Kina Mayele wawekewa sheria kali Misri
Muktasari:
- Ligi Kuu ya Misri inashirikisha timu 21 ambapo kwa sasa, kinara ni Al Masry yenye pointi 11 katika michezo mitano.
Chama cha Soka Misri kimeweka sheria kali ya faini za fedha kwa wachezaji au maofisa wa timu watakaojihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu au kucheza rafu kuanzia katika msimu huu na kuendelea.
Sheria hiyo tayari imeshaanza kufanyiwa kazi kwa baadhi ya wachezaji na timu katika ligi hiyo ambayo anacheza nyota wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mchezaji anayeonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kosa la utovu wa nidhamu au rafu ya hatari, anafungiwa michezo mitatu na kupewa adhabu ya fainali ya Pauni 50,000 za Misri, sawa na Sh2.6 milioni za Kitanzania.
Timu ambayo wachezaji wake kuanzia watano na kuendelea wataonyeshwa kadi za njano katika mchezo mmoja nayo itatozwa fainali ya Pauni 50,000 za Misri.
Kiasi hicho cha fedha pia kitatozwa kwa timu ambayo mashabiki wake watatumia tochi za mionzi kwa ajili ya kuwamulika wachezaji wa timu pinzani.
Kosa la mashabiki kutoa lugha chafu na udhalilishaji kwa timu pinzani, litasababisha adhabu ya Pauni 100,000 (Sh5.2 milioni) kama ambavyo itakuwa kwa timu ambayo itamshambulia refa kwa vitendo au maneno.
Tayari adhabu hizi zimeshaanza kuwa mwiba kwa timu na baadhi ya wachezaji ambao wamejihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu katika mechi za hivi karibuni.
Mfano ni beki wa Zamalek, Mahmoud Hamdy ambaye ametozwa faini ya Pauni za Misri 50,000 na kufungiwa idadi ya michezo mitatu kwa kosa la kutoa lugha chafu kwa mchezaji wa timu pinzani katika mchezo ambao timu yake ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Wadi Degla.
Wadi Degla nayo imetozwa Pauni 50,000 za Misri kwa kosa la wachezaji wake sita kuonyeshwa kadi za njano katika mchezo huo dhidi ya Zamalek.
Al Ahly imetozwa faini ya Pauni 100,000 kutokana na kosa la mashabiki wake kutoa lugha chafu kwa wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Pyramids FC.