Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elimu itolewe kuhusu sheria, kanuni soka la Wanawake

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na taasisi zingine limetakiwa kutoa elimu kwa wadau kuhusu haki za wachezaji wa kike wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.

Sheria ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) linatoa haki hizo lakini uchunguzi uliofanywa na Mwanaspoti umebaini haifahamiki kwa wachezaji wengi, makocha na hata uongozi wa vilabu.

Mbali ya elimu inapendekezwa kuwapo uwezeshaji wa kiuchumi kwa timu za wanawake kwa kuwa nyingi hazina uwezo wa kuwalipa wachezaji kwa kukosa wadhamini.

Vilevile wadau wanasema ni muhimu kuwapo ushirikishwaji wa Serikali, mashirika na taasisi za kimataifa katika utoaji elimu kuwawezesha wachezaji kujua njia za kudai haki zao kisheria endapo mikataba yao itavunjwa au watabaguliwa kwa sababu ya ujauzito.

Kocha wa Fountain, Mirambo Kamiri anashauri: "Mamlaka itoe elimu kwa wahusika, hususani wachezaji waweze kudai haki zao kwa sababu zipo kisheria. Sheria ipo ili kumfanya mchezaji wa kike awe na muda mzuri wa kupumzika na kurudi kiwanjani akiwa na afya njema na kuonyesha kiwango kilekile.”

Ushauri kama huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Bunda Queens, Alley Ibrahim anayesema: "Kwa mtazamo wangu sheria hii iko sawa kwa sababu inampa nafasi mchezaji ya kucheza mpira na kuzaa kwa wakati mmoja."

"Ninachoweza kushauri ni kwamba, elimu inatakiwa itolewe ili sheria itekelezwe kwani wengi wetu hatuifahamu. Inabidi tupewe elimu kuanzia sisi viongozi na wachezaji,” anasema.

Mlezi wa zamani wa timu ya Baobab, Inocencia James anasema ili sheria ifanye kazi lazima kampuni kubwa zidhamini vilabu kwani itakuwa rahisi kwa timu kupata pesa za kuwalipa wachezaji.

"Lazima kuwe na mdhamini anayeeleweka, labda benki au taasisi nyingine kama ilivyo kwa soka la wanaume,” anasema.

Kocha wa timu ya Ceassia, Ezakiel Chobanka anasema ni muhimu viongozi wa timu wanapoelimishwa nao welimishe wachezaji ili wazifahamu sheria na kanuni.

"Ushauri wangu ni elimu tu kwa wachezaji na hili linaweza kufanywa na mamlaka. Wachezaji wengi hawajui sheria hii ikiwezekana katika mikataba yao kiwepo kipengele kinachoelezea hili. Fikiria tu mimi mwalimu nipo katika mpira wa miguu kwa miaka zaidi ya sita na sifahamu, vipi kwa wachezaji, wao ndio hawafahamu kabisa," anasema Kocha wa Mashujaa Queens, Ally Ally na kuongeza:

"Viongozi wanaosimamia timu za wanawake ndio wawe wa kwanza kuelimishwa, TFF wanatakiwa walitilie mkazo suala hili."


Mtazamo kiuchumi, kisheria

Kutokana na timu kueleza ukosefu wa fedha unachangia masilahi ya wacheza kutozingatiwa, mtaalamu wa masuala ya uchumi Dk Abel Kinyondo anasema njia zinazoweza kuchukuliwa ili vilabu viwe na mapato zaidi ni kuwa na udhamini kutoka kampuni na taasisi mbalimbali.

Anasema ili timu za wanawake ziweze kujikwamua kiuchumi lazima kuzingatia uweledi katika ligi.

"Kama ligi ya wanaume ilihitaji kuwa 'professional' ili kuanza kupata udhamini na timu kuwa katika hali nzuri kidogo kiuchumi, kwa upande wa wanawake inabidi wafanye mara mbili zaidi. Watu waone wachezaji, timu na mamlaka zinazosimamia zilivyo makini na kazi zao na zinavyojiheshimu,” amesema.

Dk Kinyondo amesema: "Wakifanya yote haya naamini wadhamini wataanza kumwagika, shida iliyopo ni wanawake ambao ni wachezaji kwenye ligi na wanaowasimamia wanaiga au wanapita kwenye nyayo zilezile walizopita wanaume. Hivyo watu wanaotazama mpira wanaona kama mpira wa kiume. Tazama hata wachezaji wanavyojionyesha."

Anasema katika nchi zilizoendelea watu ambao hawataki vurugu na wanajiheshimu huwa wanapendelea kwenda katika mechi za wanawake kwa sababu wanaamini ni sehemu ambayo hawawezi kukutana na vurugu au mambo yaliyopo kwenye soka la wanaume.

"Huku kwetu ni tofauti, soka la wanawake linaenda kulekule kwa wanaume hali inayosababisha wadhamini kuona ya nini kudhamini kwa watu ambao wanaigiza kuwa wanaume wakati naweza kwenda kwa wanaume wenyewe ambako pia soka limeendelea zaidi. Mwanamke ana utambulisho wake, naamini wakiamini kwenye utambulisho wao, mpira wa wanawake utakusanya pesa na udhamini wa kutosha," anasema.

Simon Patrick, aliyewahi kuwa mwanasheria wa Yanga anatoa rai kwa mamlaka kujikita katika utoaji elimu ili wachezaji waelewe sheria.

