Ihefu sasa yaitishia Simba

WAJUKUU wa Mbogo Maji hawashikiki kwenye Dimba la Highland Estates, Mbarali baada ya kuwachakaza vigogo wa soka Yanga na Azam na sasa inazipigia hesabu alama tatu kutoka kwa Simba.

Ihefu iliyoanza msimu ikiburuza mkiani kwenye msimamo wa Ligi Kuu inapiga hesabu za kumaliza nafasi tano za juu kwenye michezo mitano iliyosalia.

Katika michezo minane ya mwisho imecheza uwanja wa nyumbani imeshinda sita, ikapoteza mmoja dhidi ya Polisi Tanzania kwa mabao 2-1 Novemba 16 na sare ya bao 1-1 dhidi ya Singida Big Stars, Februari 12.

Timu nyingine iliyovuna alama tatu kwa Ihefu ikiwa nyumbani ni Namungo iliyoshinda bao 1-0, lakini tangu mzunguko wa pili uanze imepoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga ikiwa ugenini kwa bao 1-0.

Ihefu inajiandaa kuikaribisha Simba Aprili 8 ambapo Novemba 29, mwaka jana iliivunja ‘unbeaten’ ya Yanga ambayo ilicheza michezo 49 bila kufungwa.

Wanambogo Maji hao tayari wanapiga hesabu za kumaliza nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi - nafasi ambayo Geita Gold inashika kwa sasa ikiwa na alama 34 ikiizidi Ihefu kwa alama moja na zitakutana Mei katika Uwanja wa Highland Estates.

Kocha msaidizi wa Ihefu, Zubery Katwila alisema kikubwa wanachofanya kwa sasa ni kuhakikisha wanapunguza makosa wanapokuwa uwanjani hasa wanapocheza na wapinzani wenye uwezo mkubwa.

“Unapokuwa na nidhamu ya mchezo na kujua mbinu za mpinzani wako inakupa nafasi ya kwenda kutengeneza mabao ambayo mara zote yamekuwa yakizaa matunda, marekebisho tunayafanya.

“Najivunia kuwa na wachezaji ambao wana uwezo wa kutumia vyema mipira iliyokufa kwa sababu michezo kadhaa tumefaidika na mabao ya aina hii, hivyo inapotokea tunapenda kuona tunakuwa makini kuitumia,” alisema Katwila.

Hata hivyo, kocha msaidizi wa Azam, Kally Ongala alisema kitu ambacho kiliwafanya kupoteza mchezo huo ni kushindwa kutumia vyema mbinu walizokuwa wameziweka.

Azam mara ya mwisho kushinda ugenini ilikuwa Desemba 4 kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi dhidi ya Polisi Tanzania kwa bao 1-0 lililofungwa na Ayoub Lyanga ambapo katika michezo saba ugenini imeshinda mmoja, sare tatu na kupoteza mitatu.

Huo ndio mchezo wa kwanza kwa Azam kupoteza mbele ya Ihefu kwani katika michezo mitatu ya nyuma waliyokutana tangu kupanda Ligi Kuu Bara, Azam imeshinda michezo yote.