JICHO LA MWEWE: Azam wamepiga breki za katuni kwa akina Sure Boy?

Muktasari:

  • TUNAELEKEA mwezi mmoja sasa rafiki zetu watatu wamesimamishwa pale Azam. Salum Abuubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahaya na Agrey Morris ambaye ni nahodha wa timu. Inakuaje nahodha wa timu anasimamishwa kwa matatizo ya utovu wa nidhamu? Inashangaza kidogo. Moja kati ya sifa ya nahodha ni nidhamu.

TUNAELEKEA mwezi mmoja sasa rafiki zetu watatu wamesimamishwa pale Azam. Salum Abuubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahaya na Agrey Morris ambaye ni nahodha wa timu. Inakuaje nahodha wa timu anasimamishwa kwa matatizo ya utovu wa nidhamu? Inashangaza kidogo. Moja kati ya sifa ya nahodha ni nidhamu.

Kuna mambo matatu nyuma ya pazia. Yanajadilika. Kwanini akina Sure Boy wamesimamishwa? Inadaiwa walitoa maneno machafu kwa Meneja wa timu, Luckson Kakolaki. Sijui ilikuaje lakini binafsi nimeshangaa kidogo kwa sababu Kakolaki alikuwa mchezaji mwenzao hapo zamani.

Vyovyote ilivyo ni kwamba walimtolea maneno machafu wakafungiwa. Habari za ndani katika kile ambacho nakifahamu, Azam walikuwa wanataka kuondoa ‘ufaza’ kutoka kwa wachezaji wakongwe klabuni hapo. Hao wachezaji hapo wanaweza kuwa wachezaji waliocheza muda mrefu zaidi klabuni.

Inaonekana kwamba Azam wanamsaka mchawi katika klabu yao. Wanataka kuondokana na uchafu wote ambao umesababisha timu yao kusuasua licha ya matumizi makubwa ya pesa ambayo wamekuwa wakiyafanya klabuni hapo lakini bado wameachwa mbali na Simba na Yanga.

Miongoni mwa wanaotajwa kuwa ‘wachawi’ katika maendeleo ya timu ni hawa wachezaji wakongwe akina Sure na Wenzake. Kwamba wanaigawa timu katika makundi na huwa wanapenyeza sumu mbaya kwa wachezaji wapya wanaokuja klabuni hapo.

Hisia hizi zipo muda mrefu miongoni mwa watendaji na matajiri wa Azam kwamba kuna wachezaji wanajisikia sana na wana kundi lao ndani ya Azam. Wengine bado wapo ndani ya klabu wengine hawapo. Wasiokuwepo ndio akina Himid Mao, John Bocco na wengineo. Walioendelea kuwepo ndio hawa akina Sure Boy.

Kwahiyo hawa akina Sure Boy walikuwa wanatafutiwa kisiki tu wajikwae kisha waanguke. Operesheni hii ya kusafisha virusi ilipangwa kwa muda mrefu kwa sababu Azam wameendelea kujitafuta kujua nani mchawi wao ndani na jje ya uwanja.

Na sasa imetokea. Tatizo hapa kisichojulikana ni jambo gani linafuata baada ya hapo. Kitendo cha Azam kuwasimamisha kwa muda usiojulikana ni tatizo. TFF wanapaswa kuingilia kati. Mchezaji lazima apewe adhabu kulingana na misingi ya haki zake. Anaweza kufungiwa kwa mechi kadhaa au miezi kadhaa.

Kunfungia mchezaji au kiongozi au mwamuzi kwa muda usiojulikana ni adhabu iliyopoteza maana na misingi ya haki za Mfanyakazi. Atakuwa nje mpaka lini? Labda kama ni maisha yake yote. Labda kama ni mpaka mwisho wa mkataba. Adhabu lazima iwe na ukomo ulio wazi. Kwa hapa Azam imeteleza hata kama wachezaji walikuwa ni tatizo.

