Kambi Yanga sasa Uturuki

Muktasari:

  • YANGA imeshtuka imeangalia ratiba ya kalenda ya mashindano ya CAF, inayoanza Agosti 12 na fasta wakaamua kubadili gia angani na kufumua mambo yote waliyoyapanga kwa maandalizi ya msimu ujao ikiwamo ishu ya kambi yao iliyopanga iwe Boston Marekani na kupelekwa Uturuki.

YANGA imeshtuka imeangalia ratiba ya kalenda ya mashindano ya CAF, inayoanza Agosti 12 na fasta wakaamua kubadili gia angani na kufumua mambo yote waliyoyapanga kwa maandalizi ya msimu ujao ikiwamo ishu ya kambi yao iliyopanga iwe Boston Marekani na kupelekwa Uturuki.

Iko hivi. Mwanaspoti liliwataarifu mapema bilionea wa klabu hiyo, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ alitaka kambi iwe jiji la Boston Marekani, huku kukiwa pia na machaguo mengine ikiwamo Uturuki au Afrika Kusini, lakini sasa imefahamika rasmi kwamba Yanga itaenda kujifua Ulaya.

Mabosi wa Yanga, sasa wanatafuta mji bora ambao watakwenda kuweka kambi hiyo ambayo hadi sasa kuna uwezekano ikawa kambi ya wiki tatu kujiandaa na msimu mpya.

Tayari Yanga imepanga kwamba wachezaji wao watakuwa na siku 10-15 za mapumziko baada ya kucheza mchezo wa mwisho wa msimu huu kwenye Fainali ya Kombe la Azam Shirikisho (ASFC) dhidi ya Coastal Union. “Hatuwezi kutoa mapumziko ya zaidi ya hapo kutokana na muda mdogo, wachezaji wakisharudi haraka timu inatakiwa kuondoka kuekekea kambini,” alisema bosi huyo.

“Tunachofanya sasa ni kuangalia mji gani utakaokuwa na mazingira bora zaidi ya maandalizi, pia uwezekano wa kupata mechi za kirafiki za kujipima nguvu. Unajua safari ya kwenda Boston hakuna uwezekano wa kupata ndege ya moja kwa moja hadi huko hivyo kuna siku za kupoteza hapa mpaka kufika huko,” aliongeza kigogo huyo.

“Hii ndio sababu kubwa hasa tunaiona haina afya kwa klabu kambi ya huko tofauti na Uturuki tutakokwenda moja kwa moja tukitokea hapa, ratiba hii ya CAF inatubana kwenye muda kutokana na ligi kuchelewa kumalizika.”

Hata hivyo, Mwanaspoti inafahamu ishu za visa kwa wachezaji wanaotoka nchi zisizo na mahusiano mema na Marekani nazo zimechangia jambo hilo.

Yanga ikitoka Uturuki itarejea moja kwa moja nchini kuanzia Agosti 4 tayari kwa maadhimisho ya wiki ya Mwananchi mbayo huenda ikafanyika Agosti 6.

Aidha wiki inayofuata tayari timu hiyo itakuwa katika maandalizi ya mwisho kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali na kwa mujibu wa kalenda ya CAF mchezo wa kwanza utapigwa kati ya Agosti 12-14, mabingwa hao wakisubiri kujua watakutana na timu ipi na wataanzia wapi.