FIFA yamchelewesha Mayele Hispania
Muktasari:
- Mwishoni mwa mwezi uliopita, Mayele aliibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi za Ndani Barani Afrika
Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limefanya agizo ambalo linaweza kumfanya nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele kuchelewa kujiunga na Kambi ya timu ya Taifa ya DR Congo itakayoanza Desemba 7, 2025 nchini Hispania.
Kambi hiyo ni kwa ajili ya maandalizi ya DR Congo kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizopangwa kuanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Agizo hilo la FIFA ni la kuziruhusu klabu kutowaachia wachezaji wao kwa ajili ya kujiunga na timu zao za taifa zinazoshiriki AFCON hadi Desemba 14, 2025 ikiwa ni siku saba tu kabla ya kuanza kwa fainali hizo.
Uamuzi huo umekuja kufuatia presha ambayo ilianza kuzikabili klabu zinazoshiriki Ligi kubwa duniani ya kuwakosa baadhi ya nyota wao ambao walitakiwa kujiunga na kambi za timu zao za taifa mwanzoni mwa Desemba kwa ajili ya kujiandaa na AFCON.
Mayele amekuwa nyota tegemeo wa Pyramids FC hivyo kwa uamuzi huo, maana yake klabu yake itakuwa na uhakika wa kumtumia katika mechi ya Ligi Kuu ya Misri dhidi ya Petrojet, Desemba 6 na kisha mechi ya Kombe la Misri dhidi ya National Bank Egypt, Desemba 9.
Afueni kubwa huenda ikawa kwa klabu ya Sunderland inayoshiriki Ligi Kuu England ambayo sasa itakuwa na uhakika wa angalau siku 14 za Desemba, kukaa na wachezaji wake zaidi ya saba ambao wanasubiriwa kuzitumikia timu zao za Taifa kwenye AFCON 2025.
Katika hatua nyingine, kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo kwa ajili ya Fainali za AFCON 2025 kilitangazwa jana huku kukiwa na mshtuko wa kuachwa kwa nyota wa Newcastle United, Yoanne Wissa.
Wissa ameachwa kwa vile bado hajaanza kucheza mechi za kiushandani baada ya kupona majeraha yaliyomuweka nje tangu mwanzoni mwa msimu.
Kikosi hicho kina mchezaji mmoja tu anayecheza ndani ya Bara la Afrika ambaye ni Fiston Mayele.
Makipa wanaounda kikosi hicho cha nyota 26 na klabu zao kwenye mabano ni Theo Fayulu (FC Noah), Lionel Mpasi (Le Havre) na Mathieu Epolo (Standard Liège).
Mabeki ni Aaron Wan-Bissaka (West Ham), Gédéon Kalulu (Aris Limassol), Arthur Masuaku (Sunderland), Chancel Mbemba (Lille), Axel Tuanzebe (Burnley), Rocky Bushiri (Hibernian), Joris Kayembe (Genk) na Steven Kapuadi (Legia Warsaw).
Viungo ni Noah Sadiki (Sunderland), Edo Kayembe (Watford), Samuel Moutoussamy (Atromitos), Charles Pickel (Espanyol), Ngal'ayel Mukau (Lille), Mario Stroeykens (Anderlecht), Théo Bongonda (Spartak Moscow), Michelangelo Balikwisha (Celtic), Nathanaël Mbuku (Montpellier) na Brian Cipenga (Castellón).
Washambuliaji kwenye kikosi hicho ni Simon Banza (Al Jazeera), Fiston Mayele (Pyramids), Samuel Essende (Augsburg), Meschak Elia (Alanyaspor) na Cédric Bakambu (Real Betis).