Iran yawalilia waliouawa shambulio la Marekani, ikitua Mexico
Muktasari:
- Watu wapatao 175 walifariki dunia baada ya kombora la Marekani kulenga shule ya wasichana na kuua wanafunzi hao.
Timu ya taifa ya Iran imeibua mjadala mpya wa kisiasa kuelekea Kombe la Dunia 2026 baada ya wachezaji wake kuwasili nchini Mexico wakiwa wamevaa beji maalumu za kuwakumbuka watoto waliopoteza maisha katika shambulio la kombora la Marekani mapema mwaka huu.
Wachezaji hao walionekana wakishuka kutoka kwenye ndege wakiwa wamevaa beji zilizoandikwa namba 168, ikiwa ni kumbukumbu ya watoto waliouawa katika tukio lililotokea Februari 28, 2026 mjini Minab, kusini mwa Iran.
Kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi zilizotolewa na mamlaka za Iran, watu 175 walifariki dunia baada ya kombora la Marekani kulenga eneo la kijeshi lililokuwa karibu na shule ya wasichana, lakini likagonga shule hiyo kwa makosa. Serikali ya Iran imesema wengi wa waliofariki walikuwa wanafunzi wa kike.
Hatua hiyo imekuja wakati uhusiano kati ya Iran na Marekani ukiendelea kuwa wa mvutano, huku kukiwa na malalamiko kutoka Tehran kwamba baadhi ya viongozi na watendaji wa timu hiyo walinyimwa viza za kuingia Marekani, moja ya nchi waandaaji wa Kombe la Dunia 2026 pamoja na Mexico na Canada.
Baadhi ya wachezaji wa Iran wakati wakiripoti Mexico kujiandaa na Fainali za Kombe la Dunia 2026. Picha na Mtandao
Licha ya changamoto hizo, kikosi cha Iran kimewasili Mexico na kupokelewa na mamia ya mashabiki waliokusanyika katika uwanja wa ndege na maeneo ya karibu.
Iran imeweka kambi yake nchini Mexico, ingawa mechi zake zote za hatua ya makundi zitachezwa Marekani.
Timu hiyo itaanza kampeni zake kwa mchezo dhidi ya New Zealand katika Uwanja wa SoFi, Los Angeles, kabla ya kukutana na Ubelgiji na baadaye Misri katika hatua ya makundi.
Shirikisho la Soka la Iran limelaani hatua ya kuwanyima baadhi ya viongozi wake viza, likidai kuwa ni mfano wa kuingiza siasa katika michezo.
Ubalozi wa Iran nchini Uturuki ulisema watu 15 kutoka idara za utawala na usimamizi wa timu walikataliwa kupewa vibali vya kuingia Marekani.
"Mmefikia kiwango cha juu kabisa cha ubaguzi na uonevu dhidi ya timu ya taifa ya Iran," ulisema ubalozi huo kupitia mtandao wa X, huku ukiitaka FIFA kuingilia kati suala hilo.
Balozi wa Iran nchini Mexico, Abolfazl Pasandideh, alidai timu hiyo imeelezwa kuwa italazimika kuingia na kutoka Marekani siku hiyo hiyo ya mechi zake.
Baadhi ya mashabiki wa Iran waliojitokeza kuipokea timu yao katika Uwanja wa Ndege jijini Mexico City. Picha na Mtandao
"Tunaruhusiwa kuingia asubuhi na tunapaswa kuondoka siku hiyo hiyo baada ya mechi," alinukuliwa akisema.
Hata hivyo, msemaji wa timu ya taifa ya Iran, Amir Mahdi Alavi, alikanusha madai hayo akisema wachezaji wamepewa viza za kuingia nchini humo na watakuwa wakisafiri kwenda katika miji ya mechi zao siku moja au mbili kabla ya michezo husika.
Kwa upande wake, ofisa mmoja wa Marekani amesema viza zote zinazohitajika kwa wachezaji na wafanyakazi muhimu wa timu ya Iran tayari zimetolewa ili kuhakikisha ushiriki wao katika mashindano hayo.
Hata hivyo, ofisa huyo alisisitiza kuwa Marekani haitaruhusu mfumo wa utoaji viza kutumiwa vibaya kwa madhumuni mengine yasiyohusiana na mashindano.
Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kuanza Juni 11 kwa mechi ya ufunguzi kati ya Mexico wakivaana na Afrika Kusini.