Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Joao Pedro afichua aliyempeleka Chelsea

Muktasari:

  • Joao Pedro alipata ushauri kutoka kwa beki wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil, David Luiz.

London, England. Mshambuliaji Joao Pedro amefichua kuwa uamuzi wake wa kutua Chelsea kwa dau la pauni milioni 60 kutoka Brighton ulitokana na ushawishi wa mshambuliaji mwenzake raia wa Brazil, Andrey Santos licha ya kwamba mchezaji huyo hajawahi kucheza hata dakika moja kwenye dimba la Stamford Bridge.

Pedro, ambaye alitambulishwa rasmi Jumatano hii kama mchezaji mpya wa Chelsea, amesema aliwasiliana na Andrey Santos kupitia Instagram kabla ya kukubali dili hilo nono:

“Nilikuwa nazungumza na Andrey kuhusu klabu, kuhusu wachezaji na maisha ndani ya Chelsea. Aliniambia mambo mazuri na nikaona ni uamuzi sahihi kujiunga,” amesema Pedro.

Andrey Santos alijiunga na Chelsea Januari 2023 lakini amekuwa akipelekwa kwa mkopo katika vilabu vya Vasco da Gama (Brazil), Nottingham Forest (England), na Strasbourg (Ufaransa). Mchezo wake pekee akiwa na jezi ya Chelsea ulitokea kwenye Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Esperance de Tunis, akicheza kwa dakika 22.

Mbali na Santos, Joao Pedro pia alipata ushauri wa kimpira kutoka kwa beki mkongwe wa zamani wa Chelsea na timu ya taifa ya Brazil, David Luiz, ingawa haikuhusiana moja kwa moja na uhamisho wake.

Kuingia kwa Pedro kumeongeza kiwango cha matumizi ya Chelsea kwenye dirisha hili la usajili hadi zaidi ya pauni milioni 200, ikiwa tayari wameshamsajili Liam Delap, Estevao Willian, Dario Essugo, Mamadou Sarr na Kendry Paez. Mchezaji huyo mwenye miaka 23 anakuja na uzoefu wa misimu mitano England akiwa na Watford na Brighton, akifunga jumla ya mabao 30 na kutoa pasi 10 za mabao katika mechi 70 alizocheza.

Pedro amejiunga na wachezaji wengine waliotoka Brighton kwenda Chelsea akiwemo Moises Caicedo, Robert Sanchez na Marc Cucurella jambo linaloashiria uhusiano wa kibiashara kati ya vilabu hivyo viwili.

Katika kutangaza usajili wake, Chelsea walitoa video ya Pedro akicheza mpira ufukweni huku muziki wa jazz wa Kibrasil ukiwa umeambatana na maneno: “Karibu Chelsea, Joao Pedro.”

Akipigwa picha rasmi akiwa amevaa jezi ya bluu, Pedro amesema: “Hii ni klabu kubwa yenye historia kubwa. Imejengwa na wachezaji wakubwa na bado ina wachezaji bora. Kuvaa jezi hii ni jukumu hapa Chelsea unapaswa kufikiria jambo moja tu: kushinda.”

Pedro sasa anatarajiwa kuonekana uwanjani katika Kombe la Dunia la Klabu, ambapo Chelsea itachuana na Palmeiras kwenye hatua ya robo fainali baada ya kuitoa Benfica katika muda wa nyongeza kwenye hatua ya 16 bora.