Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ibenge aahidi usajili wa viwango Azam

Muktasari:

  • Kocha huyo rai wa DR Congo, alisema atafanya usajili itakapohitajika lakini anaamini kikosi kilichopo ni bora kutokana na kumaliza nafasi ya tatu na kupata nafasi ya ushiriki wa michuano ya kimataifa msimu ujao.

Dar es Salaam. Azam FC imemtambulisha Florent Ibenge kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho akichukua nafasi ya Rachid Taoussi huku akiahidi kufanya makubwa ndani ya timu hiyo.

Ibenge ambaye ametua Azam baada ya mkataba wake na Al Hilal Omdurman ya Sudan kumalizika, alisema anafurahia kupata nafasi ya kuifundisha timu ambayo ina uwakilishi wa michuano ya kimataifa huku akibainisha kuwa anafahamu katika soka la Tanzania kuna timu nyingi nzuri ikiwemo Simba na Yanga lakini watapambana nazo.

“Kama ligi ya Tanzania ni namba nne kwa ubora basi timu zilizopo zina ushindani mkubwa, nimekuja kupambana ili kufikia mafanikio na sisi Azam tupo kwenye nafasi ya ushindani,” alisema na kuongeza.

“Simba msimu huu imecheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ni namna gani kuna timu bora lakini pia kuna Yanga ambayo imetwaa mataji yote ya ndani msimu huu, nahitaji ushindani mkubwa kutoka kwao, nipo tayari kwa ushindani.”

Ibenge alisema anatambua ana wasifu mkubwa lakini hiyo haitoshi kuipa mataji Azam bila kuwekeza nguvu kwenye kujenga timu bora, huku akisema kilichomleta Tanzania ni kuipambania timu hiyo kutwaa mataji ya ndani na kimataifa.

Kuhusu usajili

Kocha huyo rai wa DR Congo, alisema atafanya usajili itakapohitajika lakini anaamini kikosi kilichopo ni bora kutokana na kumaliza nafasi ya tatu na kupata nafasi ya ushiriki wa michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Kama Azam imemaliza nafasi ya tatu ni wazi kuwa ina timu bora ingawa kuna wachezaji wanatoka, hivyo kama kutakuwa na umuhimu tutaingiza nyota wengine lakini nguvu kubwa ni kuwa na nyota waliofanya makubwa,” alisema na kuonggeza.

“Siwezi kupambana peke yangu, naomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji, viongozi na mashabiki ili niipambanie timu hii kufikia malengo, kupambana peke yangu sitaweza.”

Ibenge amesema anapenda kucheza mpira mzuri lakini pia anapenda kushinda mechi na mataji, hivyo mashabiki watarajie mambo mazuri kutoka kwake.

Akizungumzia kuhusu ni mfumo gani rafiki kwake, alisema hawezi kuweka wazi hilo ila anaamini akikaa na wachezaji wa kikosi hicho kwa muda wakimuelewa kila kitu kitakuwa wazi kwenye uwanja wa mechi.

Hadi jana, Azam ilikuwa imemtambulisha rasmi beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union, huku taarifa zikibainisha klabu hiyo imemalizana na kipa Aishi Manula, mshambuliaji Muhsin Malima huku ikiwa katika hatua za mwisho kumrudisha kiungo wao wa zamani, Himid Mao.

Katika kipindi cha misimu mitatu aliyoitumikia Al Hilal, Ibenge ameiongoza kwenye mechi 91 ambapo kati ya hizo ilishinda 55, sare 20 na kupoteza 16, huku kikosi hicho kikifunga mabao 158 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 62.

Ibenge ameiwezesha Al Hilal kushinda taji la Ligi Kuu Sudan, Kombe la Ligi (Sudan Super League) na ubingwa wa heshima wa Ligi Kuu Mauritania iliyoshiriki 2024-2025 kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyopo kwao Sudan.

Kabla ya Al Hilal, Ibengé alianza kazi ya ukocha nchini Ufaransa, alizinoa timu za ES Wasquehal na SC Douai, mwaka 2012 alipata fursa ya kuwa kocha wa Shanghai Shenhua nchini China alikokaa kwa kipindi kifupi, kisha 2014 alirudi Afrika kuifundisha AS Vita Club ya DR Congo.

Mwaka huohuo, Ibengé aliteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya DR Congo (Leopards) alifanikiwa kuipa ubingwa wa mashindano ya African Nations Championship (CHAN) mwaka 2016, hata hivyo mwaka 2017 alijiuzulu kuwa kocha wa taifa na 2019 akarudi tena AS Vita.

Mwaka 2021, Ibengé alienda Morocco kujiunga RS Berkane kama kocha mkuu ambapo msimu wa 2021/22 alitwaa Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na kikosi hicho sambamba na Kombe la Morocco, kisha 2022 ndipo alikwenda Sudan kuifundisha Al-Hilal kabla ya sasa kutua Azam.