Kama wachezaji wamekuwa na nidhamu mbovu zaidi basi walipaswa kubanwa na vipengele vya mkataba ambavyo vingeuvunja mkataba wenyewe kutokana na matatizo ya utovu wa nidhamu wa mchezaji mwenyewe. Ni jambo linalofanywa na klabu mbalimbali kubwa duniani bila ya kujali hadhi ya mchezaji.

Labda Azam walipaswa kukaa mezani na akina Sure na kuvunja mikataba yao mbele ya Mameneja wao. Sidhani sana kama wachezaji wangepinga hili hasa ukizingatia kwamba kwa sasa wachezaji wenyewe hawawezi kukosa timu kubwa.

Labda hiki ndicho ambacho pia kinawahangaisha watu wa Azam katika mioyo yao. Waliwahi kufanya kosa linalofanana na hili wakati mtu mmoja alipopewa madaraka pale Azam akaamua kuweka masharti magumu ya mkataba kwa baadhi ya wachezaji wakongwe klabuni na wachezaji hao wakaamua kutimka zao.

Kama masikhara vile Azam iliwapoteza John Bocco, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe na Aishi Manula ambao walikwenda Simba na kuipa mataji manne mfululizo ya Ligi kuu huku wakiwa wachezaji muhimu klabuni hapo. Ni maamuzi ambayo Azam wanajutia mpaka kesho hata kama hawatatoka hadharani na kukiri jambo hilo.

Lazima kuna hofu pale Azam kwamba labda wakichana mkataba wa Sure Boy huenda akajongea Jangwani kutia nguvu eneo la katikati akiungana na Yannick Bangala, Khalid Aucho na Fei Toto. Yanga wataimarika zaidi ya hivi walivyo sasa ambapo tayari wanasumbua na mechi baina yao iliyopita tayari ilikuwa nzito kwa Azam.

Tayari msimu uliopita kabla hata akina Aucho hawajafika Yanga walionyesha nia ya kumtaka Sure Boy. Sidhani kama wanaweza kupoteza fursa adhimu ya kumchukua kama mchezaji wa bure endapo Azam watauchana mkataba wa staa huyo mtoto wa staa wa zamani wa klabu yao, Abuubakar Salum.

Lakini huenda pia mabosi wa Azam wanawaza itakuaje mchezaji kama Mudathir akienda kuongeza nguvu Msimbazi. Itakuwa hadithi ile ile ya akina Nyoni ba wenzake. Hii hofu lazima ipo na kama haipo nadhani Azam wangekuwa wamechana mikataba ya akina Sure muda mrefu sasa.

Agrey sio tatizo lao la msingi sana. Umri wake umegota na hata akiachwa wakubwa wenzao hawawezi kumchukua. Kwa sasa anasomea ukocha pale Karume. Labda swali la kujiuliza ni namna ambavyo mahusiano yake na Azam yanavyokaribia kuvunjika katika nyakati muhimu kama hizi.

Wote tunafahamu kwamba Agrey alikuwa na fursa ya kuanza kuwa kocha msaidizi pale pale Azam kabla ya kwenda kwingineko au kupanda kuwa kocha mkuu klabuni hapo. Inakuaje mahusiano yanakufa katika dakika hizi za majeruhi? Kama Azam wanashindwa kumuamini kama mchezaji wataweza kumuamini kama kocha?

Vyovyote ilivyo Azam wanapaswa kulimaliza suala hili mapema. Lina ladha mbaya. Akina Sure Boy watakaa nje mpaka lini? Tunahitaji kuona vipaji vyao uwanjani wakiwa na jezi ya Azam au jezi za wakubwa wengine. Maisha lazima yaendelee. Wapo wachezaji wengi wasio na nidhamu ambao waliadhibiwa na maisha yakaendelea.

Wapo wacheze wengi wasio na nidhamu ambao waliondoka klabuni na klabu ikaendelea. Hakuna mchezaji aliye mkubwa kuliko timu. Labda Azam wamng’ate Jongoo kwa kutumia meno tu. Hakuna jinsi. Vinginevyo kwa sasa ni kama wamepiga breki za katuni tu kwa mastaa hao. Ni kama vile wana hofu watakwenda kwingineko.