"Sheria inawapa wanawake haki ya kufanya kazi ambayo haipaswi kuondolewa kwa sababu tu amepata mimba, na hasa hawa wachezaji, mpira ni ajira yao ambayo hairuhusiwi kumnyima haki ya kuwa na familia kwa maana ya kuzaa.

Anashauri kufanyike semina ndani ya timu kuwafundisha wachezaji kuhusu haki zao ili waweze kudai pale zinapovunjwa.


Alichosema Msigwa, TFF

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, anasema Serikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limeandaa semina kadhaa kuhusu masuala ya afya ya uzazi.

Amesema pia zimezishirikisha taasisi za masuala ya afya ya uzazi kwa wachezaji wa timu za wanawake.

"Mathalani, Januari mwaka huu yalifanyika mashindano ya Gift- U17 yaliyokua chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambalo liliendesha semina kwa timu za wanawake za JKT Queens na TDS Girls Academy U15 zilizoshiriki mashindano hayo," amesema.

Amesema zipo timu za wanawake ambazo baadhi ya wachezaji wana watoto na wanaendelea na shughuli za mpira pasipo kuwa na changamoto.

Mkurugenzi wa sheria, habari na masoko wa TFF, Boniface Wambura amesema wataendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na chama cha wachezaji kwa sababu ni suala endelevu.

"Wito wangu kwa wachezaji wanaopatwa na shida kama kuvunjiwa mkataba baada ya kupata ujauzito waje wawasilishe malalamiko, wasiogope. FIFA wameanzisha sheria hizi ili kuwalinda wachezaji lakini ili tuchukue hatua lazima waseme," amesema.


Taratibu za kufuata

Kwa mujibu wa miongozo na sheria za FIFA ikiwa mchezaji anaona hajatendewa haki na timu yake wakati analea au ana ujauzito, anaruhusiwa kushtaki kwa kufuata utaratibu ufuatao:

Atatakiwa kuhifadhi baruapepe, ujumbe, nakala za mkataba, malipo na vyeti vya daktari; ushahidi utakaosaidia kudhibitisha ukiukwaji wa haki zake.

Atawasiliana na shirikisho la mpira la nchi husika au chama cha wachezaji (kama FIFPro).

Kupitia chama cha wachezaji anaweza kusaidiwa kwa kupatiwa ushauri wa kisheria au kwa upande wa shirikisho wanaweza kuchukua hatua dhidi ya timu.

Ikiwa hatua hizo hazitafanikiwa, mchezaji anaruhusiwa kuwasilisha malalamiko kwa kamati ya hadhi ya wachezaji ya FIFA.

Ikiwa utaratibu utafuatwa na timu ikakutwa na hatia inaweza kukumbana na adhabu ya kutakiwa kumlipa mchezaji fedha kama fidia, kulazimishwa kulipa haki zake na kumrejesha kazini au kutozwa faini na kufungiwa kusajili kwa kipindi maalumu.


Ushauri wa daktari

Dk Abdul Mkeyenge, mtaalamu wa masuala ya uzazi kwa wanawake anatoa ushauri kwa taasisi na wachezaji wa kike akisema: "Watambue wana haki ya kuwa na familia na kuwa na watoto, hivyo wakipata wa kuwaoa waoelewe ila tu wanaume wao waelewa mpira ndiyo maisha yao.”

Amesema wachezaji lazima waangalie namna ya kuzaa mapema kwani mwanamke anapofika miaka 45 na kuendelea anaweza kuwa katika hatari ya kutoweza kuzaa kwa sababu muda huo inakuwa ni kipindi ambacho baadhi ya wanawake wanakuwa katika ukomo wa hedhi.

"Taasisi na timu ziwe zinatoa elimu kwa wachezaji juu ya umuhimu wa kuwa na watoto au kuanzisha familia mapema," anasema.

Anashauri mwanamichezo wa kike baada ya kufanyiwa upasuaji apumzike walau miaka miwili, lakini si chini ya miezi sita.

Dk Mkeyenge anasema kupumzika kwa walau miezi sita ni kwa ajili ya kuhakikisha anamlea mtoto wake kwa ukaribu zaidi ikiwa ni pamoja na kumnyonyesha.

"Anayejifungua kwa njia ya kawaida au upasuaji wapumzike kwa muda usiopungua miaka miaka miwili ikiwa ni wachezaji, kwani katika kipindi hicho naamini miili yao itakuwa sawa kupokea mazoezi na kazi ngumu, mfano kwa wale wanaojifungua kwa upasuaji, huwa tunawapasua chini ya kitovu sasa baada ya pale huwa inawaacha na kidonda.

“Kile kidonda huwa ndani na nje. Nje huwa rahisi kupona lakini ndani huchelewa kwa hiyo kama hatapata muda mwingi wa kupumzika anaweza kujitafutia matatizo, ikiwa ni pamoja na hitilafu au wengine huwa mshono unapasuka," anasema.


Kimataifa ikoje

Barani Ulaya baadhi ya timu zina sera zinazowalinda wachezaji wa kike wakiwa na ujauzito na baada ya kujifungua.

Mfano, AC Milan huwaongezea mikataba nyota wake waliopata ujauzito katika mwaka wa mwisho wa mkataba licha ya kuwa hawatawatumia katika michezo.

Wanaporejea kiwanjani, timu hugharimia malazi na usafiri kwa watoto na wahudumu wao pale klabu inapokwenda kucheza nje ya Jiji la Milan.


Imeandikwa kwa udhamini wa Taasisi ya Gates Foundation