Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinda wa miaka 15 aweka rekodi Premier

Muktasari:

  • Arsenal ina imani kubwa kwamba wamempata lulu mpya. Uchezaji wake wa kwanza tayari umeandika jina lake kwenye historia ya klabu na huenda ikawa mwanzo wa safari ndefu yenye mafanikio katika klabu hiyo ya kaskazini mwa London.

London, England. Max Dowman ameweka historia mpya kwa kuwa mchezaji wa pili mwenye umri wa miaka 15 kuichezea Arsenal katika Ligi Kuu ya England (Premier League), baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Leeds siku ya Jumamosi.

Kiungo huyo mshambuliaji alishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wa Arsenal kwenye Uwanja wa Emirates alipoingia kuchukua nafasi Noni Madueke dakika ya 64, Arsenal ikiwa tayari inaongoza kwa mabao 4-0. Dowman alionyesha uwezo mkubwa uwanjani, na alihusika moja kwa moja kwenye bao la tano la Arsenal baada ya kufanyiwa madhambi yaliyozaa penalti.

Dowman, mwenye umri wa miaka 15 na siku 229, sasa ndiye mchezaji wa pili mdogo zaidi kuwahi kuichezea Arsenal kwenye EPL, nyuma ya Ethan Nwaneri ambaye aliweka rekodi mwaka 2022 akiwa na miaka 15 na siku 181. Nwaneri pia alishiriki mechi hiyo ya Jumamosi, akicheza baada ya nahodha Martin Odegaard kuumia kipindi cha kwanza. Hadi sasa, Nwaneri ameichezea timu ya wakubwa ya Arsenal mara 38, ikiwa ni pamoja na michezo 26 ya ligi.

Kuchomoza kwa Dowman kumevutia hisia kubwa msimu huu wa kiangazi, baada ya kung’ara katika ziara ya maandalizi barani Asia, akiwavutia wengi kwa uwezo wake dhidi ya timu kama Newcastle, AC Milan na Tottenham. Katika mechi dhidi ya Newcastle, alipata penalti baada ya kumhadaa nyota wa Brazil, Joelinton.

Nyota huyo chipukizi ameshapata sifa kutoka kwa wachezaji wakubwa. Declan Rice amemtaja kuwa “mchezaji bora wa miaka 15 nchini Uingereza”, huku Odegaard akisisitiza umuhimu wa kuwa na subira naye.

“Ni mchezaji wa kipekee, mwenye kipaji kikubwa, na kila mtu amekiona hilo katika mechi za maandalizi,” alisema Odegaard. “Hatupaswi kumpa shinikizo kubwa au matarajio makubwa mno. Tunapaswa kumsaidia, kumpa muda na nafasi ya kukua kwa utulivu. Naamini atakuwa mchezaji mkubwa kwa Arsenal.”

Odegaard, ambaye naye alipata umaarufu akiwa na miaka 16 alipojiunga na Real Madrid, anasema uzoefu wake unaweza kuwasaidia Dowman na Marli Salmon, kijana mwingine wa miaka 15, kujifunza namna ya kuhimili maisha ya soka ya watu wazima.

Kocha Mikel Arteta pia amemsifu Dowman na kuahidi kuwa Arsenal itasimamia kwa makini maendeleo yake, kama ilivyofanya kwa Nwaneri na Myles Lewis-Skelly. Akiwa na urefu wa futi 6 na uwezo wa kucheza katikati au pembeni, Dowman anaonekana kuwa na sifa zote muhimu za mafanikio kimwili na kitekniki.

Walimu wake huko Hale End wamefananisha mtindo wake wa uchezaji na nyota wa zamani wa Brazil, Kaka, huku mashabiki wakitoa mlinganisho wa juu zaidi kutokana na matarajio makubwa waliyo nayo.

Ingawa hawezi kusaini mkataba wa kitaalamu hadi atakapofikisha miaka 17 mwishoni mwa mwaka ujao, Arsenal ina imani kubwa kwamba wamempata lulu mpya. Uchezaji wake wa kwanza tayari umeandika jina lake kwenye historia ya klabu na huenda ikawa mwanzo wa safari ndefu yenye mafanikio katika klabu hiyo ya kaskazini mwa London.