Jezi bandia 446 za Simba zakamatwa Kilimanjaro
Muktasari:
- Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watuhumiwa 11 wakiwemo wafanyabaishara wa Manispaa ya Moshi, Mkoani humo kwa kuuza na kusambaza jezi feki za timu ya Simba.
Moshi. Jeshi la polisi Mkoani Kilimanjaro linawashikilia watuhumiwa 11 wakiwemo wafanyabaishara wa Manispaa ya Moshi, Mkoani humo kwa kuuza na kusambaza jezi feki za timu ya Simba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 24, 2022 Kaimu Kàmanda wa polisi mkoani hapa, Yahaya Mdogo amesema wamekamata jumla ya jezi 446 zenye thamani ya zaidi ya Sh15.6 milioni katika opereseheni iliyofanyika kuanzia Machi 21 hadi Machi 23 mwaka huu.
"Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilipata taarifa fiche kuhusu uwepo wa wafanyabiashara wa mkoa Kilimanjaro hasa Manispaa ya Moshi wakiuza jezi feki za Timu ya mpira wa miguu ya Simba, jezi ambazo si halisi zinazotengenezwa na kampuni ya Vunjabei,"
"Kwa kushirikiana na Kampuni ya Vunja Bei kumefanyika operesheni ya pamoja kwenye maduka ya wafanyabiashara wilaya ya Moshi Manispaa na
kufanikiwa kukamata watuhumiwa 11 na jezi bandia za timu ya Simba za rangi tofauti zipatazo 446 zenye thamani ya Sh15.6 milioni" amesema Kàmanda Mdogo
Kamanda Mdogo amesema katika uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Vunja Bei, imebainika kuwa jezi hizo ni feki kutokana na kwamba hazina ubora na ni tofauti na zinazotengenezwa na kampuni hiyo ya Vunja bei iliyopewa zabuni ya kutengeneza na kusambaza jezi za timu ya Simba.
Kamanda Mdogo amesema wanaendelea na uchunguzi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.
Aidha Kamanda Mdogo amewataka wafanyabaishara kufanya biashara kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na mamlaka zinazohusika.