
“Ninaamini maisha ya mchezaji hayahusiani na soka pekee, bali pia namna anavyoishi nje ya uwanja ndiyo humsaidia kuwa bora zaidi ndani ya uwanja. Kupitia maisha ya kawaida, najifunza, nakua na kupata utulivu unaonisaidia kufanya vizuri ninapokuwa uwanjani, “alieleza nyota huyo wakati akizungumza na Mwananchi.
Chikola alizaliwa Septemba 22, 1998 katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Mvomero, katika msimu uliopita ulionekana kuwa wa mafanikio kwakwe baada ya kufanya vizuri alipokuwa na Tabora United ambayo kwa sasa ni TRA United.
Katika msimu huo wa 2024-2025, Chikola alihusika katika mabao tisa ambapo alifunga saba na kutoa pasi mbili za mabao. Kutokana na kiwango hicho nyota huyo aliingia kwenye tetesi za usajili kwenda Yanga ambapo alijiunga na Wananchi hao Julai 23, 2025.
Kiungo huyo anatarajiwa kurejea Yanga ifikapo Juni 30, 2026 ambapo mkataba wake wa mkopo kuitumikia Singida Black Stars utakuwa umemalizika tangu alipojiunga na walima alizeti hao katika dirisha dogo la Januari.