Coastal Union yasitisha ubabe wa Yanga

Winga wa Coastal Union, Erick Msagati akifunga goli katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. PICHA NA MICHAEL MATEMANGA

Mshambuliaji Mudathir Abdallah hataweza kusahaulika katika vichwa vya wachezaji wa Yanga na mashabiki wao baada ya kufunga bao la ushindi kwa Coastal Union na kuipa pointi tatu.

Mudathir aliingia uwanjani dakika ya 70 akichukua nafasi ya Sultan Kasikasi aliyeumia ambapo dakika 13 baadaye akapachika bao hilo lilisitisha mechi 21 bila kupoteza katika ligi.

Bao hilo Mudathir aliwazidi akili mabeki wa Yanga na viungo wake waliokuwa wamezubaa akiachia shuti kali lililochana nyavu na kuwa bao la ushindi.

Hata hivyo Coastal Union walistahili ushindi huo baada ya kuwabana vyema wageni wao kipindi cha pili huku mwiba akiwa Hamad Majimengi ambaye kasi yake ilikuwa kwa mabeki wa Yanga.

Licha ya mabadiliko ya Kocha wa Yanga Cedric Kaze kuwatoa Farid Mussa/Deuse Kaseke hayakuweza kusaidia kitu katika kuongeza kasi ya kusaka ushindi.

Matokeo hayo ya Yanga kukubali kichapo cha mabao 2-1 kinaifanya Yanga kusubiri hatma ya viporo vitatu vya watani wao Simba.

Yanga mechi ya mwisho ya mashindano kufungwa ilikuwa Machi 12, 2020 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar na msimu huu wa 2020/21 Yanga imecheza michezo 21 na kushinda 14 ikitoka sare 7.