Kalaba hajafa, yupo mahututi

Nahodha wa zamani wa TP Mazembe na timu ya taifa ya Zambia, Rainford Kalaba yupo katika wodi ya wagonjwa mahututi huko Zambia baada ya kupata ajali ya gari iliyotokea katikati ya Kafwe na Lusaka, Zambia, leo.
Kalaba, 37, amewahishwa hospital baada ya gari ndogo aina ya Mercedes Benz aliyokuwamo ikiendeshwa na mwanamke ambaye hajafahamika kugongana na lori la mafuta.
Awali, staa huyu aliripotiwa kuwa amefariki kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TP Mazembe katika ukurasa wao wa mtandao wa Facebook kabla ya baadaye miamba hao wa Afrika kutoa taarifa nyingine iliyoeleza kwamba mchezaji huyo hajafa bali yupo kwenye hali mbaya.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Polisi la Zambia inaeleza:"“uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba ajali ilitokea baada ya gari aina ya Benz kujaribu kuipita gari nyingine bila ya tahadhari, na kusababisha kwenda kulivamia lori lililokuwa linakuja.”
Kabla ya kustaafu Julai, 2023 akiwa na Mazembe, Kalaba alikuwa tegemeo akiisaidia timu hiyo kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2015 ambalo nyota mwenzake wa wakati huo Mbwana Samatta alimaliza mfungaji bora wa michuano hiyo na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wanaocheza soka ndani ya bara hili.
Akiwa na Mazembe amewahi kukutana mara mbili na Simba. Ya kwanza mwaka 2011, kwenye Ligi ya Mabingwa katika hatua za awali ambapo walishinda mechi zote mbili, pia wakakutana mwaka 2019 katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa ambapo Mazembe ilipita kwa ushindi wa mabao 4-1 walioupata DR Congo baada ya mchezo wa mkondo wa kwanza hapa Dar es Salaam kumalizika kwa suluhu. Katika ushindi huo Kalaba alitoa asisti moja.